Je, wajua kuwa video tisa za muziki Tanzania ambazo zimetazamwa zaidi ya mara milioni 100 katika mtandao wa YouTube, saba kati ya hizo zimeongozwa na Director mmoja ambaye ni Kenny chini ya Zoom Extra?.
Jina la Director Kenny lilipata umaarufu zaidi baada ya kufanya kazi na Harmonize kipindi bado yupo na WCB Wasafi, ndani ya muda mfupi kazi yake ikawavutia na wasanii wengine wa lebo hiyo na ndipo mchezo ukabadilika.
Yeye na Harmonize walifahamiana kipindi anafanya kazi chini na Director Hanscana kama msaidizi, video ya kwanza Kenny kufanya peke yake ni yake Lava Lava, Dede (2017), kisha Nishachoka (2017) ya Harmonize.
Hadi sasa amefanya kazi na wasanii kama Diamond Platnumz, Alikiba, Rayvanny, Marioo, Zuchu, Aslay, Nandy, Mbosso, Jay Melody, Vanessa Mdee, Mwana FA, Darassa, Ruby, Mac Voice, Jux na Mimi Mars.
Wengine ni Professor Jay, Ben Pol, AY, Dully Sykes, Young Lunya, Baba Levo, Queen Darleen, Mr. Blue, Khadija Kopa, Q Chief, RJ The DJ, Barakah The Prince, Mrisho Mpoto, Lulu Diva n.k.
Kazi yake imepelekea kushinda tuzo mbalimbali za kimataifa kama Muongozaji Bora wa Video, ameshinda All Africa Music Awards (AFRIMA) 2019, African Entertainment Awards USA 2021, African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) 2021 n.k.
Ndani ya miaka nane ya kufanya kazi hii, moja ya mambo ambayo Kenny anajivunia na amefanikiwa, ni kuweza kuwapatia wasanii wa Bongofleva picha safi kama ile ambayo walikuwa wanafunga safari kuifuata katika mataifa mengine hasa Afrika Kusini.
Kubwa zaidi kati ya video zaidi ya 70 ambazo ameongoza tangu 2017 hadi 2024, zimetazamwa zaidi ya mara bilioni 2 YouTube akiwa ndiye muongozaji (director) pekee wa video za muziki Tanzania na Afrika Mashariki mwenye rekodi hiyo.
Unapaswa kujua kati ya video tano za Diamond ambazo zimetazamwa zaidi ya mara milioni 100 YouTube, Kenny kaongoza nne ambazo ni Yope Remix (2019), Inama (2019), Waah! (2020) na Jeje (2020) ambayo iliongoza Afrika kwa kutazamwa mwaka huo.
Na video nyingine za wasanii wa Bongofleva zilizotazamwa zaidi ya mara milioni 100 YouTube ambazo Kenny kafanya ni Kwangwaru (2018) ya Harmonize, Sukari (2021) ya Zuchu, na Number One (2020) ya Rayvanny, mshindi wa BET 2017.
Video mbili za Bongofleva zenye namba sawa na hizo ambazo Kenny hajahusika nazo, ni Nana (2015) yake Diamond ikiongozwa na Godfather wa Afrika Kusini, pia kuna Enjoy (2023) ya Jux ikiongozwa na Fole X aliyeshinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2023.
Wakati Diamond akiwa msanii namba mbili Afrika aliyetazamwa zaidi YouTube nyuma ya Burna Boy kutokea Nigeria, Kenny amehusika pakubwa katika rekodi hiyo ambayo inaipa heshima kubwa Bongofleva.
Huko YouTube, mtandao wa kucheza video ulioanzishwa Februari 14, 2005, huko San Mateo, California nchini Marekani, kwa ujumla video za Diamond zimetazamwa zaidi ya mara bilioni 2.8 huku Kenny akichagia zaidi ya nusu ya namba hizo.
Ikumbukwe Agosti 2023 ndipo Burna Boy alimpiku Diamond, hiyo ni baada ya kutazamwa mara bilioni 2.241 YouTube huku Diamond akiwa na bilioni 2.240, ila licha ya kupoteza rekodi hiyo Diamond ameendelea kusalia kuwa kinara Afrika Mashariki na Kati.
Baada ya kuchana na Zoom Extra, zamani Zoom Production ambayo ipo chini ya WCB Wasafi hapo Januari 2022, Kenny alifungua kampuni yake, DK Company Limited ambayo moja ya huduma inazotoa ni pamoja na kutengeneza video za muziki.
Chini ya himaya hii mpya Kenny ametoa video kama Nakupenda (Jay Melody), Sumu (Alikiba), Napona (Nandy), Hakuna Matata (Marioo), Single Again (Harmonize), I Dont Care (Darassa), Hapa (Ibraah), Lala (Mimi Mars), Follow Me (Aslay) n.k.
Na baadhi ya wasanii wa kimataifa aliofanya nao kazi ni Wizkid, Burna Boy, Davido, Rema, Joeboy, Mr. Flavour, Koffi Olomide, Innoss'B, Makeda, Jah Prayzah, King 98, Sho Madjozi, Jay Rox, Jose Chameleone, Fik Fameica, Bahati, Nai Boi, Tanasha Donna n.k.

Leave a Reply