Malkia wa Hip Hop Soul na RnB Marekani, Mary J. Blige (54) ameshtakiwa na aliyekuwa mwanamitindo wake, Misa Hylton kwa madai ya kumkosesha mamilioni ya fedha kufuatia kuingilia na kutibua mipango yake ya kibiashara.
Hylton anadai kuwa Mary J, mkali wa kibao, Family Affair (2001), alikwamisha albamu ya rapa Vado isitokea hadi pale atakapositisha ushirikiano wao kibiashara kupitia kampuni yake ya M.I.S.A Management.
Katika nyaraka za mahakama zilizopatikana na AllHipHop, Hylton anadai Mary J kupitia kampuni yake, Beautiful Life Productions, alijaribu kuharibu uhusiano wake wa kibiashara na Vado ambao ungempatia asilimia 20 ya mapato ya rapa huyo.
Hati za mashtaka zinadai kwamba Mary J alijaribu kumshawishi Vado avunje makubaliano ya kufanya kazi na M.I.S.A ya Hylton wakati wa walipokutana katika mikutano ya faragha maeneo mbalimbali kama ufukweni na hoteli.
Pia inadaiwa kuwa mlinzi Mary J ambaye ndiye mpenzi wake, alitaka kumsaini Vado na kumwambia atapoteza fursa nyingi za kisanaa na kiuchumi ikiwa ataendelea kubaki chini ya usimamizi wa M.I.S.A.
Ikumbukwe Vado alisaini mkataba wa kusimamiwa na M.I.S.A kimuziki hapo Julai 25, 2023 lakini baadaye akasaini tena na Beautiful Life Productions mnamo Oktoba 1, 2023, hatua ambayo ndio chimbuko la mgogoro huo.
Hati za mashtaka zinaendelea kudai kuwa katika ujumbe wa ambao Mary J alimtumia Vado, alisema hatatoa albamu yake iliyokamlika Julai 2024 iwapo ataendelea kufanya kazi na M.I.S.A ambayo ameshindwa kuvunja mkataba wake aliyosaini hapo awali.
Hylton anasema kufuatia Mary J kufanya fitna ili albamu ya Vado isitoke, amemuacha msanii huyo katika utumwa wa kiuchumi maana hawezi kulipa fedha za kuvunja mkataba wa rekodi lebo ya M.I.S.A. ambao ni Dola5 milioni, kisha kutengeneza maisha yake.
Ikumbukwe Mary J. Blige alianza muziki mwaka 1988 wakati aliposainiwa na Uptown Records na Andre Harrell, kisha alianza kazi ya kuingiza sauti za chini (back vocal) katika nyimbo za wasanii wengine kwenye lebo hiyo kama vile Father MC na Jeff Redd.
Mshindi huyu Grammy mara tisa, alitoa albamu yake ya kwanza, What's the 411? (1992) ambayo inatajwa kuwa ya kwanza duniani kwa kufanikiwa kuchanganya muziki wa R&B na Hip Hop katika utamaduni wa Pop.
Ametoa albamu 14 ambazo nne kati ya hizo zimeshika namba moja chati ya Billboard 200, huku nyimbo zake maarufu kama Real Love, You Remind Me, I'm Goin' Down, Not Gon' Cry, Be Without You, Just Fine na Family Affair zikishika namba moja Billboard Hot 100.

Leave a Reply