Mwanamuziki wa Bongo Fleva nchini, Diamond Platnumz ambaye kwa sasa anatamba na wimbo wake wa ‘Down’, ameweka wazi sababu kubwa inayomfanya awekeze nguvu katika shughuli mbalimbali nje ya muziki, akisema hana imani sana na biashara ya muziki.
Wakati alipokuwa kwenye mahojiano na ‘Revolt’ ameeleza kuwa biashara ya muziki haieleweki ndio maana anaamua kujichanganya katika biashara nyingine mbalimbali ikiwemo sabuni, lebo, kituo cha redio na televisheni nk.
“Siamini sana katika Muziki maana ukitegemea muziki siku moja usipoachia wimbo ambao utatrenda basi jua umekwisha. Muziki kwangu ni mtaji wa kuanzia ili niwe na maisha bora mimi na familia yangu,” amesema Simba
Akizungumza kuhusu ‘Komasava’ kukubaliwa na mastaa kutoka Marekani akiwemo Travis Scott na Chris Brown ameeleza kuwa hakuwahi kufikiria kama wimbo huo ungekuwa mkubwa kiasi hicho.
“Sikuwa na matarajio makubwa, lakini ilinithibitishia kwamba kila kitu kinawezekana. Nitaendelea kufanya kazi kwa bidii na ubunifu.
“Sikumbuki ni lini nilitoa albamu mwisho, lakini mwaka huu nitatoa albamu yangu mpya yenye sauti za kipekee na ushawishi wa wasanii mbalimbali,”amesema Simba
Mbali na hilo amegusia kuhusu kupiga show katika jukwaa la kimataifa la HOT 97 Summer Jam mwaka 2025 ambapo ameeleza kuwa limemletea heshima kubwa katika muziki.
“Ni heshima kubwa kwangu kuwakilisha muziki na utamaduni wa Afrika. Tulikuwa tunaangalia katika televisheni zamani, sasa tupo hapa tukiwakilisha bara letu. Nawataka Waafrika wote waje na kuunga mkono, siyo Waafrika tu, bali kila mtu anayependa muziki wa Afrika na Kiswahili,”amesema
Diamond pia alieleza namna alivyofanya kazi na kutia bidii ili kufanikisha ndoto yake ya kuwa msanii mkubwa.
“Nilimwambia mama yangu sitaki kuendelea na shule, nataka kufanya muziki. Familia yetu ilikuwa maskini, hivyo ilikua vigumu kupata pesa za kwenda studio. Nilijaribu kuuza nguo, kufanya kazi kituo cha mafuta, hata kuiuza pete ya dhahabu ya mama yangu ili niweze kulipia muda wa studio.
“Nilianza kufanya muziki kwa sababu niliupenda, na watu wakaanza kuniamini, walisema ‘Unaweza, unaweza kufanya hivi.’ Nilihisi wimbo wa wasanii wengine haukuwa na kitu cha kipekee, nilitaka kuthibitisha kwamba kila kitu kinawezekana na kuhamasisha watu kutoka sehemu yangu,”amesema Diamond

Leave a Reply