Uhusiano unapovunjika, wanawake ndio wanaoumia zaidi

Uhusiano unapovunjika, wanawake ndio wanaoumia zaidi

Kwa kuangalia idadi ya watu wanaoathirika kufuatia kuvunjika kwa uhusiano kati ya mwanamke na mwanaume mtu atagundua kwamba wanawake ndiyo ambao hupatwa na athari kubwa zaidi. Kwa mfano ukichukua watu ishirini, wanawake kumi ambao wameachwa na wapenzi wao na wanaume kumi ambao nao wameachwa pia na wapenzi wao, utagundua kwamba, wakati ni wanaume watatu tu kati ya hao kumi ndio  watakaosumbuliwa sana na na hali hiyo, kwa wanawake idadi itakuwa ni saba kati ya hao kumi.

Watu wengi wanaweza kukimbilia kwenye kusema hali hiyo inatokana na utegemezi wa wanawake kwa wanaume. Hii ikiwa na maana kwamba, wanaathirika zaidi kwa sababu, kwa kuachwa ina maana pia kwamba hawataweza tena kupata mahitaji ambayo walikuwa wanapewa na wanaume hao. Dhana kama hii inaweza kuwa na ukweli fulani, lakini hali halisi inakataa. Kuna wanawake ambao wana uwezo mkubwa nap pengine ndiyo wanaowalisha na kuwavisha wanaume, lakini wanapoachwa na wanaume hao huathirika sana.

Wanawake wa aina hii inadaiwa kwamba huathirika zaidi kuliko wale walio tegemezi. Kuathirika huku kwa ziada huhusishwa kwa kiasi kikubwa na ukweli kwamba wanaume ni watu wa kutoa ili kupalilia penzi, lakini hapa badala ya kutoa wanapewa na bado wanaondoka. Hili huwatanza wanawake wa aina hii. Lakini sababu ambayo huenda wengi wetu tulikuwa hatuijui kuhusiana na suala hili la wanawake kuathirika zaidi baada ya kuvunjiaka kwa penzi au kuachwa ni ‘ndoto.’ Kimaumbile wanawake huota zaidi ndoto za mchana au hufikiria zaidi kuhusu maisha yao ya kimapenzi yatakavyokuwa ukilinganisha na wanaume. Siyo kufikiria tu, bali hufikiria kwa njia inayoonyesha kuwa maisha hayo yatakuwa kama peponi.

Wanawake, wakiwa bado wasichana (baada ya kuvunja ungo) huanza kufikiria na kupiga picha jinsi busu lao la kwanza litakavyokuwa, mtu ambaye watabusiana awali. Hufikiria pia kuhusu wapenzi wao wa awali watakavyokuwana jinsi itakavyokuwa watakaposhiriki nao tendo kwa mara ya kwanza na huwa wanapiga picha ya jinsi siku yao ya harusi itakavyokuwa na watu watakaowaona.

Katika kupiga picha huko huwa  wanafikiria namna ambavyo mambo hayo yote yatakavyoenda vizuri bila doa, huwa wanajiona wakiwa wamefanikiwa katika hatua zote na hatimaye kuishi kwa raha mustarehe milele na watakaokuwa wapenzi wao. Kwa upande wa wanaume hakuna ndoto za aina hii na hata kama zipo ni kwa wachache sana, wakati kwa wanawake ni kama sehemu ya makuzi kwao.

Kwa hali hiyo, ukiacha mazingira wanamokulia wanawake, kwa sehemu kubwa hukua wakiwa na hizo ndoto zao, ambazo kwao siyo ndoto bali ukweli. Wanapokuja kwenye ukweli wa uhusiano hugundua kwamba busu la awali siyo kama walivyotegemea liwe, mpenzi wa awali siyo kama walivyomtegemea awe na wala maisha ya ndoa siyo matamu kama walivyokuwa wameota. Kwa kuwa hawakujiandaa wala kutegemea mazingira magumu ya uhusiano, hawakuwa wakiota kuhusu ugumu wa uhusiano bali wororo, wanapokutana na masuala ya kuvunja moyo kama kuachwa hubabaika sana. Kwa kuwa akilini mwao walikuwa na picha ya mafanikio katka uhusiano, kushindwa kwa uhusiano, huwafanya wajione kwamba, wao ndiyo wakosaji, wameshindwa kulinda uhusiano ambao katika ndoto zao waliamini kwamba ni mzuri na usio na doa

Ukiangalia kwa makini katika uhusiano, wanawake ndio wanaojitahidi sana kulinda uhusiano usivunjike, wao ndiyo wavumilivu zaidi, ndiyo ambao hujitahidi kuyarudisha mambo yaende sawa pale yanapokwenda kombo hata kama kufanya hivyo kunawagharimu. Yote hii ni juhudi yao ya kutaka kuishi kwa kadiri ndoto zao za kabla zilivyowaonyesha, kwamba uhusiano kati ya mwanamke na mwanaume ni mtamu, mororo na usio na chembe ya doa.    






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Shaban Kaluse

A Sales and Marketing in the hospitality Industry and also a freelance journalist, writing about love and relationships and educative articles which aims for youths, every Tuesday on Mwananchi Scoop.


Latest Post

Latest Tags