Nyota wa soka wa Ureno ambaye kwa sasa anaichezea Al-Nassr ya Saudi Arabia, Christian Ronaldo (CR7), ametangaza uchumba wake rasmi na mwanamitindo maarufu Georgina Rodríguez kwa kumvisha pete ya almasi. Wachumba hao wa muda mrefu wamedumu katika mapenzi kwa takribani miaka tisa sasa.
Georgina, mwenye asili ya Argentina na Hispania, alithibitisha habari hiyo kupitia Instagram yake jana Jumatatu, Agosti 11, 2025 akionesha pete ya almasi kwenye kidole chake.
“Ndiyo nakubali. Katika hili na maisha yangu yote,” aliandika kwa Kihispania.
Kabla ya hapo, Georgina alikuwa amewahi kuvalia pete nyingine ya almasi, lakini wawili hao walikuwa bado hawajachumbiana rasmi. Tetesi za uchumba zilianza mwezi uliopita baada ya Georgina kushiriki picha za chakula cha usiku chenye mandhari ya harusi, mapambo ya maua meupe na bendi ya muziki.
Mwezi uliopita, Ronaldo aliweka wazi kwa nini bado hawajafunga ndoa, akisema:
“Nitakapomwambia, ‘tutakapopata hisia hiyo sahihi,’ anajua ninachomaanisha. Inaweza kuwa mwaka mmoja, miezi sita au mwezi mmoja. Nina uhakika kwa asilimia 1000 itatokea.”
Wawili hao wamekuwa pamoja tangu 2016 na wana binti wawili Alana (7) na Bella (2). Georgina pia ni mama wa kambo wa watoto watatu wengine wa Ronaldo.
Katika kipindi chake cha I Am Georgina kwenye Netflix, alifichua jinsi marafiki wanavyomchangamsha kwa kumuuliza kila mara kuhusu tarehe ya harusi, wakirejea hata wimbo wa Jennifer Lopez “The Ring or When” kumtania.
Hata bila kufunga ndoa, Ronaldo mara kadhaa amekuwa akiishi na Georgina kama mke wake. Mwaka jana Desemba, kwenye tuzo za Globe Soccer Awards jijini Dubai, alisema: “Ni heshima kubwa kushinda tuzo hii. Mwanangu mkubwa yupo hapa, mke wangu [Georgina] yupo hapa.”
Katika michezo ya mitandaoni ya Mr. and Mrs kwenye YouTube mwezi Agosti, wote walionekana pia wakiwa wamevaa pete za ndoa. Katika mahojiano mengine, Ronaldo alimtaja Georgina kama mke wake.
Kwa sasa, Ronaldo anaichezea Al-Nassr nchini Saudi Arabia, na wanandoa hao wanaishi mjini Riyadh.

Leave a Reply