Toleo la 22 la tamasha la muziki la Sauti za Busara linalofanyika kila mwaka mwezi Februari Visiwani Zanzibar, limetajwa kuja kivingine huku likiongeza wasanii wa ndani na nje ya nchi kuweza kushirikiana kwa pamoja.
Akizuzungumza na waandishi wa habari leo Januari 21, 2024 Mkurugenzi wa Tamasha hilo Journey Ramadhan ameweka wazi kuwa tamasha hilo limelenga kuwakutanisha wasanii wa ndani na nje ili kuimarisha umoja wao.
“Tamasha la Sauti za Busara linapenda kuwakutanisha wasanii wa ndani na wa nje na hii inaenda kutengeneza na kuimarisha umoja wao na miundombinu, kuna project tunaita Swahili countes, wasanii wa ndani na nje huwa wanakaa kwa muda wa wiki moja.
"Wanashirikiana pamoja, wanafanya mazoezi pamoja na sisi tumewapa nafasi ya kishirikiana, kutokana na hii inatengeneza na kuimarisha miundombinu kati ya wasanii wa ndani na nje kushirikiana si kwa ajili ya tamasha bali sehemu nyingine,”amesema Journey Ramadhan
Aidha Journey ameweka wazi kuhusiana na matarajio ya tamasha hilo kwa mwaka 2025 huku wakiwekeza zaidi katika harakati za amani, ushirikiano na haki za kijamii.
“Sauti za Busara 2025 inatarajiwa kuwa tukio lisilosahaulika, likiwa na kauli mbiu ‘Amani ndio mpango mzima’, tunalenga kutumia nguvu ya muziki kuhamasisha amani, maelewano na kuongeza uelewa kuhusu jukumu la kubadilisha jamii kupitia muziki. Tunajivunia sana kuonyesha wasanii wa kipekee wanaoongoza katika harakati za amani, ushirikishwaji, na haki za kijamii,” amesema
Hata hivyo katika tamasha hilio mwanamuziki wa Hip Hop nchini Frida Amani ametajwa kuwa msanii wa kwanza wa kike wa hip hop atakayetumbuiza ambapo ataungana na mastaa wengine akiwemo Thandiswa (Afrika Kusini), Blinky Bill (Kenya), Christian Bella & Malaika Band (Tanzania).
Bokani Dyer (Afrika Kusini), The Zawose Queens (TZ/UK), Kasiva Mutua (Kenya), Zanzibar Taarab Heritage Ensemble (Zanzibar), Leo Mkanyia & Swahili Blues (Tanzania), Boukouru (Rwanda), Tryphon Evarist (Zanzibar), Charles Obina (Uganda) na Baba Kash (Tanzania).
Wasanii wengine watakaoshiriki ni Assa Matusse (Msumbiji), Mumba Yachi (Congo), Nidhal Yahyaoui (Tunisia), Étinsel Maloya (Reunion), WD Abo (Sudan), B.Junior (Mayotte), uKhoiKhoi (Afrika Kusini), Joyce Babatunde (Kamerun) na wengine wengi.
Leave a Reply