Peter Akaro
Imekuwa ajabu kuona wimbo wa Rayvanny, Nesa Nesa (2024) uliotoka takribani miezi mitatu iliyopita ukirejea tena katika chati na sasa challange zake zimeshika kasi katika mtandao wa TikTok uliojizolea umaarufu kwa kupaisha nyimbo mpya.Wimbo huo ambao kawashirikisha Diamond Platnumz na Khalil Harrison kutokea Afrika Kusini huku S2kizzy akiwa mtayarishaji, ulijumuishwa katika albamu yake ya pili 'The Big One' ambayo ilitoka Desemba 23, 2024 chini ya Ziik Media na NLM.
Hatua hii ni mwendelezo wa Diamond na S2kizzy kuacha alama katika muziki wa Rayvanny maana baadhi ya kazi ambazo wamewahi kufanya pamoja hapo awali zimewahi kuwa na matokeo ya kushtua.
Utakumbuka Diamond ndiye alimtoa Rayvanny kimuziki chini ya WCB Wasafi kupitia wimbo wake, Kwetu (2016) baada ya kusota sana Tip Top Connection bila kupata fursa ya kuwika kimuziki licha ya jitihada nyingi alizofanya.
Chini ya WCB Wasafi, Rayvanny akawa msanii mkubwa na chapa yenye ushawishi akishinda tuzo za kimataifa kama BET (Marekani) 2017, Zikomo (Zambia) 2022, Afrimma (Marekani) 2022, EAEA (Kenya) 2022, DIAFA (Dubai) 2022 n.k.
Licha ya kushinda tuzo ya BET, hakuna ubishi kuwa mafanikio ya Rayvanny kimataifa yalianza baada ya kuachia wimbo wake, Tetema (2019) uliyotengenezwa na S2kizzy wa Pluto Republic, huku akimpa shavu Diamond, mshindi MTV EMAs mara tatu.
Video yake hadi sasa imetazamwa zaidi mara milioni 89 YouTube ikiwa ni ya pili kwa Rayvanny kupata namba kubwa katika mtandao huo baada ya kupitwa na ile ya wimbo, Number One (2020) akimshirikisha Zuchu ambayo imetazamwa zaidi ya mara milioni 103.
Wimbo huo ulifika mbali na kumvutia mwanamuziki mkubwa duniani kutoka Colombia, Maluma ambaye aliupenda na kuomba kurudia sehemu yake, ndipo akatoa ngoma, Mama Tetema (2021) akimshirikisha mwenye wimbo wake ambaye ni Rayvanny.
Toleo hili jipya lilifanya vizuri likishika namba moja Billboard Mexico Airplay, hivyo Rayvanny kuwa msanii wa kwanza nchini kuingia chati hizo, na mara ya pili kwa upande wa Billboard baada ya hapo awali kutamba Billboard Top Triller Global Chart.
Na wimbo huo ndio ulimpa Rayvanny nafasi ya kutumbuiza katika hafla ya tuzo za MTV EMAs 2021 huko Hungary akiwa na Maluma, hivyo kuandika rekodi kama msanii wa kwanza Afrika kufanya hivyo.
Baada ya kuondoka WCB Wasafi, Rayvanny alitoa wimbo, Nitongoze (2022) ukitayarishwa na S2kizzy huku akimshirikisha Diamond, huu nao ulifanya vizuri hadi kushinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) kama Wimbo Bora wa Kushirikiana 2022.
Hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza katika historia kwa Rayvanny kushinda TMA maana tuzo hizo zilikuwa zimesimama tangu mwaka 2015 hadi zilipokuja kurejea tena 2022 kwa msaada wa serikali baada ya wasanii na wadau kuomba sana zirejeshwe.
Kwa muktadha huo, kila ambapo Diamond na S2kizzy wanahusika katika kazi ya Rayvanny, basi tegemea maajabu au rekodi ambazo zimekuwa zikiacha alama kubwa katika muziki ambao umesikilizwa zaidi ya mara milioni 300 katika mtandao wa Boomplay.
Utakumbuka hadi sasa Rayvanny na Diamond wameshatoa nyimbo 10 pamoja ambazo ni Salome (2016), Iyena (2018), Mwanza (2018), Tetema (2019), Timua Vumbi (2019), Amaboko (2020), Woza (2020), Nitongoze (2022), Yaya (2023) na Nesa Nesa (2024).
S2kizzy ambaye alianza kuvuma baada ya kutengeneza mdundo wa wimbo wa Country Boy, Aah Wapi (2016), kati ya nyimbo hizo 10 amehusika kutengeneza tano ambazo ni Tetema, Amaboko, Nitongoze, Yaya na Nesa Nesa.
Ikumbukwe wimbo wa kwanza kwa S2kizzy kurekodi na Diamond ni Far Away (2018) akimshirikisha Vanessa Mdee, na tangu wakati huo wametoa kazi nyingi zilizofanya vizuri ikiwemo Komasava (2024) ulioingia Billboard U.S Afrobeats Songs ukiwa ni wimbo kwanza kutoka Tanzania kuingia katika chati hizo.
Leave a Reply