Mwigizaji wa filamu nchini, Alex Mgeta 'Ngosha' ameweka wazi sababu ya kufanya maigizo mengi yanayomuonesha kama mwanaume mwenye msimamo.
Akizungumza na Mwananchi, Ngosha amesema sababu inayopelekea kufanya hivyo ni baada ya kuona kizazi hiki vijana wengi wamepoteza sifa na nguvu ya uanaume. Hivyo hutumia ucheshi na maigizo kuonesha jinsi wanapaswa kuwa.
"Hiki kizazi vijana wengi wa kiume wamepoteza ile nguvu ya uanaume. Natumia katika ucheshi lakini nataka kuonesha kwamba mwanaume unatakiwa kuwa na misimamo na maamuzi, mamlaka na kutoa unyonge.
"Ukiwa mnyonge mwanamke anakuwa mnyonge mara mbili kwa hiyo sisi wanaume tumekosa hamasa ya kujiona tunaweza. Mimi nimekuja kuwapa misimamo, unamkuta mtoto wa kiume anajinyonga kwa sababu ya mapenzi sio sawa," amesema Ngosha.
Mwigizaji huyo ambaye mara nyingi hutumia uhusika wa Usukuma amesema alianza kutumia uhusika huo miaka sita iliyopita.
"Huu uhusika ulianza miaka kama sita iliyopita. Kulikuwa na shirika moja watu wa hisani kutoka Marekani walikuwa na tamthilia ambayo aikuwa anasimamia Jacob Stephen 'JB' katika stori yake ilikuwa inamuhitaji msukuma. Kwa hiyo kulikuwa na usaili watu wengi lakini nilivyokanyaga pale basi nilivyopita tu wakasema tuliyekuwa tunamtafuta ndio huyu," amesema Ngosha.
Amesema baada ya kuanza kuigiza kama msukuma watu wengi wa kabila hilo walipenda na iliwatia nguvu kujitokeza mbele na kusema wao ni Wasukuma.
"Baada ya kufanya Wasukuma wengi walipenda baada ya kuona kwamba wamepata mwakilishi wa kabila lao, na ndomaana unaona sasahivi wasukuma wote wanajitokeza maana walikuwa wanajificha wanasema ni Wanyarwanda" amesema Ngosha.
Amesema anatamani watu wamfahamu kama mchekeshaji kwa sababu ndiyo kitu anachokifanya tangu mwanzo.
"Mimi ni mchekeshaji toka mwanzo tunaita 'Comedy Drama', nimekuwa mcheshi tangu shule tangu nikiwa nyumbani mdogo kabisa. Unajua watu wengi wanashindwa kuelewa Comedy Drama kuna wasanii wapo wakubwa wanamefanya hii mfano marehemu Kanumba alikuwa ni komedi.
"Lakini alikuwa anafanya kwa kiwango fulani, JB anafanya Comedy Drama kwa hiyo kuna komedi inaigizwa kwa asilimia mia kuna zile zinafikisha ujumbe lakini zinakuwa na ucheshi ndani yake mimi ni mchekeshaji kabisa," amesema Ngosha.
Aidha, amesema mara nyingi huigiza akiwa na wanawake warembo kwani maigizo yake hayashushi thamani ya mwanamke.
"Mimi niseme namshukuru Mungu mabinti wengi wa kike wazuri wanapenda kufanya kazi na mimi, kwa sababu huwa siwadhalilishi alafu huwa na watia moyo nawashauri vizuri na ni kibali watu wanamna hiyo ndio wanakuja sana.
"Kabisa kuna watu wanaweza kufanya maigizo na mwanamke lakini maudhui hayo yasimfanye mwanamke huyo kuendelea kuwa na thamani yake na kumpunguzia. Kuna maudhui yanashusha thamani ya binti lakini kunanyingine inaweka levo nzuri kwa binti huyo," amesema Ngosha

Leave a Reply