Jeshi la polisi lakanusha  Ebitoke kutekwa

Jeshi la polisi lakanusha Ebitoke kutekwa

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara limekanusha madai ya msanii wa vichekesho Ebitoke kutekwa na watu aliowataja kwenye ukurasa wake wa Instagram, kama ilivyoelezwa.

Akizungumza Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Mtwara jana, Issa Suleiman kuwa Anastanzia Exavery Mahatane (27) almaarufu Ebitoke alifika mkoani Mtwara tangu mwezi Aprili 2025 na kufikia katika hoteli moja iliyoko Msanga Mkuu na kuomba hifadhi kwa watu waliokuwa wanafahamiana kabla ya maisha yake kumwendea vibaya.

Taarifa hiyo ilifafanua kuwa, “Tarehe 30 Julai mwaka huu, mtu mmoja aitwaye Anastanzia Exavery Mahatane (27), maarufu kama Ebitoke ambaye ni msanii wa komedi hapa Tanzania, mkazi wa Dar es Salaam, ambaye kwa sasa anaishi katika Kata na Kijiji cha Msanga Mkuu Wilaya ya Mtwara, alichapisha taarifa katika akaunti zake za mitandao ya kijamii ikiwamo Instagram kuwa yeye kwa sasa yupo Mtwara na kwamba ametumbukizwa katika shimo huko kwenye fukwe za Msanga Mkuu na kwamba wapo watu ambao aliwataja kwa majina kuwa wanataka kumuua.”

Aidha, “Kwa kuwa Jeshi la Polisi jukumu lake la msingi ni kulinda raia na mali zao, lilianza uchunguzi wa haraka sana ilikujua ukweli wa taarifa iliyotolewa na Anastanzia Mahatane.”

Katika uchunguzi wa awali, limebaini kwamba ndugu Anastanzia Mahatane alifika mkoani Mtwara tangu mwezi Aprili 2025 na kufikia katika hoteli moja iliyopo Msanga Mkuu na kuomba hifadhi kwa watu waliokuwa wanafahamiana kabla ya maisha yake kumwendea vibaya huko alikokuwa.

“Kwamba tarehe 31 Julai saa 11:00 jioni Jeshi la Polisi mkoa wa Mtwara lilimkamata Anastanzia Mahatane huko katika fukwe za Msanga Mkuu akiwa katika hali inayoonekana kuwa amechanganyikiwa na wala hakuwa ametumbukizwa katika shimo wala kutekwa kama ambavyo alivyokuwa ameeleza katika mitandao hiyo ya kijamii.”



“Anastanzia Exavery Mahatane amefikishwa katika Hospitali ya Mkoa wa Mtwara kwa ajili ya matibabu. Jeshi linawaomba ndugu na jamaa wa Anastanzia Exavery Mahatane maarufu Ebitoke kufika Mkoa wa Mtwara kutoa msaada au kumchukua ndugu yao,” imeeleza taarifa hiyo.

Ikumbukwe siku mbili zilizopita Ebitoke alichapisha ujumbe katika mitandao yake ya kijamii akieleza rafiki yake anayefahamika kwa jina la Lola anataka kumuua.

“Natuma meseji kwa familia yangu, naposti kwenye mitandao yangu ya kijamii, mimi niko Mtwara mkiona nimetekwa au nimepotea mjue nimeuliwa na Lola ambaye ni Flora. Akishirikiana na Lucas ambaye ndiye mume wake pamoja na kaka yake ambaye ni Kevin wakishirikiana na wafanyakazi wao ambao ni Yosia, Beni Gujo na Eva.
Mashabiki zangu mkiona sipo duniani mjue nimeuliwa na Lola naapia kwa jina la mwenyezi Mungu na mama yangu.

“Hivyo mnisaidie kupigania haki yangu. Mama yangu nakupenda sana wewe pamoja na ndugu zangu. Mama yangu rafiki yangu Lola ndiyo kaniua kwa kujifanya ananisaidia kumbe amenitupa kwenye shimo ambalo lipo kwenye beach yake ambayo nimekuwa nikiitangaza, naombeni mnisaidie kupambania haki yangu,” imeeleza taarifa hiyo.

Aidha, Jeshi la Polisi limeagiza ndugu wa mchekeshaji na mtengeneza maudhui, Anastanzia Exavery Mahatane maarufu Ebitoke kufika mkoani hapo kwa ajili ya kumchukua ndugu yao.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags