Mr Ebbo kwenye safari ya Danny Msimamo

Mr Ebbo kwenye safari ya Danny Msimamo

Hadi katikati ya miaka ya 2000, Danny Msimamo alikuwa miongoni mwa marapa wakali katika Bongofleva akitambulika na wengi kama msanii mwenye uwezo wa kufikiri nje ya box na nyimbo zake nyingi zinathibitisha hilo.

Danny Msimamo katika safari ya muziki alipita studio nyingi ila Motika Records na Aigies Records ndizo zimebeba historia kubwa kwake maana nyimbo zake nyingi maarufu zimetengenezwa hapo. Fahamu zaidi.

Kipindi akijitafuta, Danny Msimamo aliwahi kuwa katika kundi moja na Mkoloni ambaye baadaye alienda kuunda kundi la Wagosi wa Kaya na Dr. John, kundi lake na Mkoloni lilikuwa linaitwa Hood Tanga Line.

Huyu jina lake kamili ni Daniel Kamili, hilo la ‘Msimamo’ lilikuja alipoanza muziki akipambana katika tasnia kisha kurudia masomoni na baadaye kurejea tena kwenye muziki, akaona kujiita ‘Danny Msimamo’ itafaa zaidi kutokana alisimamia alichoamini.

Hata hivyo utasikia watu wengine wakimuita ‘Danny Msimamo, Kijana wa Makamo’, hiyo ilikuja tu wakati akitafuta vina katika nyimbo zake haina maana yoyote katika uhalisia wa maisha yake.

Akiwa shule akakutana na Saimon Sayi ‘Complex’ wakawa wanafanya muziki pamoja na walifanikiwa kushinda katika mashindano ya kuchana huko Tanga, ni mashindano ambayo Professor Jay alishuhudia wakitangazwa washindi.

Complex ambaye alifariki mwaka 2005 katika ajali ya gari, alikuwa na uwezo mkubwa kama rapa na prodyuza, ndiye mtu wa kwanza kurekodi wimbo wa Danny Msimamo, Mic lakini haukufanikiwa kutoka.

Wimbo uliomtoa Danny kimuziki ni ‘Mic’, sasa wimbo huu alipanga kuurekodi Bongo Records kwa P-Funk Majani baada ya kupewa ofa hiyo ila nafasi ikakosekana kutoka kipindi hicho kila msanii alitaka kurekodi hapo.

P-Funk alivutiwa na uwezo wa Danny baada ya kumsikia katika nyimbo za Wagosi wa Kaya ambazo bado zilikuwa hazijatoa ndipo akampa ofa hiyo ya kurekodi bure.

Kufuatia kukosa nafasi kwa P-Funk, rafiki yake, Mr. Ebbo akamwambia warudi Tanga wakarekodi studio kwake ndipo wakazama Motika Records, Mr. Ebbo akatengeneza mdundo kisha ikatoka ngoma hiyo (Mic) iliyomleta mjini Danny Msimamo.

Kwa kifupi Mr. Ebbo aliyefariki mwaka 2011, ndiye alimtoa Danny Msimamo kwa sababu alitengeneza wimbo wake wa kwanza na ndiye alimchukua kutoka Tanga hadi Dar es Salaam kwa ajili ya kuusambaza katika vituo vikubwa vya redio.
Na kabla ya kurekodi wimbo huo na kuutoa, Mr. Ebbo alikuwa akizunguka na Danny katika shoo zake na hata alipoanza kuwika kimuziki bado alifanya hivyo na muda mwingine alichukua sehemu ya malipo yake na kumpatia.

Baada ya kutoka kimuziki, Danny akaja kukutana tena na rafiki yake wa muda mrefu, Complex ambaye alikuwa anafanya kazi Aigies Records kama prodyuza, basi akamkaribisha studio hapo waweze kufanya kazi pamoja tena.

Alichofanya Danny ni kwenda na daftari lake la nyimbo studio na kuangalia upi anaweza kurekodi kwa siku hiyo, ndipo akakutana na mashairi ya ngoma, Siku Nzuri iliyokuja kufanya vizuri kuliko Mic.

Hata hivyo, wakati Danny anaandika wimbo huo, sio kwamba hata alikuwa na siku nzuri kama anavyoeleza katika ngoma hiyo, ni siku ambayo alikuwa hana fedha, mambo hayaendi ila ukakumbuka zile siku nzuri vinavyokuwa, ndio msingi wa wazo lake.

Sasa baada ya kuachia wimbo, Siku Nzuri na kubamba na hadi kupata show nyingi, ndipo Danny akasikia maneno ya watu yakidai kuwa alipata wazo la kutunga wimbo huo kutoka katika wimbo wa Ice Cube ‘It Was a Good Day’ lakini anasisitiza hilo ni wazo lake.

Na hata kipindi anarekodi Aigies Records na Complex, Danny alikutana na Chid Benzi ambaye alikuwa anatafuta nafasi ya kutoka, kipindi hicho Chid anaimba na sio kurap kama alivyokuja kutambulika akishinda tuzo ya TMA 2006 kama Msanii Bora wa Hip Hop






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Masoud Kofii


Latest Post

Latest Tags