Msanii wa Bongofleva Harmonize wakati akielekea kutoa dozi ya burudani 'Tukaijaze Nangwanda' itakayofanyika Mtwara, ameandaa mashindano ya kusaka vipaji vya muziki.
Harmonize ameeleza kuwa shindano hilo ambalo amelipa jina la Konde Talent Search litafanyika ndani ya siku mbili Machi 27 Lindi na Machi 28 Mtwara. Huku zoezi la kujiandikisha katika mashindano hayo likianza Machi 25.
"Kuelekea tukaijaze'Nangwanda' ndugu zangu wa Kusini mwa Tanzania kutana na hili jukwaa linaloweza kubadili maisha yako kama kweli una kipaji basi wakati wako ndio huuu. Ni program ya siku mbili kabla ya usiku wa Eid Mosi.
"Mkoa wa Lindi tunakutana Rwangwa Machi 27, Mtwara mjini Machi 28. Ninaimani kupitia jukwaa hili tunaweza kukutana na wakina Konde Boy wengine. Fika mapema jiandikishe pambania kipaji chako hakuna gharama yoyote ya kushiriki,"amesema harmonize
Hata hivyo Konde Boy ataongozana na timu ya watu sita ambao watakuwa majaji kwenye shindano hilo ambao ni pamoja na Master J, Wema Sepetu, Lulu Diva, Dj Seven, Kimambo na BBoy.
Utakumbuka, awali Harmonize alisitisha shoo hiyo ya Tukaijaze Nangwanda iliyotarajiwa kufanyika Januari 1, 2025. kutokana na kuingiliana kwa ratiba nyingi za shoo za nje ya nchi kwa wakati huo.
“Tumejitahidi kufanya kila liwezekanalo ndani ya uwezo wetu mpaka kufikia now ila kwa masikitiko makubwa haitowezekana tena tarehe 1/1/2025 kama tulivyopanga poleni sana kwa usumbufu. Ratiba za nchi jirani zimeingiliana na tukaijaze Nangwanda kama mlivyoona tarehe 28 Desemba nilikuwa nchini Uganda tarehe 31 natakiwa niwe Kenya,” aliandika Harmonize.
Harmonize baada ya kusitisha shoo hiyo aliweka wazi kuwa shoo hiyo haina na dhumuni la kutoa burudani pekee, bali yeye na timu yake walihitaji kurudisha shukrani kwenye jamii kwa kusaidia wazee, vituo vya afya na watu wenye uhitaji.

Leave a Reply