Idadi ya watu wanaotumia vipodozi hapa nchini ni kubwa hasa kwa wanawake. Hata hivyo, wanaume nao baadhi wamekuwa wakitumia kwa ajili ya kujiweka katika hali nzuri kimwonekano. Wanaita urembo.
Hii imekuwa ni kawaida. Lakini, wengi hawajui kama vipodizi baadhi vina madhara makubwa na kuna uwezekano hata wa kupoteza maisha kutokana na kuzidisha au namna ya kutumia ikikosewa.
Hilo limemkuta nyota wa muziki wa dansi nchini, raia wa DR Congo, Nyoshi Al Saadat ambaye anasimulia mkasa mzima hadi kunusurika kufa kutokana na vipodozi (mkorogo).
Nyoshi anasema licha ya watu kumwona anapendeza kutokana na kujichubua kama ilivyo kawaida kwa wanamuziki na raia wengi wa nchini kwao, lakini hakuna aliyewahi kuuliza kama vipodozi hivyo vina madhara ya kufikia hatua ya mtu kufariki dunia.
Kwenye mahojiano na Mwanaspoti ameulizwa kuhusu madhara aliyowahi kupata kutokana na vipodozi anavyotumia na hapa ameeleza;
“Hili swali unaloniuliza kuhusu madhara kama niliwahi kuyapata kwa kutumia mkorogo kwa miaka kadhaa, sijawahi kuulizwa sehemu yeyote, sema watu huwa wanafurahia tu ninaposema natumia mkorogo. Sasa ngoja nikwambie, kama mimi mkorogo ulitaka kuniua kipindi cha nyuma."
"Kama kawaida yangu kutochagua vipodozi vya kutumia kwenye ngozi yangu. Kuna wakati sura yangu na ngozi yangu ilikuwa haieleweki, kumbe vipodozi vingine nilikuwa natumia vyenye sumu kutokana na zoazoa yangu ya vipodozi, haikuniacha salama kwani nilijikuta nikisumbuliwa na magonjwa ya ngozi ambayo baadaye yalikuja kugeuka na kuwa kansa ambayo ilitishia uhai wangu."
“Nilivyoona ngozi yangu inakuwa mbaya na kuharibika niliacha kutumia, ikabidi niende Muhimbili (Hospitali ya Taifa) kutokana na matatizo niliyoyapata, ilibidi madaktari wanifanyie matibabu na kuja kukaa vizuri. Baadae daktari alinimbia baadhi vipodozi nilivyochanganya vilikuwa na sumu na vingeweza kupoteza uhai wangu," ameema Nyoshi.
Hata baada ya kupata mkasa huo mzito, Nyoshi amesema hakukaa kimya na kusubiri afe bali alijikuta akihangaika huku na kule kupigania uzima wake.

Leave a Reply