Kumekuwa na lawama nyingi kutoka kwa baadhi ya mashabiki na wadau wa muziki zikitupwa kwa wasanii ambao huanza kufanya aina fulani ya muziki na baadaye kubadilika na kufanya aina nyingine.
Msanii kuhamia katika aina nyingine ya muziki inaweza kusababishwa na vitu mbalimbali kama kulifuata soko la muziki lilipo, sababu nyingine ni msanii kuhitaji kuonesha uwezo wake wa kufanya vitu vingi kwenye sanaa yake.
Kuna mifano mingi ya wasanii ambao waliamua kusaliti chama baada ya kutekwa na aina nyingine ya muziki hii ilitokea hata kwa Jux ambaye alianza kutambulika kama msanii wa R&B lakini sasa anafanya aina tofauti. G Nako naye alianza kama rapa lakini kwa sasa ni moja kati ya viraka wakubwa akiwa anafanya aina nyingi za muziki kama Singeli, Amapiano na aina nyingine.
Wasanii waliobadilika kutoka kwenye aina moja ya muziki na kwenda nyingine ni wengi lakini kwa leo tumuangalie Billnass ambaye mwanzo alitambulika kwenye tasnia ya muziki kama rapa baada ya kutoa ngoma yake 'Ligi Ndogo' iliyotoka Desemba 29, 2015 akiwa na mkali wa Bongo Fleva, TID.
Pia aliachia nyimbo nyingine za mtindo wa rapu kama Chafu Pozi 2016, Mazoea Ft Mwana FA 2017, Sina Jambo 2017, Tagi Ubavu 2018, Labda Nizikwe 2018, Funga Feti 2019, ngoma ambazo zilimpa heshima kubwa na kutambulika kama moja ya rapa wa kali nchini.
Lakini msanii huyo alianza kubadili gia 2018 baada ya kukutana na Whozu kwenye ngoma yao 'Kwa Leo', Billnass akionesha uwezo wake mwingine wa kuimba nyimbo zilizochangamka tofauti na rapu.
Akafanya hivyo tena kwenye 'Naleft' iliyotoka 2019 akiwa na Whozu tangu hapo amekuwa mtu wa kubadilika mpaka sasa ana ngoma nyingi za aina tofauti tofauti huku baadhi ya mashabiki wakidai amesaliti muziki uliomtambulisha.
Billnass pia ni miongoni mwa wasanii ambao wamepita vizuri na upepo wa muziki wa amapiano huku akifanikiwa kutengeneza ngoma Hit. Mwaka 2021 aliachia remix ya ngoma ya Tit For Tat ya kwake Ril Vin ambayo ni amapiano. Mwaka 2022 alishirikiana na msanii wa Bongo Fleva, Rayvanny na kuachia ngoma ya Utaonaje ambayo pia ipo kwenye mahadhi ya amapiano. Mwaka huohuo alichia 'Chetu' ambayo ni amapiano.
Mwaka 2023, walikutana na Marioo kwenye ngoma ya Maokoto ambayo ni amapiano ikiwa moja kati ya ngoma zake kubwa kwenye historia ya muziki wake. Ameendelea na amapiano mpaka kwenye ngoma yake ya 'Maboss' iliyotoka 2024, akiwa na Jux, Kinamba Namba ya 2024 akiwa na G Nako, Whozu, Apuki na Dj Joozey.
Hata hivyo, licha ya Billnass kufanya vizuri kwenye muziki wa amapiano hajawasahau mashabiki wake wa mtaani kwani ameendelea kufanya kazi akiachia nyimbo kama vile Magetoni ya 2024, Boda akiwa na Mbosso 2025, Puuh akiwa na Jay Melody 2023, Bye akiwa na Nandy 2022, Mafioso, Deka, Bugana, Tatizo na nyingine nyingi.
Akizungumza na Mwananchi Docta Ulimwengu ambaye anasimamia chapa za mastaa kama Hamisa Mobetto, Jux na Idris Sultan na hapo awali alimsimamia Jay Mondy amesema ili msanii aweze kudumu kwenye gemu anatakiwa kubadilika mara kwa mara huku akimtolea mfano Jux.
"Msanii anatakiwa kufahamu kuwa kila baada ya miaka mitano kinaibuka kizazi kipya kwa hiyo nyimbo ambazo wamependa wakati huu ni tofauti na watazopenda kwa wakati ujao. Hivyo ni vizuri kwenda na wakati na kubadilika mara kwa mara msanii hatakiwi kung'ang'ania aina moja ya muziki.
"Pia msanii anatakiwa kwenda sambamba na teknolojia ya sasa kwa sababu huko ndipo muziki unapouzwa yaani hata kama msanii haelewi anatakiwa kuwa na 'team' ya watu ambao wanamsaidia kufikia mitandao hiyo,"amesema.

Leave a Reply