Kupeana tafu ndio mpango mzima kwenye maisha, hiyo imejidhihirisha kwa baadhi ya wasanii wa muziki nchini ambao wamezibeba historia za mafanikio ya wasanii.
Katika historia ya baadhi ya mastaa ndani yao kuna majina ya wakali wengine.
Dongo Janja, Madee ndiye msanii wa kwanza kuamini kipaji cha Dogo Janja na kumuweka kwenye ramani ya muziki.
Kwa mujibu wa Janjaro anasema mwaka 2009 ndio kwa mara ya kwanza alikutana na Madee akiwa na wasanii wengine walipo kwenda Arusha kwaajili ya show ndipo Janjaro alipoomba nafasi ya kuonesha uwezo wake wa kuchana japo wengi walimbeza kutokana na umri wake.
Lakini alipopata nafasi aliwaacha midomo wazi na huo ndio ukawa mwanzo wa Madee kumsaidia Dogo Janja mpaka sasa ni miongoni mwa wasanii wali fanikiwa sana. Madee ni kama Baba kwenye muziki wa Janjaro.
Roma - Moni Centrozone, wimbo wa Usimsahau Mchizi ndio ulikuja kupiga tiki na kumtambulisha kisawa sawa Moni Centrozone kwenye gemu ya Hiphop Tanzania.
Wimbo huo ambao ni wakushirikiana uliachiwa Januari 16, 2017. Japo kuwa Malume alikuwa na ngoma zake tayari ameshatoa kama Kirikuu, Sembe Dona lakini kupitia wimbo wa Usimsahau Mchizi mitaa ikampokea.
Diamond Platnumz - Wapo wengi waliofahamika kupitia yeye kati yao ni Harmonize. Mafanikio yake makubwa aliyapata baada ya kupata tafu kutoka kwa Mondi.
Kupitia WCB Harmonize aliweza kuchota maarifa ya biashara ya muziki na uandishi.Huku naye akifanikiwa kuanzisha lebo yake inayofahamika kama 'Konde Music'.
Marioo - Chino Wanaman, inaeleweka kuwa kabla ya Chino kupindukia kwenye muziki alikuwa ni dansa wa Marioo ambapo alimtambulisha vyema kwenye ulimwengu wa muziki akicheza ngoma zake lakini pia kutumbuiza nae pamoja. Mwaka 2023 Chino aliingia rasmi kwenye muziki na kuanza kuachia ngoma kama 'Gibela'
Chino amefanikiwa kushinda tuzo kama dansa bora wa kiume kwenye tuzo za TMA mwaka 2022, lakini pia mwaka 2024 alishinda kipengele cha msanii bora chipukizi kwenye tuzo hizo.
Coutry Wizzy - OMG (Young Lunya, Conboi na Salmin Swaggs), Country Wizzy alikuwa miongoni mwa wasanii wa mwanzo kulibariki kundi la OMG ambalo lilikuwa likiundwa na rappers hao watatu kwani alisaidia kuwakutanisha na baadhi ya watu muhimu kama wasimamizi wa kazi zao akiwemo Big Sheshe lakini pia kuwapitisha kwenye baadhi ya studio japo yeye alikuwa hajajipata kiivo ila alionesha kuwasapoti.
Alikiba - ni wazi ngoma ya Nai Nai ya kwake Ommy Dimpoz ft King Kiba ilifanikiwa kumtambulisha vyema Ommy kwenye tasnia ya muziki.
Msanii Ommy Dimpoz, katika wimbo huo ambao korasi kachapa Alikiba umeonekana kumpatia mashabiki wengi wa mwanzo.
Hata hivyo, Alikiba ameendelea kutambulisha vipaji vingi kwenye muziki wa Bongo Fleva miaka ya hivi karibuni alifungua lebo yake ya muziki 'Kings Music' ambapo alifanikiwa kuwasaini na kuwatambulisha wasanii kama Killy, Cheed, K2ga, Tommy Flavour, na Vannilah ambao wote wamefanikiwa kuwakilisha vyema kila mmoja kwa nafasi yake.
Killy na Cheed walijitoa Kings Music na kwenda Konde Music kwa Harmonize ambapo napo mambo hayakuwa kama walivyotarajia wakasepa.
Hamis Mwinjuma Mwana 'FA' ndio msanii wa kwanza kuamini katika kipaji cha Maua sama zaidi ya miaka kumi iliyopita Falsafa Baba alimpigia simu Maua na kutaka kufanya nae ngoma ya 'So Crazy'.
Enzi hizo Maua hafahamiki akiwa Moshi kimasomo lakini pia alikuwa akifosi kwenye mitandao ya kijamii kutangaza muziki wake na ndipo Mwana FA alimuona na kumfungulia njia.
Hata hivyo, ushirikiano wa Maua na FA umeendelea siku hadi siku kwani wamefanikiwa kutengeneza ngoma kali kila walipokutana ikiwa ni pamoja na Gwiji, Hata Sielewi na nyingine.

Leave a Reply