Ndivyo tunavyoweza kusema kufuatia mwanamuziki wa Canada, Justin Bieber (31) anayefanya shughuli zake nchini Marekani kuendelea kuandamwa na mambo ambayo yanatishia hatima ya sanaa yake na kuleta wasiwasi kwa wanaomzunguko.
Watu wake wa karibu wameuambia mtandao wa People wiki hii kuwa msanii huyo anakabiliwa na changamoto nyingi zinazotokana na kufanya maamuzi mabaya yanayoathiri uhusiano wake na watu, fedha na biashara.
Hayo yanajiri wakati kukiwa na habari zinazodai kuwa Bieber ana deni la mamilioni ya dola kutokana na kughairisha ziara yake ya Justice mwaka 2022, hivyo waandaaji wanataka kulipwa fidia.
Lakini ripoti za ndani zinasema kuwa Bieber anapitia hali ngumu kihisia, miongoni mwa mambo yanayompa mfadhaiko mkubwa ni pamoja na kesi zinazomkabili rapa Sean 'Diddy' Combs ambaye alikuwa na ukaribu naye hasa miaka ya 2010.
Pia kuvurugika kwa uhusiano wake na aliyekuwa meneja wake, Scooter Braun aliyetangaza kuachana na usimamizi wa kazi za staa huyo wa kibao, Never Say Never (2011) mwaka uliopita, ni kati ya mambo yanayomkosesha usingizi.
Lingine liloacha maswali na kuonyesha wazi kuwa Bieber hayupo sawa hasa na washirika wake wengi kibiashara ni hatua ya kutangaza hadharani kupitia Instagram kuwa ameacha kufanya kazi na chapa ya mitindo ya Drew House.
"Mimi Justin Bieber sijihusishi tena na chapa hii [Drew House], hainiwakilishi tena mimi au familia yangu au maisha yangu," aliandika katika Insta Story hapo Aprili 10.
Hata hivyo, mshindi huyo Grammy mara mbili yuko mbioni kuzindua chapa yake mpya ya mavazi iitwayo SKYLRK. Mtu wake wa karibu amedokeza bila kutaja tarehe rasmi ya mradi huo mkubwa kuanza.
Habari hizi mpya zinaibuka baada ya mmoja wa watu waliokuwepo katika menejimenti ya Bieber hapo awali kuuambia mtandao wa The Hollywood Reporter kuwa msanii huyo amepoteza mwelekeo wa kibiashara.
"Tunamuona akipotea hivi hivi... ni kama kutazama mfano halisi wa mtu asiyeishi kusudi lake. Amepotea, hakuna anayemlinda kwa sababu hakuna mtu anayetaka kuwa karibu naye, unapomwambia hili hapana, anakufukuza," chanzo hicho kilieleza.
Chanzo hiki ndicho kimeibuka madai ya Bieber kudaiwa mamilioni ya dola baada ya kughairisha ziara yake ya kimuziki ambapo alitarajiwa kufanya matamasha kadhaa lakini wawakilisha wake wameimbia People kuwa madai hayo ni ya uongo.
Ikumbukwe Justin Bieber alivuma zaidi kimuziki duniani kupitia albamu yake ya kwanza, My World 2.0 (2010) iliyoshika namba moja Billboard 200 na kumfanya kuwa msanii mdogo zaidi kuongoza chati hizo baada ya miaka 47.
Na albamu hiyo ndio iliyotoa wimbo wake maarufu 'Baby' akimshirikisha Ludacris, video yake ambayo ilikuwa na mastaa kama Drake, Lil Twist na Tinashe, imetazamwa YouTube mara bilioni 3.3 ikiwa ni video ya 39 iliyotazamwa zaidi duniani kwa muda wote.

Leave a Reply