Ni utamaduni wa Zuchu kuwatenga wenzake

Ni utamaduni wa Zuchu kuwatenga wenzake

Ikiwa ni miaka mitano tangu ametoka rasmi kimuziki, Zuchu amefanikiwa kuwa chapa kubwa yenye ushawishi katika Bongofleva na kimataifa ambapo ameshirikiana na wasanii wakubwa na kuweka rekodi nyingi za mauzo.

Hata hivyo, kuna eneo moja linaloacha alama ya ulizo kuhusu mwenendo wa Zuchu kimuziki, nalo ni jinsi anavyoshirikiana na wasanii wenzake kutokea nje ya WCB Wasafi, rekodi lebo inayomsimamia. 

Ikumbukwe kwa mara ya kwanza Zuchu alivuma kimuziki kupitia wimbo wake 'Wana' kutoka katika Extended Playlist (EP) yake, I Am Zuchu (2020) ambayo ilikaa katika chati za YouTube Music Tanzania kwa wiki zaidi ya 100. 

Akiwa anaendelea kufanya vizuri na albamu yake ya kwanza, Peace and Money (2024), tayari Zuchu ameshinda tuzo saba za muziki Tanzania (TMA) akiwa ndiye msanii aliyeshinda mara nyingi zaidi tangu msimu wa 2021. 

Kwa sasa Zuchu anavuma kupitia wimbo mpya, Hapa (2025) ambao ameshirikishwa na G Nako, rapa kutokea makundi ya Nako 2 Nako Soldiers na Weusi, washindi wa TMA 2013 kama Kundi Bora la Mwaka.

Ni kolabo nzuri kwa ujumla lakini inaacha swali moja tu, nalo ni iwapo video yake itatoka!, swali hilo linakuja kufuatia utamaduni wa Zuchu kutoshiriki katika video za wasanii wengi wanaomshirikisha nje ya WCB Wasafi.

Yaani Zuchu akishirikishwa na mwanamuziki hasa wa Bongofleva kutoka nje ya lebo inayomsimamia, basi kuna asilimia ndogo sana ya video rasmi ya wimbo huo kutoka bila kujali ukubwa wa aliyeshirikiana naye.

Mathalani, kolabo yake na Dogo Paten, Afande (2025) ambayo imefanya vizuri sana ikiwakosha mashabiki wengi wa Singeli, hadi sasa ni zaidi ya miezi miwili tangu wimbo huo kuachiwa lakini video yake haijatoka na hatujui kama itakuja kutoka!.

Akiwa kama msanii mchanga anayetaka kulishika soko, ni wazi kuwa Dogo Paten angefurahi kushirikiana na Zuchu katika video ya wimbo wake maarufu zaidi lakini ni wazi hilo lipo nje ya uwezo wake.

Tunaweza kusema Dogo Paten bado ni mwanamuziki mdogo na pengine ndio sababu video hiyo haijatoka hadi sasa lakini kuna majina makubwa katika Bongofleva ambayo Zuchu aliyatosa vilevile!.

Jux katika albamu yake ya kwanza, King of Hearts (2022) alimshirikisha Zuchu katika wimbo 'Nidhibiti' ambao ulipokelewa vizuri ila video yake hadi hii leo haijatoka, lakini kolabo zote za Jux na Diamond Platnumz (Sugua, Enjoy na Ololufe Mi) video zake zimetoka.

Rapa kutoka Classic Music Group (CMG), Darassa alishirikiana na Zuchu katika ngoma yake, Romeo (2024) ila video nayo haikutoka, lakini Darassa aliposhirikiana na Nandy katika wimbo 'Loyalty' video ilitoka na kushinda TMA 2021.

Naye Whozu alitoa ngoma na Zuchu, Attention (2024) lakini yakawa ndio yale yale, na hilo linaibua swali iwapo ni utamaduni wa Zuchu kuwatenga kimtindo wanamuziki wenzake kutoka nje ya WCB Wasafi linapokuja suala la video za kazi zao?

Ndani ya WCB Wasafi, anashirikishwa sana tu na video zinatoka, kwa mfano Rayvanny alitoa kolabo mbili na Zuchu, Number One (2020) na I Miss You (2022), na zote hizi video zake zilitoka.

Na Januari mwaka huu video ya wimbo 'Number One' ilifikia rekodi ya kutazamwa zaidi ya mara milioni 100 YouTube ikiwa ni video ya kwanza ya Rayvanny kufanya hivyo na ya nane ndani ya Bongofleva kufikia namba hizo za juu.

Kwa upande wake D Voice, mwanamuziki wa mwisho kutambulishwa WCB Wasafi akitoka na albamu yake, Swahili Kid (2023), ndani ya muda mfupi amemshirikisha Zuchu katika nyimbo tatu na mbili kati ya hizo video zake zimetoka.

Video ya kolabo yao, BamBam (2023) tayari imetazamwa YouTube zaidi ya mara milioni 19 ukiwa ndio wimbo wa D Voice wenye namba za juu zaidi katika mtandao huo unaotumiwa na mashabiki wengi hapa nchini.

Ikumbukwe Desemba 2021, video ya Zuchu 'Sukari' iliandika rekodi kama video ya muziki iliyofanya vizuri YouTube Afrika mwaka huo ikitazamwa zaidi ya mara milioni 60, huku ikifuatiwa na ile ya Wizkid ft. Tems, Essence (2021) iliyotazamwa mara milioni 53.

Hata hivyo, mwaka uliofuatia Zuchu alishindwa kuifikia rekodi hiyo mbele ya Rema wa Nigeria ambaye video ya wimbo wake, Calm Down (2022) ilitazamwa zaidi ya mara milioni 300 na kuongoza Afrika ikifuatiwa na remix yake ambayo sasa imefikia bilioni 1.1.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags