ODEMBA NA NDOTO YA AFYA KWA MAMA NA MTOTO

ODEMBA NA NDOTO YA AFYA KWA MAMA NA MTOTO

Miriam Odemba ni mwanamitindo anayepeperusha bendera ya Tanzania katika anga za kimataifa ambaye hivi sasa amekuwa akija nchini mara kwa mara kwa lengo la kuisadia jamii hasa watoto na wakina mama.

Odemba ambaye kwa sasa anaishi Paris nchini Ufaransa na ameanzisha taasisi yake ya Miriam Odemba Foundation (MOF) ambayo imeungana na taasisi ijulikanayo African Reflection (ARF) kwa lengo la kuisaidia jamii.

Najua mwanachuo unayetamani kufanya makubwa ndani ya jamii yako ukisoma Makala hii utapata maarifa na kutambua nini unapaswa kufanya katika kusadia watu wanaokuzunguka pindi unapofanikiwa kwa kipato.

Akizungumza na mwandishi wa makala hii, Odemba anasema kwa kuwa taasisi yake na ARF wote wana malengo ya kuisaidia jamii katika nyanja tofauti na wameona ni vema wakafanya kazi kwa kushirikiana ili waweze kuwafikia wahitaji wengi zaidi kwa haraka na uhakika.

Anasema taasisi ya ARF imebobea katika kutoa misaada ya kuchimba visima na tayari wameshaifanya kazi hiyo sehemu mbalimbali hapa nchini.

Anasema taasisi yake pia imekuwa ikijishughulisha na kutoa misaada kwenye masuala ya elimu na kujenga visima vya maji hasa katika shule zilizopo vijijini lengo likiwa wanafunzi na watoto wapate maji safi na salama.

 

“Oktoba 23, mwaka jana tulitembelea Mkuranga kwa ajili ya kutumiza ahadi ya kuchimba visima katika kijiji cha Kiwambo kwenye shule ya msingi Kiwambo ambayo ina wanafunzi 366.

“Uwepo wa kisima ambacho kinatoa maji safi na salama shuleni hapo umewaokoa wakinamama na watoto ambao wanapitia changamoto nyingi pindi wanapokwenda kutafuta maji mtoni,” anasema na kuongeza

“Pia imewasaidia wakina mama hao kuwa na afya njema kwani kila mtu anatambua maji ni muhimu katika mwili wa binadamu, maana akikosa maji safi basi afya yake inaweza kuteteleka,” anasema

Sababu zilizomfanya kujenga visima

Anasema moja ya sababu zilizomfanya ajenge visima hivyo huko vijijini ni kuona maji ya mtoni wanayotumia watoto na kina mama sio safi na salama kwa afya zao na wanakijiji kwa ujumla.

“Akina mama na watoto wanapotafuta maji kuna uwezekano wa kupata changamoto za kudhurika na wanyama wakali kama vile nyoka, pia njia inayotumika wakati wa kutafuta maji ni nyembamba na zilizogubikwa na majani marefu na utelezi wakati wa mvua hivyo ni hatari sana kwao wanapokuwa na  ndoo kichwani,” anasema.

Anasema usalama wa mtoto wa kike ni mdogo kwa kuwa mabwawa yako mbali hivyo ni rahisi kwa watu waovu kutumia fursa hiyo kufanya ubakaji na kusababisha mimba zisizokuwa rasmi ambazo zinaweza kuwapatia magonjwa mbalimbali.

“Kwa kuwa maji yanafuatwa mbali hivyo hukwamisha shughuli nyingine za maendeleo kama vile biashara, kilimo, mifugo na shughuli zingine,” anasema.

Hata hivyo anasema ukiweka changamoto hizo kando, kuna watoto wa kike hasa wanafunzi waliopo vijijini hawana uwezo wa kujinunulia taulo za kike hivyo huwafanya kushindwa kwenda shule wakati wa hedhi.

“Rai yangu kwa serikali kuondoa kodi katika taulo za kike na mashirika, taasisi tushirikiane kuwawezesha watoto wa kike kupata taulo hizo ili wawe na amani na furaha kipindi chote cha hedhi kwani jambo hilo sio ugonjwa bali ni mabadiliko katika mwili wa binti,” anasema na kuongeza

“Binafsi nawiwa sana kusaidia jamii ya wahitaji ili waondokane na hali ngumu ya maisha hivyo basi nitakaporejea Ufaransa nitahakikisha nawafikia wahisani wa nchi hiyo na nchi nyingine ili watusaidie kutimiza ahadi tulizofanya kwa wananchi huko Mkuranga,” anasema.

Awashauri wasanii nchini      

Odemba, amewataka wasanii nchini kujitokeza kwa wingi kuisaidia jamii hiyo ya kina mama, watoto na vijana kwani hayo ndio makundi yanayokutana na changamoto nyingi.

Aidha anasema, wasanii wote wanaoisaidia jamii wasifanye kwa siri bali wajitangaze ili kuhamasisha na wengine kuweza kutoa msaada huo kwa makundi hayo ili yaondokane na umaskini na changamoto zingine zinazowakabili.

“Wasanii wengi wakijitokeza na kuwasaidia wanawake, watoto na vijana watalikomboa taifa na kundi hilo ambalo linakabiliwa na changamoto likiwemo la ukosefu wa elimu, maji safi  pamoja na huduma bora za afya,” anasema.

Kuhusu taasisi yake ya Kimbia na Odemba

Taasisi hiyo ni mwendelezo wa shauku yake ya kuona Watanzania wanashiriki kikamilifu katika kufanya mazoezi kwa lengo la kuiweka miili yao vizuri kiafya pamoja na kutengeneza marafiki wapya.

“Tunaposhiriki kwa pamoja katika Kimbia na Odemba tunatokomeza maradhi madogo madogo katika miili yetu na kujiongezea afya tele,” anasema.

Kuhusu kutafuta walimbwende anasema, ameanzisha program ya kutafuta walimbwende lengo likiwa ni kuwawezesha warembo wachanga ambao hawana watu wa kuwashika mkono ili waandaliwe na kuimarishwa katika tasnia hiyo.

“Tuna lengo la kuwatafutia kazi warembo hawa katika kampuni kubwa za nje ya nchi kama vile Afrika Kusini, Ufaransa, Uingereza, Uswizi na Marekani,” anasema na kuongeza.

“Mchakato wa kutafuta warembo ukishakamilika kutakuwa na mkataba maalum kati ya mlimbwende na Odemba Model Search ili kuweka usawa baina ya wote,” anasema.

Odemba ni nani?

Odemba ni mwanamitindo maarufu duniani aliyezaliwa Arusha mwaka 1983. Kabla ya kushiriki mashindano na maonesho makubwa mbalimbali ya urembo duniani, aliwahi kuwa Miss Temeke mwaka 1997.

Mwaka 1998 alishiriki na kuingia kwenye kumi bora ya Shindano la Miss Tanzania kisha akaingia tano bora ya Shindano la M-Net Face of Africa.

Aidha mwaka 1999, Odemba aliingia kwenye 17 bora ya Shindano la uwanamitindo linalojulikana kwa jina la Elite Model Look Tanzania, ambapo safari yake ya uwanamitindo ikiaanza rasmi .






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post

Latest Tags