Kwa sasa ni miaka zaidi ya 20 bado TID anaitumika Bongo Fleva akiwa ametoa albamu kali, ameshinda tuzo, ameanzisha bendi na tayari jina lake lipo katika orodha ya waimbaji wakali bora nchini kwa muda wote.
TID anaamini hadi sasa hakuna msanii mwenye sauti kama yake ndiyo sababu albamu yake ya kwanza akaipa jina la Sauti ya Dhahabu huku akiendelea kufanya vizuri katika miondoko ya RnB, Zouk, Afropop. Fahamu zaidi.
1. Kipindi akitafuta nafasi ya kutoka kimuziki chini ya Black Gangsters, kina TID walikuwa wakikutana katika mashindano na shoo na wenzao kipindi hicho kama Hotpot family (Soggy Doggy), GWM (KR), Dream Team (Witness a.k.a Kibonge Mwepesi) n.k.
Kati ya mwaka 1997 hadi 1999 TID alikuwa katika kundi la Black Gangsters na wenzake wanne na walikuwa wanafanya Hip Hop ila baadaye akahamia katika uimbaji.
2. TID aliamua kuwa mwimbaji baada ya kushauriwa na AY na King Crazy GK aliyemshirikisha katika wimbo wake, Tutakukumbuka. Wasanii wengine Bongo waliofanya hivyo ni Diamond Platnumz, Lady Jaydee, Jux, Dayna Nyange n.k.
3. Albamu yote ya TID, Sauti ya Dhahabu (2002) aliiandika kipindi yupo shule na hata wimbo wake 'Siamini' ulioshinda tuzo mbili za Kisima nchini Kenya umechukua mashairi kutoka katika kitabu maarufu shuleni cha Malenga Wapya.
4. Pindi albamu yake ya kwanza, Sauti ya Dhahabu (2002) ilipoingia sokoni ilimpatia Sh30 milioni na fedha hiyo ikagharamikia video chache alizofanya, pamoja na kumlipa P-Funk Majani, hivyo akabakiwa na Sh22 milioni.
5. TID alimlipa P-Funk Majani ili awe na hakimiliki ya albamu hiyo kutoka Bongo Records kitu ambacho hata Professor Jay amefanya katika albamu zake zote zilizotoka chini ya Bongo Records.
Lakini ni tofauti na wasanii baadhi ambao hawakulipia kazi zao bali waligawana faida ya mauzo ya kazi husika, hivyo hakimiliki ikabaki Bongo Records kwa Majani, miongoni mwa albamu hizo ni A.K.A Mimi (2004) ya Ngwea.
6. TID anaamini hadi sasa P-Funk Majani hajatengeneza mdundo mwingine mkali kama ule wa wimbo wake, Zeze (2002), lakini Majani mwenyewe anautaja wimbo wa Nako 2 Nako Soldiers, Hawatuwezi (2007) kati ya midundo yake mitano bora ya muda wote.
7. Seven Mosha ambaye sasa ni msimamizi wa wasanii Afrika Mashariki chini ya Sony Music, aliwahi kuwa Meneja wa TID. Kwa mujibu wa Seven, wakati huo TID alikuwa msanii mkubwa hadi soko la ndani lilishindwa kuihudumia chapa yake.
8. TID ambaye mwaka 2006 alianzisha Top Band na kuibua wakali kama Ommy Dimpoz na Steve RnB, hadi sasa amerekodi nyimbo zaidi ya 100 na kufanya kolabo zaidi ya 50 za ndani na kimataifa.
Alikubali kumuingiza Ommy Dimpoz Top Band baada ya kuimba vizuri wimbo wa Mr. Paul, Zuwena. Dili la kujiunga Top Band kwa mara ya kwanza Dimpoz alilisikia alipofika studio Sei Records.
9. Tangu ameanza muziki TID amekuwa na a.k.a nyingi kama Mzee Kigogo, Warioba n.k, ila a.k.a yake ya 'Mnyama' unajua alitoka wapi?. Hii alipewa Kenya ikiwa ni kipindi kifupi tangu atoke jela hapo mwaka 2008.
10. Wimbo wa kundi la Top Band linaloundwa na Q Chief na TID, Nilikataa (2007) wakimshirikisha Mr. Blue, ulirekodiwa na Marco Chali ila mixing na mastering alifanya Master J.
Ikumbukwe wimbo wa Mwana FA 'Binamu' toleo la pili, ndiyo ulimtambulisha Marco Chali katika Bongo Fleva, kipindi hicho Marco alikuwa anafanya kazi Kama Kawa Records ndipo baadaye akapata nafasi MJ Records yake Master J.

Leave a Reply