Mzee Kikala: Nina watoto wengi kuliko wa kwenye Kombolela

Mzee Kikala: Nina watoto wengi kuliko wa kwenye Kombolela

Wakati baadhi ya watu wakimuhurumia Mzee Kikala wa kwenye tamthilia ya ‘Kombolela’ kwa mtihani anaopitia kwa kuwa na watoto wengi wasiokuwa na maadili kwenye tamthilia hiyo. Lakini kumbe katika maisha yake ya uhalisia Kikala ana watoto wengi kuliko wa kwenye kombolela.

Tamthilia hiyo inamuonyesha Mzee Kikala ambaye jina lake halisi ni Elias Nyang’ongela akiwa na watoto sita wakubwa na wajukuu sita, lakini kila kitu wanamtegemea baba yao huyo, ikiwemo kuishi nyumbani kwake.

Ni moja ya tamthilia zinazoangaliwa sana kwa sasa, kutokana na kuigiza maisha ambayo familia nyingi za Uswahilini zenye maisha ya chini zinaishi.

Katika mahojiano maalumu ya Mzee Kikala na Mwananchi anasema hapaswi kuhurumiwa kwa kuwa na familia kubwa ndani ya Kombolela kwani kiuhalisia ana watoto saba, ilhali katika tamthilia hiyo anao sita na wajukuu kadhaa.

“Tofauti ni kuwa wa kwenye familia yangu ni wasikivu na wa kwenye Kombolela ni pasua kichwa, kha wale si watoto jamani,” anasema Kikala huku akicheka.

Swali: Tupe historia yako Mzee Kikala

Kikala: Mimi ni mzaliwa wa Sengerema Mwanza, mwenye elimu ya ngazi ya shahada ya sanaa katika masuala ya uigizaji bubu, niliyoipata nchini Sweden.

Baada ya kuhitima nilibahatika kufanya kazi ya ualimu Chuo cha Sanaa Bagamoyo, sasa TaSUba nilikofundisha kuanzia mwaka 1986 hadi 2015 ambapo kabla ya hapo nilikuwa mtumishi katika kikundi cha sanaa za ngoma cha Taifa, nikiwa mchezaji, mtunzi na mbunifu wa aina za ngoma.



Swali: Kiuhalisia una familia ya watoto wangapi?

Kikala: Nina familia ya watoto saba, lakini kila mmoja yupo na shughuli zake, na mimi ndio nawategemea, sio kama wale wa kombolela. Haaa! Haaaaa!

“Ukinihurumia kwenye Kombolela kuwa na watoto wengi, kimsingi ni wachache, wapo sita, wa kwangu halisi ni saba, tofauti yao hawa wanajitegemea na kunisaidia, wale wa Kombolela pooh hawawezekani,” anasema Kikala huku anacheka.



Swali: Ulianza lini hasa uigizaji?

Kikala: Baada ya kustaafu nilikuwa nafanya kazi na NGO moja Pangani ya kufundisha uigizaji, huko tuliandaa filamu mbalimbali lakini kubwa iliyokuja kunipa umaarufu ni pale nilipoigiza filamu ya ‘Siri ya Mtungi mwaka 2012 na ‘Bahasha’ iliyotoka mwaka 2017.

Baada ya hapo kazi mbalimbali zilikuja, ikiwemo kufanya na watu wa Bongomovie kama ile ya ‘Single Mama’ ya msanii Jacob Steven ‘JB’ na hapo ndio safari ya kushirikishwa kwenye filamu mbalimbali ikaanzia.

Nikacheza ‘Slay Queen’ niliyoigiza kama mzee mstaafu, ‘Tatu Chafu’, ‘Fimbo ya Baba’ na ‘Nawasaidieni’ na sasa kwenye tamthilia ambazo hakika nashukuru zimezidi kutangaza kipaji changu.

Swali: Unaonekana umri umeenda, unawezaje kuhimili mikiki ya kufanya kazi zote hizo?

Kikala: Ni kweli umri umekimbia, nina miaka 70 kwa sasa,lakini ninashukuru nimekuwa mtu wa mazoezi sana, jambo linalonifanya mwili wangu kuwa fiti wakati wote na pia ninajali kula yangu kwa kula vyakula vya asili bila kusahau maji mengi.

Swali: Wasanii wa zamani kwa sasa mnaonekna kurudi kwa kasi kutumiwa, unadhani imechangiwa na nini?

Kikala: Kilichochangia ni kuigiza uhalisia ambao hauishi thamani yake, hata filamu iliyoigizwa mwaka 2000 mpaka leo ukiitazama inakuvutia, pia hatuigizi ndani ya igizo, tunaigiza uhalisia wa maisha kama kufundisha, kuelimisha na kuburudisha tunawapa mashabiki kitu halisi.

Kama kuna kitu waigizaji wapya wanatakiwa kujifunza ni hiki tunachokifanya sisi, maana usanii wa maigizo ni kazi, ukiifanya ilimradi ikikutupa mkono hutakaa urudi tena.

Swali: Kuna changamoto umewahi kupitia kutokana na uiigizaji wako?

Kikala: Changamoto hazikosekani, nikianzia tu kwenye Kombolela, wengi ninaokutana nao mtaani huniambia wewe mzee ile familia itakuua kwa presha.

Ukikutana na maoni kama haya, kwa muigizaji ni jambo zuri kuonyesha kuwa unachoigiza ujumbe wake umewafikia vilivyo watazamaji.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags