Mbosso atemana na WCB, Diamond athibitisha

Mbosso atemana na WCB, Diamond athibitisha


Mwanamuziki na mmiliki wa rekodi lebo ya WCB Diamond Platnumz amethibitisha mwanamuziki wake Mbosso kujing'oa kwenye lebo hiyo.

Akizungumza na Clouds Fm  Februari 5, 2025 Diamond amesema Mbosso tayari ameanza kujisimamia rasmi ikiwa ni baada ya kukamilisha taratibu zake.


"Mbosso wiki mbili na nusu nyuma tumeongea akaniomba aanze kujisimamia nikampa baraka zote, ni mdogo wangu sababu ya mimi kumsaini nilikuwa nampenda. Na watu wengi kwenye lebo wanajua hilo.

"Mimi na Mbosso hatujawahi kugombana, labda kama tumewahi ilikuwa kwenye kujenga maendeleo ya kwake. Nikamwambia mdogo wangu kwa ulivyoniheshimu na tulivyopendana siwezi kukutoza hata shilingi kumi,"amesema Diamond

Amesema msanii huyo aliyejiunga na WCB mwaka 2018 hajalipa pesa yoyote licha ya kutaka kulipa. Hii inakuwa tofauti na baadhi ya wasanii ambao wamewahi kutoka kwenye lebo hiyo, kwani baadhi yao walilipishwa.

"Mpaka sasa hivi tumeshakamilisha process zake, na ameanza kujisimamia rasmi na hata shoo aliyofanya huku (Dodoma) amekuja rasmi kama ameshaanza kujisimamia. Kwa hiyo lazima tumuunge mkono na nitaendelea kumlinda na ataendelea kuwa familia ya Wasafi nitampigania na hata madansa wengine nilionao ni wake.

"Kwanza nimshukuru kwa kutumia hekima, alivyokuja alikua tayari kwa kulipa nikamwambia siwezi kumtoza kwa heshima na mapenzi tuliyoishi kumtoza ni aibu. Ila angekuwa mtu mwingine ambaye hatujaheshimiana lazima hela atoe. Atakayemgusa Mbosso ajue kanigusa mimi,"Diamond alimalizia

Ikumbukwe Mbosso (2018) ni msanii wa sita kusainiwa na WCB Wasafi baada ya Harmonize (2015), Rayvanny (2016), Queen Darleen (2016), Rich Mavoko (2016), Lala Lava (2017), Zuchu (2020) na D Voice (2023).

Mbosso anaenda kuongezeka katika orodha ya wasanii waliojitoa kwenye lebo hiyo. Hadi sasa wamekuwa wa nne, alianza Rich Mavoko (2018) akaanzisha lebo yake Billionea Kid, Harmonize (2019) akaanzisha Konde Music Worldwide na Rayvanny (2022) akaanzisha Next Level Music (NLM).

Hata hivyo kipindi Harmonize ametoka kwenye lebo hiyo alitozwa faini ya Sh 115 milioni. Aidha uwepo wa Mbosso WCB akiwa ametokea kwenye kundi la Yamoto Band umekuwa chachu ya mafanikio yake kimuziki. Kwani hadi sasa ametoa albamu moja akiwa chini ya WCB na nyimbo nyingi zilizofanya vizuri.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags