Msanii wa Bongo Fleva Suma Mnazaleti amesema kinachopelekea baadhi ya wasanii kupotea kwenye gemu ni ukimya na kuchukua mapumziko kwenye muziki.
Wakati akizungumzia hilo msanii huyo ametolea mfano ukimya wake wa miaka sita ulivyoathiri muziki wake na maisha binafsi.
"Athari zilikuwa kubwa muda ambao mimi napumzika ni muda ambao mimi nilikuwa nafanya vizuri sana kwenye geme. Kwahiyo kitendo cha kutokuwa active kilinishusha chart na watu wengine waliokuwa wanapambana wakapanda. Hata ambao tulitoka nao pamoja.
"Nilipoteza hata wa penzi pia wanawake walinikimbia kwa ajili ya ule umaarufu uliopotea, unaposhuka chati msanii unapata msongo wa mawazo. Kwa sababu unakuwa hujioni kwenye ile pick kwahiyo ukiwa hauna ubongo mkubwa wakufikiria mambo kwa kina unaweza ukaharibikiwa," amesema Suma.
Amesema kutokana na hilo msanii yeyote wa zamani kushirikiana na msanii anayefanya vizuri kwa sasa lengo huwa kutambulika kwa mashabiki wa msanii huyo.
"Unapokuwa kwenye chati kwa wakati wako unakuwa na mashabiki wako lakini siku zinavyoenda mbele inakuja fanbase mpya. Unachohitaji msanii ni kufanya collabo na msanii aliyepo kwenye wakati sio kwa sababu akunyanyue ni kwa sababu unahitaji mashabiki wapya wakusikie. Pia wakujue,”anasema
Hata hivyo msanii huyo amesema kwa upande wa , Dullysykes imekuwa ngumu kushuka kimuziki kutokana na kukubali kwake mabadiliko.
" Dully ni miongoni mwa wasanii wa kwanza kwenye muziki wa Tanzania maana kina Fid Q, marehemu Ngwea wanakuja wanamkuta Dully tayari ni staa. Lakini alijifunza kwamba nyakati zikibadilika inabidi uwafuate hawa vijana uendane nao sawa,”anasema
Aidha, Suma amewashauri wasanii ambao wapo kwenye chati kwa sasa kufanya uwekezaji kwani nyakati hazidumu.
"Kwenye maisha watu hawashauriki, kila mtu anajua jinsi ya kuzingatia maisha yake. Hata mimi pia kuna miaka nilikuwa nashauriwa nijenge nyumba hata mbili tatu kwa sababu kuna wakati nilikuwa napata hizo hela za kuweza kujenga.
“Marehemu bibi yangu alikuwa anaona naweza kununua viwanja kadhaa na kufanya ujenzi na alikuwa anapigania sana hiyo vita lakini sikufanikiwa nikawa mtu wa kasino, bata likalika,”anasema
Suma ni miongoni mwa wasanii wa ambao hawajakubali kuutelekeza muziki licha ya changamoto wanazopitia. Utakumbuka kati ya kazi alizowahi kuachia ni Chukua Time akiwa na Ommy Dimpoz, Agano Jipya, na nyingine nyingi lakini pia ameendelea kushirikiana na wasanii wa kizazi kipya kama Lody Music, Young Lunya, Chino Kidd na wengine wengi.
Leave a Reply