Baada ya miaka miwili ya kutengana na aliyekuwa mke wake, Achraf Hakimi amefichua kwamba talaka yake na Hiba Abouk ilimfundisha mambo mengi ambayo hakuyategemea.
Nyota huyo wa PSG na timu ya taifa ya Morocco amefunguka hayo akiwa kwenye mahojiano yake ya hivi karibuni na ABTalks akiweka wazi kuwa alipokuwa kwenye ndoa hiyo alivumilia vitu vingi ambavyo kwa sasa hawezi kuvivumilia tena.
“Nilijifunza kujipenda zaidi, kujitunza zaidi, na kuwajali watu walio karibu nami. Unapokuwa kwenye uhusiano, unavumilia mambo mengi ambayo huwezi kuvumilia kwa watu wengine.
Nilijifunza hilo peke yangu. Nilipokuwa kwenye ndoa, nilivumilia mambo mengi ambayo sasa siwezi kuvumilia na nikajiuliza, kwa nini nilivumilia mambo haya. Hiyo [ndoa] ilinifundisha mengi na kunifanya kuwa mwenye nguvu zaidi, na pia kunisaidia kujua ninachotaka. Sasa najua kwamba nikiingia kwenye uhusiano, ninaweza kuumudu vizuri,” alifunguka Hakimi
Aidha alipoulizwa kama angependa kuoa tena, Hakimi aliangua kicheko huku akieleza kuwa kwa sasa ameamua kubaki kuwa single.
“Watu wengi wanasubiri hili! Ukweli ni kwamba sijui! Siko kinyume na ndoa, na bado mimi ni kijana. Niko wazi sana na kwa sasa niko single Ninajisikia vizuri. Ninafurahia muda wangu na familia yangu, watoto wangu, na mimi mwenyewe. Ni vigumu kumpata mtu sahihi! Lakini nikikutana na mtu huyo, kwa nini isiwe hivyo?,” amesema Hakimi
Utakumbuka kuwa talaka ya wawili hao ilizua gumzo kupitia mitandao ya kijamii baada ya Hiba Abouk, kutaka mali alizokuwa nazo Hakimi na kubainika kuwa nyota huyo hana utajiri wowote kwani pesa anazozipata zote zinakwenda kwa mama yake mzazi.
Hakimi (26) ana zaidi ya utajiri wa Dola milioni 24, sawa na Sh56.2 bilioni ingawa asilimia 80 ya mshahara wake anaolipwa kwa mwezi unaingia moja kwa moja kwenye akaunti ya benki ya mama yake.
Hiba Abouk na Hakimi walifunga ndoa mwaka 2020 na wamefanikiwa kupata watoto wa kiume wawili ambao ni Amin na Naim.
Leave a Reply