Calisah: Sijutii kumrudia Mungu, mimi na muziki basi

Calisah: Sijutii kumrudia Mungu, mimi na muziki basi

Mwanamitindo maarufu nchini, Calisah amesema kwa sasa hataki tena mambo ya kidunia aliyokuwa akiyafanya mwanzo badala yake amemrudia Mungu.

Akizungumza na Mwananchi Scoop Calisah amesema kwa kipindi kirefu amekuwa akifanya vitu ambavyo havimpendezi Mungu hivyo ameamua kuachana nayo

"Nimeamua kuacha vitu vingi ambavyo nilikuwa nafanya ambavyo nimeona sio sawa na kuamua kurudi kwenye njia ambayo inampendeza mwenyezi Mungu. Nimejitathimini wapi nilipo, naenda wapi na nikajua kuna maisha mengine yapo baadaye mtu ukishafariki kwa hiyo ni neema tuu," amesema Calisah.

Amesema aliona ni vyema kuzungumza uamuzi wake huo hadharani kwa sababu vijana wengi wamekuwa wakimfuatilia kwenye mitandao hivyo ni vizuri kama wataiga mfana wake.

"Kama kijana nikaona kuingia hadharani kwa sababu vijana wengi walikuwa wakinifuatilia nikaona ni sawa nikiweka wazi, kuwa sitopendezwa na mtu akifuata maisha yangu yale ambayo mimi mwenyewe nilikuwa sipendezwi nayo zamani. Lakini natamani vijana waige mfano huu wa sasa," amesema Calisah.

Calisah ambaye wengi wanamfahamu kupitia tasnia ya mitindo amesema hatoacha kazi hiyo, bali amejiwekea misingi ya kutofanya vitu vinavyomkufuru Mungu.

"Tasnia yangu inahusiana na masuala ya buruduni na wengi wamenifahamu kutokana na kazi yangu ambayo nimekuwa nikiifanya kwa miaka mingi. Lakini kwa sasa nitaendelea kufanya kazi yangu kwa sababu sio kazi ambayo inamkufuru mwenyezi Mungu.
“Mimi ni mwanamitindo na kazi yangu ni kutangaza baadhi ya vitu nguo na bidhaa, lakini nimeweka misingi siwezi kufanya kazi ambayo naona inautata mfano kama kutangaza vilevi," amesema Calisah.

Amesema ataendelea na mtindo wake wa maisha kama vile kufanya mazoezi na kuweka mwili vizuri katika hali ya usafi kwa sababu dini haijakataza.
"Nimeona watu wengi walikuwa wanadhani nilivyorudi kwenye dini labda watakuwa hawaoni nikifanya mazoezi au hawaoni nikikaa tumbo wazi. Mimi ni tofauti na hao watu wengi ambao wamezoeleka.
“Kuna watu walitangaza wanaachana na muziki alafu wakarudi kufanya muziki, mimi nimetangaza narudi kwa Allah, lakini suala la kujipenda kufanya mazoezi kuwa fiti, kuvaa vizuri litaendelea," amesema Calisah.

Calisah ambaye ametokea kwenye video nyingi za muziki kama video King, kwa sasa hatoweza kuvaa uhusika huo tena.

"Kwa upande wa muziki siwezi kufanya kazi yoyote inayohusiana na muziki, kwa sababu muziki ni haramu. Hata mtu awe na shilingi ngapi siwezi kufanya. Lakini kuigiza naweza kufanya jambo lolote ambalo haliendani na maadili ya dini siwezi kufanya,”amesema na kuongezea

"Hakuna ambacho najutia hata kimoja Mungu huyohuyo aliyenifanya kuwa Calisah ndiyo huyo ambaye amefanya leo niwe hivi nilivyo. Lakini mkisema najutia hapana sijutii chochote nitakuwa nakufuru. Mimi nipo sawa na sijutii,” amesema Calisah.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Masoud Kofii


Latest Post

Latest Tags