Mtoto wa kwanza wa msanii Jose Chameleon, Abba Marcus ameweka wazi kuwa baba yake anasumbuliwa na maradhi ya kongosho (Acute Pancreatitis) iliyosababishwa na uraibu wa pombe kali kwa muda mrefu.
Abba Marcus ameweka wazi kupitia video aliyoiweka kwenye mitandao ya kijamii huku akiwalaumu zaidi familia ya baba yake kwa kushindwa kujali hali ya mtoto wao na kuwaacha marafiki wa Jose wakihangaika zaidi kwa ajili ya afya yake.
Kwa mujibu wa madaktari na wataalamu, endapo Jose Chameleone hatoacha unywaji wa pombe huenda akawa na miaka miwili tu ya kuishi.
"Natamani kila mmoja afahamu kuwa kama baba yangu ataendelea na unywaji wa pombe kwa mujibu wa madaktari hatochukua miaka zaidi ya miwili kuishi, hii inaniumiza sana kwa sababu huyu ndio baba yangu niliyemfahamu kwa muda wangu wa maisha," amesema Marcus.
Abba aliwataka mashabiki na marafiki wa baba yake kumpa ushirikiano ili kuimarisha afya yake na ustawi wake kwa ujumla.
"Tunatakiwa tushirikiane ili kumpa baba yangu msaada anaohitaji, nimekerwa, nina hasira sana na baba yangu kwa sababu nahisi anafanya maamuzi ya ubinafsi, nina ndugu wanne hivyo baba yangu anahitaji kuwa hai ili kunitunza mimi na ndugu zangu,” amesema Abba.
Abba pia aliwataka wakosoaji kuacha kumshikilia mama yake Daniella kuwajibika kwa afya ya baba yake akisisitiza kuwa hana uhusiano wowote na afya ya mwimbaji huyo.
Leave a Reply