Mrembo wa Dunia 2024, Suchata Chuangsri maarufu kama Opal, ametua nchini leo Julai 15, 2025 kwa ziara maalumu ya kuunga mkono mpango wa Royal Tour, unaolenga kutangaza utalii na utamaduni wa Tanzania duniani.
Opal amepokelewa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na viongozi wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo wakiongozwa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Sanaa, Dk Emmanuel Ishengoma pamoja na Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Dk Kedmon Mapana.
Kwa mujibu wa Basata wamesema kuwa ziara hiyo inalenga kuimarisha uhusiano wa kisanaa na kiutamaduni baina ya Thailand na Tanzania, sambamba na kuvitangaza vivutio vya kipekee vya Tanzania kupitia sura za warembo wa dunia.
“Ziara hii ni fursa adhimu kwa taifa kuonesha uzuri wake mbele ya dunia kupitia nguvu ya sanaa, urembo na utalii,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Opal anatarajiwa kutembelea maeneo mbalimbali ya kihistoria na kivutio ikiwemo mbuga ya Serengeti, Zanzibar na Mlima Kilimanjaro, huku akishirikiana na wasanii na wanamitindo wa hapa nchini katika maonyesho maalumu yatakayofanyika jijini Arusha na Dar es Salaam.
Mpango wa Royal Tour ulianzishwa na Rais Samia Suluhu Hassan mwaka 2021 kama njia ya ubunifu ya kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia simulizi za vivutio vya asili, historia na watu wake.
Opal, ambaye amejizolea umaarufu kwa kutumia urembo wake kuhamasisha utalii barani Asia, amesema anajivunia kuwa sehemu ya juhudi za kuitangaza Tanzania kama kivutio bora cha utalii duniani.
“Nimevutiwa sana na utamaduni na ukarimu wa Watanzania. Niko hapa kushuhudia na kuisemea Tanzania kupitia macho yangu na uzuri wake wa kipekee,” amesema Opal.
Ziara yake inatarajiwa kudumu kwa siku saba na inaratibiwa kwa ushirikiano wa Basata, Wizara ya Utamaduni na kampuni binafsi za utalii.

Leave a Reply