Msanii wa muziki wa hiphop nchini, Rapcha ambaye kwa sasa anatamba na Mixtape yake mpya ya ‘Usichukue Sifa za Mungu’ iliyotoka Aprili 25,2025, ameelezea namna ambavyo kazi hiyo inagusa maisha yake.
Akizungumza na Mwananchi msanii huyo amesema sababu ya kuiita project hiyo Usichukue Sifa za Mungu ni kutokana na msukumo aliopata wakati akiandaa.
"Project nimeiita Usichukue Sifa za Mungu kutokana ni msukumo nilioupata wakati naandaa. Nilikutana na huo ujumbe wakati naandaa albamu yangu naamini kupitia hiyo itaweza kugusa watu wengi kama vile ambavyo mimi ilinigusa," amesema Rapcha.
Amesema kwa kiasi kikubwa kazi hiyo inagusa maisha yake na jamii inayomzunguka.
"Kwa kiasi kikubwa kila kitu kinahusiana na mimi, hata kama sio moja kwa moja lakini kupitia jamii nimeona kupitia watu kwa ufupi inanigusa kwa asilimia kubwa," amesema Rapcha.
Amesema ushawishi wa kuandaa kazi bora ambayo imekubalika na wadau, mashabiki na wasanii wenzake ni kutokana na uwezo ambao amekuwa nao tangu miaka ya nyuma.
"Nafikiri ni namna ambavyo Mungu amepanga iwe kwa sababu zake binafsi. Mimi kila ninachokifanya utukufu na sifa zote ziende kwake. Sijui kwanini watu hawakutegemea kukutana na mawazo makubwa kama yale lakini kwa mtu ambaye ananisikiliza tangu zamani anaelewa vile ambavyo nimekuwa nikifanya kuanzia miaka mitano nyuma mpaka sasa," amesema Rapcha.
Rapcha amesema wimbo wake wa 'Comfort Zone' ambao amemshirikisha Banana Zolo alitaka kuelezea uhalisia wa mwanadamu jinsi asivyopenda kuridhika.
Pia, wimbo wa Happy Nation unaopatikana katika Mixtape hiyo amesema unamuhusu kwa sababu amejiimbia kama mtu ambaye yupo kwenye taifa lenye furaha japo anakutana na changamoto kadhaa.
"Happy Nation ni wimbo unaoongelea maisha ya mtu anayeishi katika taifa la furaha kwa hiyo imeeleza struggle zake na pia imeeleza namna ambavyo amebarikiwa.
“Kwa hiyo mimi nimejiweka kama huyo mtu ambaye yupo kwenye hilo taifa la furaha nikaongelea na kitu kama hicho kuonesha namna mama watoto wangu alivyojifungua bila matatizo," amesema Rapcha.
Aidha amefafanua namna P Funk Majani, alivyompa mchongo uliomuingizia pesa zaidi ya Sh20 milioni, kama alivyoimba kwenye wimbo wake Dont Play This Song unaopatikana kwenye Mixtape hiyo akisema "Muziki umechange my story sitosahau siku Father P ananipa deal la Over 20 mil"
"Ilikuwa ni deal iliyokuwa inahusisha project yangu ya Wanangu99 lazima iwe hivyo kwa sababu muda huo nilikuwa na mabadiliko makubwa nakuvutia dili ya aina yoyote," amesema Rapcha.
Amesema sababu ya kumtumia mtangazaji Barbara Hassan kama sehemu ya kiunganishi katika mradi huo ni kwasababu alitamani watu wajue namna alivyokuwa akijisikia wakati anaenda shule miaka ya nyuma wakati anamsikiliza mtangazaji huyo.
"Kwa sababu ni mtu ambaye nimekuwa nikimsikia na kumuweka kwenye albamu nilitaka watu wajue vile nilikuwa najisikia wakati naenda shule nilikuwa namsilikiza kwenye radio," amesema Rapcha.

Leave a Reply