Kala Jeremiah hakuwa na ndoto ya muziki

Kala Jeremiah hakuwa na ndoto ya muziki

Nyota yake iling'aa baada ya kuonekana katika shindano la kusaka vipaji la Bongo Star Search (BSS) na sasa Kala Jeremiah ni miongoni mwa wasanii bora wa Hip Hop kuwahi kutokea Bongo.

Ameshinda tuzo tatu za muziki Tanzania (TMA), ametoa albamu moja, Pasaka (2013), huku nyimbo zake nyingi zikiwa daraja kati ya jamii na utawala kitu kilichompa umaarufu. Huyu ndiye Kala Jeremiah.

Baada ya kumaliza kidato cha nne mwaka 2001 Kala aliandika makala kuhusu kuwasaidia wananchi maskini akiwa la lengo isomwe redio na mamlaka zisikie na kuchukua hatua lakini hilo halikufanikiwa ndipo akaona muziki ni njia sahihi kwake kufikisha ujumbe ila hakuwa na ndoto hiyo.

Hadi mwaka 2004 Kala alikuwa hajui kama ana kipaji cha muziki, wakati huo alikuwa anauza mitumba huko Mlango Mmoja, Mwanza ingawa alikuwa anaupenda muziki wa Hip Hop sana.

Mwaka 2005 ndipo Kala alirekodi wimbo wake wa kwanza, ni katika studio ya Ujumbe Records iliyokuwa Mwanza jengo la Chama cha Mapinduzi (CCM) na Prodyuza aliyesimamia kazi hiyo anaitwa Brother John.

Baada ya watu kusikia wimbo huo ndipo wakamshawishi Kala kuja Dar es Saalaam kwa ajili ya kurekodi, akafanya hivyo na baadaye kuibuka katika shindano la BSS na kufanikiwa kushika nafasi ya nne.

Utakumbuka baadhi ya wasanii wengine walioibuliwa na BSS ambao wameweza kufanya vizuri Bongo ni Peter Msechu, Walter Chilambo, Kayumba, Frida Amani, Phina n.k.

Ngwea ndiye aliyemvutia zaidi Kala hadi kuanza kupenda Hip Hop na kujifunza kuchana na kuandika mistari, ni msanii wake bora wa Hip Hop kwa muda wote na ndio sababu ya kumpatia moja ya tuzo zake za TMA alizoshinda.

Baada ya kutoka kimuziki Kala alipata changamoto ya nyimbo zake kutopewa nafasi redioni hadi kuamua kukimbilia Uganda kupumzika huko, ni kitu alichokizungumzia katika wimbo wake wa Dear God.

Wimbo wake maarufu, Dear God (2013) hana kiitiko kwa sababu ni sala kwake ambapo alikuwa anazungumza na Mungu, anautaja kama wimbo uliokuwa mrahisi kwake kuandika kutokana ilikuwa sala tu.

Baada ya kushika nafasi ya nne katika BSS 2006, Kala alipewa zawadi ya kompyuta na meza yake pamoja na deki, lakini anamini fursa aliyoipata ya kutambulika na wengi ndio kitu cha muhimu zaidi kuliko zawadi.

Ikitokea Kala akagombea nafasi yoyote ya uongozi, basi wimbo wake, Nchi ya Ahadi (2015) akimshirikisha Roma ndio atautumia zaidi kwenye kampeni zake kwa sababu anaona ujumbe wake ndio kiu ya wananchi wengi kutoka kwa viongozi wao.

Kala Jeremiah ndiye msanii wa kwanza kutokea BSS kushinda tuzo nyingi za TMA ambapo mwaka 2013 alishinda tatu kwa mpigo ikiwemo ya Msanii Bora wa Hip Hop na ndio aliyompatia Ngwea ingawa tayari alikuwa ameshafariki.

Hata hivyo, kwa sasa Phina ndiye msanii wa BSS mwenye tuzo nyingi za TMA akiwa nazo nne alizoshinda mwaka 2021 na 2022, huyu ni mshindi wa BSS 2018 akitokea Mwanza, mkoa ambao Kala alianzia muziki ingawa yeye alizaliwa Shinyanga.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags