Leo Julai 15, 2025 Tanzania imepata ugeni, Miss World 2025, Suchata Chuangsri 'Opal'. Mrembo aliyezaliwa mwaka 2003 huko Phuket, Thailand. Na yeye ndiye mwanamke wa kwanza kutoka Thailand kushinda taji hilo.
Mrembo huyo alimaliza elimu ya msingi shule ya Kajonkietsuksa na sekondari katika Shule ya Triam Udom Suksa, ambako alichukua kozi ya Kichina chini ya mtaala wa Sanaa.
Kabla ya kuwa Miss Universe Thailand, Suchata alikuwa akisoma shahada ya kwanza ya Sayansi ya Siasa na Mahusiano ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Thammasat.
Aidha Opal ni muhamasishaji kuhusu saratani ya matiti, jambo hilo ndilo lilimfanya ashiriki mashindano ya urembo ili kueneza uelewa kuhusu maradhi hayo. Wito wa kuzungumzia saratani aliupata baada ya kufanyiwa upasuaji wa uvimbe katika matiti yake yote mawili aliofanyiwa kipindi akiwa na miaka 16.
Mwaka 2022, akiwa na miaka 18, alishiriki mashindano ya Miss Universe Thailand 2022 na akamaliza akiwa mshindi wa nafasi ya tatu (third runner-up). Baadaye alipandishwa hadi kuwa nafasi ya pili (second runner-up) baada ya Nicolene Limsnukan, aliyeshika nafasi ya kwanza kujiondoa.
Kisha mwaka 2024, Suchata alichaguliwa kuiwakilisha Bangkok kwenye mashindano ya Miss Universe Thailand 2024. Alishinda mataji kadhaa maalum, zikiwemo Miss Charming Talent na Miss Beauty and Confidence. Mwishoni mwa mashindano hayo, alitawazwa kuwa Miss Universe Thailand 2024.
Hata hivyo, Aprili 22,2025 Opal aliteuliwa na Shirika la Miss World Thailand kuiwakilisha nchi hiyo kwenye mashindano ya Miss World 2025 nchini India.
Ndipo katika mashindano hayo yaliyofanyika Mei 31, 2025 jijini Hyderabad mrembo huyo aliibuka mshindi na kutawazwa rasmi kuwa Miss World 2025, akiwa mwanamke wa kwanza kutoka Thailand na wa pili kutoka Asia ya Kusini-Mashariki kushinda taji hilo la kimataifa.

Leave a Reply