Tiwa Savage Hataki kusaini msanii akihofia msongo wa mawazo

Tiwa Savage Hataki kusaini msanii akihofia msongo wa mawazo

Nyota wa muziki kutoka nchini Nigeria, Tiwa Savage wakati akifanya mahojiano na Forbes Africa. Amekiri kutokuwa na mpango wa kuongeza msanii kwenye lebo yake ya The 323 Entertainment record label, huku akidai anakwepa msongo wa mawazo unaotokana na kusimamia vipaji.

"Kila mtu huniambia kila wakati. Utasaini msanii lini? sidhani kama ninaweza kusaini msanii mwingine, kwa sababu wasanii wana dhiki naweza kuwa nimelala tu, halafu nitaamka na msanii wangu anavuma kwa kitu kingine," alisema Tiwa.

Hata hivyo, licha ya kutoonyesha kuhitaji kusaini wasanii ameweka wazi nia yake ya kuunga mkono vipaji vya wasanii chipukizi kwa kufungua shule ya muziki.

"Nina zawadi ya kusaidia, ndiyo sababu ninajaribu kufungua shule ya muziki, ambapo unaweza kwenda na baadaye kusaini lebo ambayo inaweza kukusaidia," amesema Tiwa.

Mkali huyo wa muziki pia aliwahasa wasanii chipukizi dhidi ya kukimbilia umaarufu, akisisitiza umuhimu wa kujenga misingi imara kabla ya kufikia kwenye kilele cha kazi zao.

"Tunza sana mwanzo wako. Wasanii wengi hukimbilia kileleni, lakini ukiwa hapo, unakabiliwa na shinikizo mipasho, matamasha na majukumu. Jenga msingi imara usijipoteze mwenyewe,"amesema Tiwa

Aidha, zaidi ya mafanikio ya msanii binafsi, Tiwa amesisitiza haja ya wasanii wa Afrika kuchukua udhibiti wa sanaa na tasnia yao kwa kumiliki na kutunza hadithi za muziki wao wenyewe.

"Tunahitaji kumiliki sanaa yetu, uchapishaji wetu, lebo zetu, tunahitaji kusimulia hadithi zetu wenyewe," amesema Tiwa

Pia, msanii huyo ameonyesha kuipinga dhana ya kutafuta uthibitisho wa mafanikio ya muziki wa Afrika kutoka kwenye masoko ya nje, akiwataka wadau wa tasnia kuzingatia kujenga mfumo wa muziki unaojitosheleza.

"Kwa nini tunajaribu kuingia kwenye soko lingine? Tunapaswa kujenga vyetu wenyewe ili kuwa wale wengine wanajaribu kuingia ikiwa tungekuwa na miundombinu sahihi, data ya bei nafuu, na uwekezaji, isinge tulazimu kutafuta uthibitisho mahali pengine." amesema Tiwa Savage.

Tiwa Savage ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 45, amesema anafikiria zaidi kuingia kwenye enzi yake ya unguli wa muziki wa Afrika akiwa Bilionea.

Mpango huo upo wazi kwani staa huyo amekuwa na biashara nyingi tofauti na muziki ambazo ni mafuta ya ngozi, mitindo, na kubwa zaidi ikiwa elimu kwani Tiwa savage anatizamia kufungua shule ya muziki ambayo haitotoa wasanii tu bali itakuza wataalamu wa tasnia ya muziki, kama vile watunzi wa nyimbo, watayarishaji, wataalamu wa muziki na wanasheria.

"Nafikiri mara nyingi watu wanapofikiria muziki, wanafikiria kuwa msanii tu lakini kuna mambo mengi kwenye tasnia. Ninataka kujenga shule au programu ya ufadhili wa masomo ambayo inafundisha hivyo" amesema Tiwa






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Masoud Kofii


Latest Post

Latest Tags