Vijana Wa 2000 Ni Wazee Wa 2025

Vijana Wa 2000 Ni Wazee Wa 2025

Kuna watu wetu wamegoma kuzeeka. Kama siyo kiakili basi kimwili. Wapo wanaotaka miili ya 2000 iwe vilevile hadi leo. Na mawazo yao ya 2000 pia yaendelee kuwa vilevile hadi leo. Hili nalo ni janga la kitaifa. Nitarudi.

Ilikuwa Ijumaa. Nikiwa na vazi langu kulingana na siku husika. Kama kawa nikapita Masjid kidogo kupata daawa kidogo. Kutoka kwa Maalim Ubai Dulla Alii. Imamu wetu wa msikiti wa kitaa chetu, kijana mdogo sana.

Lakini umri wake siyo kigezo cha yeye kukosa maarifa ya imani. Ana madini sana. Akikutia neno unaweza kuanza safari rasmi ya kuelekea akhera bila kuaga. Hutaitamani tena dunia hii ya Ikangalombo na Mpanzu.

Nikiwa njiani kutokea Masjid, mara paaa, nakutana na Suma. Huyu ni mshikaji wangu wa kitaa. Yeye na dini ni paka na panya. Yeye na Masjid walipeana talaka rasmi, hata kabla hajabalehe. Anakereka na mahudhurio yangu ya ibadani.

Mtu wa bata sana. Na kila mja na lake jema. Pamoja na mapungufu yake ya kiimani. Lakini Mwenyezi Mungu, haki ya Mtume kamjaalia sana ushawishi. Maneno yake matatu Lissu anaweza kuomba apewe kadi ya sisiemu.

Hata sikumbuki kilichotokea. Ghafla tu nikajikuta nipo baa na Suma. Na pisi kali tatu. Vinywaji mezani, mbuzi choma na majina ya wahudumu wa baa na jikoni yote nimeyakariri. Sina habari tena.

Nimekuwa mwenyeji tena ni alwatani. Katika wale madem yupo na Suzzy wa Sinza Mapambano. Suzzy ambaye ni tatizo mtambuka. Popote alipo ujue kuna mwisho mbaya sana, wa pesa au lolote linalohusiana na bata.

Suzzy wa Sinza Mapambano ni noma. Anaweza kukusanya kijiji cha pisi kali kutoka Afrika Sana hadi Shekilango. Mkahama viwanja hata saba ndani ya saa chache kwa usiku mmoja. Anajua nini mwenye pesa anataka.

Kuna siku alitukutanisha masela saba kwa pamoja. Wote tunamtaka Sabra wa Mikocheni kwa Warioba. Mtoto wa Kirangi kutoka Kondoa. Amekwenda hewani, mzuri mpaka uzuri wenyewe unamuogopa.

Masela wote saba tulimlipa pesa ya udalali. Tulimpa pombe yeye na huyo Sabra wake. Na wote tulitawanyika bila yoyote kumpata Sabra. Na mbaya zaidi hata Sabra hakujua kama yupo pale anakidalaliwa.

Suzzy siyo mdogo. 'Eji goo', toka enzi za Juma Nature na Sinta, P Funk na Kajala. Mpaka wakati huu wa Marioo na Paula. Diamond na Zuchu. Suzzy yupo na michongo yake ni ile ile. Na maeneo yake yaleyale ya Sinzani.

Sasa siku hiyo nilikuwa na Suma CNN na Suzzy Kimeo. Suma tulimpa jina la CCN kwa sababu ya kukesha kila siku na kuongea sana. Suzzy aliitwa Kimeo kwa sababu ya kutia watu hasara. Ila ajabu watu wanawapenda kinoma.

Kwa sababu pamoja na yote. Ni watu wanaorahisisha mambo. Kwa watu wa bata watanielewa. Ila kwa wale wainjilisti na maimamu, kunielewa ni ngumu. Sasa niko na 'Dabo S' yaani Suma na Suzzy. Sina ujanja tena.

Nimefikaje pale, wakati nilitoka Masjid kuswali? Nikiwa na kanzu na sendozi zangu safi. Mara hii nimevalia 'jinsi' na raba, 'fomu siksi waiti' na kapelo. Na tayari nimedondosha bata mezani, na zile totozi za maana kweli.

Sina habari. Nimejiachia. Utadhani mimi ndiyo Abdul. Yule anayesifika kwa pesa za kuweza kumng'oa hata 'bigi mani' kutoka himaya ya Ufipa Ufipani. Nimeshasahau mawaidha ya Imamu wetu Ubai Dulla Alii. Shetani!

Kadiri saa zinavyoongezeka na watu wakazidi kuongeza. Idadi ya mademu ikiwa kubwa zaidi. Akili yangu ilianza kufanya kazi vizuri. Hata kukumbuka nimefikaje pale. Ni ushawishi wa Suma baada ya kuniambia kuna 'dili' flan.

Hakuna cha 'dili' wala dalali. Walitaka kulewa tu baada kusoma alama zao za nyakati. Nilikuwa na mpunga flan hivi, baada ya mkeka kutiki. Arsenal walinipa pesa baada ya kuwafuata mazima dhidi ya Madrid. Tajiri!

Elewa nilikuwa na pesa. Kwa wewe na shangazi yako mngenunua kiwanja Kiluvya au Makabe. Mjenge kinyumba chenu cha kujisitiri. Sasa hiyo pesa mimi nilikuwa sehemu flan naiteketeza kwa pombe, nyama na totozi. Sijali!

Kuna bwege nilimchana kuwa mkeka wangu umetiki, nina pesa za Mdosi. Naye akawa 'afisa tangazo'. Kasimulia wana kitaa, wakaamua kunijaza na kunikutanisha na totozi zile amazing. Mimi ni nani nisitumie pesa?

Jumamosi asubuhi naamka niko hoi. Nikigeuka sioni mazingira niliyozoea. Nipo hotelini. Kando kuna kiumbe wa kike kajilaza kifudifudi. Nilitabasamu kilofalofa. Baada ya kuona ngozi yake 'supa', laini kama tambi.

Chini kuna chupa za pombe. Viatu na vitambaa tambaa ambavyo huwezi kuamini kama ni mavazi. Tena vazi kutoka kwenye mwili wa ile pisi pale kitandani. Yes ana nyama nyingi sana na kinguo ni kidogo.

Kuangalia simu. Nakutana na 'misdi kolo' kibao. Za Suma 28, za Suzzy 30. Meseji za Suma 5 na Suzzy 9. Meseji zote zinaulizia kama nipo salama. Na nimelala wapi. Naachana na simu zao na kuinua kichwa kutazama nje.

Dirisha pana la kioo mbele ni uwanda mpana. Napikicha macho ili nijionee vyema. Kumbe ni bahari, na nipo nje ya Dar. Hapa ni Bagamoyo. Sitaki hata kutazama salio lililobaki, sitaki kujua hata jina la yule dem.

Suzzy na Suma mashetani wenye miili ya watu. Wapuuzi waliokataa kuzeeka. Hawataki kuishi sawa sawa na umri wao. Wanaotaka sote tuishi kibwege kama wao. Nikiri kwamba hawa watu ni mawakala wa shetani rasmi.

Mungu yupo atanipigania.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags