Mfahamu Elissa Anayetamba Bongo Na Wimbo Wa Halali

Mfahamu Elissa Anayetamba Bongo Na Wimbo Wa Halali


Takribani miezi mitatu sasa watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini Tanzania hususani TikTok na Instagram wamekuwa wakitumia wimbo wa ‘Halali’ katika machapisho yao huku ngoma hiyo ikijizolea umaarufu hasa kipindi cha Ramadhani.

Na sasa mfahamu mwimbaji wa wimbo huo.

Jina lake kamili Elissar Zakaria Khoury, maarufu Elissa ni mwimbaji wa Kiarabu kutoka Lebanon, anajulikana kwa nyimbo zake za mapenzi na muziki wa kisasa wa Kiarabu. Alianza kujihusisha na muziki mwaka 1992 huku akipata umaarufu baada ya kuachia album yake ya pili iitwayo ‘W'akherta Ma'ak’ mwaka 2000.

Elissa anajulikana kupitia ngoma zake maarufu kama Ayshalak, Hob Kol Hayati, Maktooba Leek, na Halali huku akiripotiwa kuuza rekodi milioni 30 kwenye kila wimbo duniani kote, aidha amewahi kushinda tuzo nyingi ikiwemo World Music Award ambayo ameshinda mara tatu kama msanii wa Kiarabu aliyefanikiwa zaidi.

Mafanikio hayo makubwa hayakuja kwa kubahatisha ni kutokana na upambanaji wake pamoja na ubunifu wake wa kutumia Lugha tatu katika uimbaji ambazo ni Kiarabu, Kifaransa na Kiingereza.



Licha ya kufanya vizuri katika muziki Elissa ana Shahada ya Kwanza ya Sayansi ya Siasa kutoka katika Chuo Kikuu cha Lebanon, lakini hajawahi kutumikia taaluma yake hiyo aliyosomea kwani amejikita zaidi katika muziki na sanaa.

Mwaka 2017 aligunduliwa kuwa na saratani ya matiti (breast cancer) jambo ambalo limemfanya awe kimya kwa zaidi ya mwaka mzima ambapo mwaka 2018 alitangaza kupona kabisa ugonjwa huo.

Alishiriki safari yake ya kupambana na saratani kupitia wimbo wake wa "Ila Kol Elli Bihibouni" (Kwa Wote Wanaonipenda), ambao ulileta mwamko kuhusu ugonjwa huo kwa mashabiki wake.

Akiwa kama msanii ambaye anajihusisha zaidi katika kuimba nyimbo za mapenzi lakini kwa upande wake anatajwa kutokuwa na mahusiano wala ndoa lakini anaamini katika upendo wa kweli.

“Naamini sana kwenye upendo wa kweli kwa sababu, Upendo wa kweli ni ule unaojitolea, uaminifu na heshima. Wakati mwingine, ni muhimu kujua kwamba upendo siyo tu kuhusu hisia, bali pia ni kujenga uhusiano wa kudumu na wenye thamani,”alisema Elissa

Umaarufu wake katika mitandao ya kijamii ya Tanzania

Elissa amejizolea umaarufu mkubwa nchini Tanzania kutokana na nyimbo zake zenye mvuto na hisia. Watanzania wengi wameonyesha upendo wao kwake kupitia mitandao ya kijamii, wakishiriki nyimbo zake katika machapisho na video zao. Kwa mfano, kwenye Instagram, wimbo wake "Halali" umetumika sana katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani. (kwa mujibu wa google).

Kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii hasa TikTok na Instagram kwa Bongo wimbo huo umekuwa ukitumiwa hasa katika sherehe za ndoa pamoja na mabibi harusi waliofunga ndoa wiki chache kabla ya Ramadhani huku ukipata maoni mbalimbali.

“Isimitiii Ubahti uhalali wamechoka kupika uji”, “Ubahti uhalali hajarudi leo kula iftari yupo kwa haramu anapikiwa daku,” huku mwingine wakionesha upendo zaidi kupitia wimbo huo wakiandika “Wimbo wa kwenye harusi yangu nishapata bado bwana harusi,”, “Msipoweka wimbo huu kwenye harusi yangu hamli,”

‘Halali’ wa Elissa uliachiwa rasmi Mei 7, 2024, katika albamu yake iitwayo "Ana Sekketen" album hiyo iliyobeba nyimbo 10.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags