Kwa nyakati tofauti Diamond ameonesha mapenzi na heshima kubwa kwa muziki wa pwani, hasa mduara mtindo unaotamba zaidi kwenye sherehe za harusi za watu wa Tanga na Zanzibar.
Lakini kutokana na msanii huyo kuonesha ukubwa wake, kwa sasa muziki wa mduara umeanza kuchukuliwa kwa uzito zaidi, hasa katika mitandao ya kijamii, ambapo kutokana na baadhi ya ngoma zake muziki huo umekuwa ukipenya nje ya mipaka ya Bongo.
Kama utani, Simba alionesha uwezo wake wa kuimba nyimbo za mduara kwa mara ya kwanza miaka 10 iliyopita kupitia wimbo uitwao ‘Nasema Nawe’, akimshirikisha mkongwe wa muziki wa Taarab, Khadija Kopa.
Wimbo huo uliofichua upande mwingine wa Diamond ambapo watu wengi walikuwa wamemkariri kwa uimbaji wake wa Bongo Fleva huku wimbo huo wa mduara mpaka kufikia sasa ukitazamwa zaidi ya mara milioni 49 kwenye mtandao wa YouTube.

Aidha baada ya miaka 10 kupita mwaka 2025, msanii huyo amerudi tena kwa kishindo baada ya kuachia ngoma yake ya Mduara iitwayo ‘Kuna’ ambayo inaendelea kufanya vizuri katika mitandao ya kijamii hususani TikTok huku ukichezwa na mashabiki mbalimbali kutoka nchi jirani kama vile Kenya, Uganda, Zimbabwe. Hata hivyo, mpaka kufikia sasa Kuna imetazamwa mara milioni 1.1 huku ikishika nafasi ya pili katika chati mbalimbali kama YouTube.
Mbali na kupiga mawe mawili ya uhakika katika muziki wa mduara msanii huyo pia amekuwa akiupiga mwingi katika muziki wa Sebene, ambao una asili ya Congo huku akifanya kolabo na wasanii wa nchi hiyo akiwemo Fally Ipupa, Innoss’B, Koffi Olomide na wengineo.
Leave a Reply