Peter Akaro
Staa muziki Marekani, French Montana ambaye pia ana asili ya Morocco ameonekana kwa mara nyingine tena akiwa na anayetajwa kuwa mpenzi wake mpya, na huyu si mwingine ni binti wa Mfalme wa Dubai, Sheikha Mahra.
French Montana na Sheikha Mahra, anayejulikana pia kama Xtianna katika mtandao wa Instagram, walionekana wakiwa karibu sana huko mjini Paris, Ufarasa wiki iliyopita, zikiwa zimesalia siku chache kabla ya wiki ya mitindo ya Haute Couture.
Kwa mujibu wa vibe, wawili hao walionekana wakiwa wameshikana mikono na kupiga picha pamoja tena kwa mahaba tele lakini suala la kuweka rasmi uhusiano huo kwa umma limebaki baina yao.
Jumanne hii Sheikha kupitia Insta Story ameposti picha ikionesha mkono wake na wa mwanaume aliyevalia koti la manyoya huku wakiwa wameshika kofuli katika mnara wa Paris wa Eiffel, kisha picha hiyo kupambwa na emoji nyekundu ya moyo.
Inaaminika kuwa ingawa wawili hao wameonekana hadharani, wanajaribu kulinda faragha yao kwenye mitandao ya kijamii, hivyo moyo mwekundu uliwekwa juu ya kofuli hilo kwa lengo la kuficha majina au herufi za majina yao.
Watu wengi kwenye mitandao ya kijamii wanaweza kuelewa hali hiyo nataka kuonyesha niko na mtu, lakini sitaki dunia ijue ni nani huyo!.
Hayo yanajiri baada ya hivi karibuni French Montana kufanya mahojiano na Rah Ali kwenye kipindi cha Sited na kufunguka mambo kadhaa kuhusu maisha yake.
Mtangazaji huyo alimpongeza Montana kwa kuendelea vizuri na kazi zake, kisha kuchomekea huwenda chanzo cha nguvu na furaha yake ni hatua ya kuacha pombe, lakini pia huenda kuna mwanamke maalum katika maisha yake. Hata hivyo, mwanamuziki huyo hakutaka kuingia katika mtego huo!.
"Nitaruka hilo," alisema na kuendelea. "Nataka maisha yangu ya faragha yabaki kuwa ya faragha.... Nahisi kila mara yanapoingia kwenye vyombo vya habari, mambo huenda kombo baada ya hapo."
Kwa kuzingatia kuwa huenda ana uhusiano na binti wa kifalme mtoto wa Waziri Mkuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Mohammed bin Rashid Al Maktoum, kulinda faragha yao kuna maana kubwa.
Isitoshe, Sheikha Mahra alitalikiana na mume wake wa zamani, Sheikh Mana al Maktoum mnamo Julai 2024 ikiwa ni miezi michache tu baada ya kupata mtoto wao wa kike, kutokana na kile kinachotajwa kama usaliti kwenye ndoa.
Ikumbukwe Montana alivuma zaidi na albamu yake ya kwanza, Excuse My French (2013), ikishika nafasi ya nne chati ya Billboard 200, huku wimbo wa kwanza 'Pop That' aliowashirikisha Rick Ross, Drake, na Lil Wayne, ukiingia 40 bora ya Billboard Hot 100.
Baadaye alikuja kufanya vizuri zaidi na wimbo wake, Unforgettable (2017) akishirikiana na Swae Lee, mashabiki wengi Afrika wamemfahamu Montana kupitia wimbo huo ambao video yake iliyofanyika Uganda imeshatazamwa YouTube zaidi mara bilioni 1.8.
Leave a Reply