Wikiend iliyopita wawili hao walifanya sherehe nyingine Miami (white wedding), Marekani, ambapo Davido alitumia zaidi ya dola milioni 3.7 (zaidi ya shilingi bilioni 9.7) kwenye sherehe huku akimzawadia Chioma saa ya kifahari yenye thamani ya zaidi ya dola 300,000 na kuvaa vifungo vya shati vilivyo na picha ya mtoto wao marehemu Ifeanyi kama kumbukumbu.
Utakumbuka kuwa wawili hao walifunga ndoa ya kitamaduni Juni 25, 2024 jijini Lagos Sherehe ambayo ilihudhuriwa na viongozi wa serikali, wasanii maarufu, na watu mashuhuri wengine, huku wengi wakimpongeza Chioma kwa uvumilivu aliuonesha kwa mkali huyo wa Afrobeat mpaka kufunga ndoa.

Davido na Chioma walianza uhusiano mwaka 2013 wakiwa wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Babcock ambapo walianza urafiki mpaka kuwa wapenzi, mwaka 2018 Chioma alionekana katika video ya wimbo wa ‘Assurance’ ambapo Davido alimtambulisha rasmi mwanamke huyo kwa mashabiki zake.
Aidha, Septemba 2019, Davido alimchumbia Chioma na kumvisha pete ya thamani wakati tayari akiwa mjamzito, Oktoba mwaka huo wawili hao walibarikiwa kupata mtoto wa kiume aliyejulikana kwa jina la Ifeanyi. Hata hivyo walipanga kufunga ndoa mwaka 2020 lakini ndoa hiyo ikasogezwa mbele kutokana na janga la COVID-19.
Oktoba 2022, wanandoa hao walipa msiba mkubwa baada ya mtoto wao wa kwanza Ifeanyi kufariki kwa kuzama kwenye bwawa la kuogelea nyumbani kwao Lagos, tukio ambalo lilipelekea wawili hao kuwa kimya kwa muda mrefu ikiwa pamoja na Davido kusitisha shughuli zake za kimuziki.
Baada ya ukimya wa muda mrefu Davido alirudi rasmi kwenye muziki Machi 31, 2023 kupitia albamu ‘Timeless’ huku wimbo wa ‘Unavailable’ kutoka katika album hiyo akimshirikisha Musa Keys ukipata umaarufu zaidi. Albamu hiyo iliweka rekodi kwenye Apple Music kwa kuwa albamu ya Afrobeats iliyosikilizwa zaidi duniani ndani ya siku moja, na kwenye Audiomack ilipata streams zaidi ya milioni 12 ndani ya saa 24, rekodi kubwa kwa msanii wa Afrika.
Mwaka mmoja baadaye wawili hao walifanikiwa kupata watoto mapacha mmoja akiwa wa kike na mwingine wa kiume, watoto ambao walionyeshwa sura zao kwa mara ya kwanza kwenye moja ya tamasha la msanii huyo, alipokuwa kwenye mahojiano Davido alifunguka kuwa pacha wa kiume anafanana matendo na marehemu mtoto wake ambaye ni Ifeanyi.
Leave a Reply