Tangu ametoka kimuziki Marioo amekuwa na mwendelezo wa kufanya vizuri ukiwa ni mwaka wa sita sasa kitu ambacho kimewashinda wasanii wengi ambao huvuma kwa muda kupitia nyimbo chache kisha kupotea.
Ila kwa Marioo imekuwa tofauti, tangu mwaka 2018 ni ngoma jua ya ngoma na nyingi ni za moto hadi kumpatia tuzo nne za muziki Tanzania (TMA) huku akiwa na albamu mbili mkononi ambazo zimempa heshima kubwa. Fahamu zaidi.
Marioo alianza kung’aa kimuziki baada ya kuurudia wimbo wa Lameck Ditto, Moyo Sukuma Damu (2016) ambao ulimvutia Prodyuza Emma The Boy na kumuomba Ruge Mutahaba ampe nafasi pale Tanzania House of Talent (THT).
Mwaka mmoja baadaye alikuja kutoka na ngoma yake, Dar Kugumu (2018) iliyotayarishwa na Abbah, huku akimwandikia Lameck Ditto wimbo mmoja, Nabembea (2017) uliofanya vizuri.
Hadi sasa Harmonize ndiye mwanamuziki Bongo ambaye ameshirikiana mara nyingi zaidi na Marioo, wawili hao tayari wametoa nyimbo nne pamoja ambazo ni Naogopa (2022), Away (2024), Disconnect (2024) na Wangu (2024).
Stans ambaye amesikika katika wimbo wa Marioo, 2025 (2024), ndiye msanii wa kwanza kumsaini na kumtambulisha katika kupitia rekodi lebo yake ya Bad Nation.
Marioo amewaandikia nyimbo wasanii kama Nandy (Wasikudanganye), Christian Bella (Pambe), Gigy Money (Papa), Dogo Janja (Banana), Lyyn (Chafu), Shilole (Mchakamchaka), Mwasiti (Bado), Amber Lulu (Jini Kisirani) n.k.
Marioo ni msanii wa tisa Tanzania kufikisha wafuasi (subscribers) zaidi ya milioni 1 katika mtandao wa YouTube akiwa ametanguliwa na Diamond Platnumz, Harmonize, Rayvanny, Mbosso, Zuchu, Alikiba, Lava Lava na Nandy.
Mtoto wa kwanza wa Marioo na Paula, Princesss Amarah ambaye ana umri wa miezi saba sasa ndiye mtayarishaji mkuu wa albamu ya pili ya Marioo, The Godson (2024) iliyotoka na nyimbo 17.
Wakati ile ya kwanza, The Kid You Know (2022) mtayarishaji mkuu alikuwa ni Abbah ambaye kamtoa kimuziki na ndiye Prodyuza aliyetengeneza nyimbo zake nyingi zaidi hadi sasa.
Hadi sasa Marioo ameshinda tuzo nne za TMA kwa misimu miwili tofauti tangu kurejea kwake 2021 baada ya kusimama 2015, wasanii wengine walioshinda idadi hiyo ya tuzo kwa misimu miwili ni Nandy, Phina na Young Lunya.
Mbosso alipaswa kusikika katika albamu ya The Kid You Know (2022) ila wimbo waliorekodi Marioo hakuutoa, kitu hicho kimeleta bifu la chini kwa chini kati ya Marioo na WCB Wasafi na hadi leo hajaweza kufanya kazi tena na msanii mwingine wa lebo hiyo.
Mpenzi wa Marioo na mzazi mwenziye, Paula, binti wa Kajala Masanja na P-Funk Majani, hadi sasa ndiye mrembo aliyetokea katika video nyingi zaidi za mwanamuziki huyo kutoka Bad Nation.
Paula ambaye kwa mara ya kwanza alionekana katika video ya Rayvanny, Wanaweweseka (2021), ametokea katika video tano za Marioo ambazo ni Lonely (2023), Tomorrow (2023), Sing (2023), Hakuna Matata (2024) na Unanchekesha (2024).
Ni wazi Marioo na Paula wanapita njia ya Rayvanny na mpenzi wake na mzazi mwenzie, Fahyma ambaye wamefanya video sita pamoja ambazo ni Kwetu (2016), Natafuta Kiki (2016), Siri (2017), Forever (2023), Habibi (2023) na Mwambieni (2023).
Utakumbuka wawili hao walifanya video ya Hakuna Matata (2024) wakati Paula akiwa na ujauzito wa mtoto wao Amarah, hiyo ni sawa na Nandy alipomuweka mumewe Billnass katika video yake, Napona (2022) wakati akiwa na ujauzito wa mtoto wao Naya.
Leave a Reply