Mpiga gitaa Omar Seseme, amefariki dunia

Mpiga gitaa Omar Seseme, amefariki dunia

Mpiga gitaa mkongwe nchini, Omar Seseme, amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu maradhi ya moyo, akiwa nyumbani kwake Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwananchi, Msemaji wa bendi ya Sikinde OG, Mwalimu Hassan Libingai, amesema taarifa za kifo cha Seseme zilipatikana majira ya saa 10 jioni Mei 12, 2025, baada ya majirani kuvunja mlango wa chumba chake saa 8 mchana walipobaini kuwa hakuwa ametoka nje tangu asubuhi.

"Tulipata taarifa kutoka kwa vijana aliokuwa akiishi nao jirani, wakisema kuwa ‘Babu’ hajatoka wala kufungua mlango wake wa chumbani tangu asubuhi. Tulipowaambia wavunje mlango, ndipo wakamkuta tayari ameshafariki dunia," amesema Libingai.


Kwa mujibu wa Libingai, hadi siku ya tukio jioni, marehemu Seseme aliwasiliana na uongozi wa Sikinde OG akiomba msaada wa kuhamishiwa maeneo ya Amana karibu na kliniki aliyokuwa akipata matibabu.

"Tulichelewa kutoa taarifa kwa umma kutokana na kuwa na mambo kadhaa ya kushughulikia, ikiwemo kuwasaka ndugu zake ambao hadi sasa hatujawapata. Tayari tumepokea mwili wake Hospitali ya Amana," amesema.

Libingai amesema Seseme alianza kuugua tangu mwaka 2022 na kwa muda mrefu alikuwa akifanya maonyesho akiwa amekaa kutokana na kuchoka kwa mwili wake.

"Ilipofika Januari 2024, tuliamua kumpeleka Hospitali ya Amana, akafanyiwa vipimo na kugundulika kuwa anasumbuliwa na moyo. Tukaandaa utaratibu wa kumfungulia kliniki na hata bima ya matibabu. Nyumba aliyokuwa akiishi hadi umauti unamkuta, ilikuwa ni mali ya bendi ya Sikinde OG," amesema.

Seseme, ambaye alianza kujiunga na Sikinde OG mwaka 2022 akitokea Supar Kamanyola ya Mwanza, aliwahi pia kutumikia bendi kadhaa maarufu zikiwemo Tam Tam, TOT na nyinginezo.

Mazishi ya msanii huyo yamepangwa kufanyika leo saa 10 jioni katika Makaburi ya Mzimuni, Mwinyimkuu Magomeni, jijini Dar es Salaam. Kabla ya maziko, mwili wake utaswaliwa katika Msikiti wa Mwinyimkuu kuanzia saa 4 asubuhi.

"Tutatoa taarifa zaidi kuhusu ndugu au taratibu nyingine pindi zitakapokamilika," amesema Libingai.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags