NDOA: Taasisi inayoua kimya kimya

NDOA: Taasisi inayoua kimya kimya

Kuna zile nyakati ambapo tunasikia au kuona kifo cha mwanandoa mmoja dhidi ya mwingine. Lakini bila shaka hivi siyo vifo vingi ukilinganisha na vile vinavyotokea bila sisi kujua. Ndoa nyingi husababisha vifo vya kimya kimya kuliko mimi na wewe tunavyofahamu.

Ndoa yenye matatizo inaweza kuwa na madhara kwenye afya yako, wakati ndoa isiyo na matatizo inaweza kukukinga na magonjwa na kukuponesha haraka na magonjwa.

John Gottman, mtaalamu anayeheshimika katika masuala ya ndoa, anaripoti kwamba, ndoa yenye matatizo, inaweza kuongeza uwezekano wa kukuletea magonjwa kwa asilimia 35! Anaamini kwamba kuitumikia ndoa yako kila siku itakusaidia zaidi kwenye afya yako au kuishi maisha marefu kuliko kutoishughulikia na ukajikuta ni mtu wa kuumwa hovyo.

Ingawa wengi wetu tunaamini kwamba hasira ni chanzo kikuu cha uhusiano mbovu, Gottman amegundua kwamba siyo hasira pekee ambazo ni tatizo, bali ni vipi tunatatua migogoro yetu kwenye ndoa.

Kutoa hasira kwa nia ya kujenga kunaweza kufanya maajabu kwa kusafisha hali ya hewa na kuurejesha uhusiano kwenye njia yake.

Hata hivyo mitafaruku huwa ni tatizo kukiwepo mambo manne ambayo ni: Kumshambulia mwenzio, (kuponda), dharau, kujitetea badala ya kuomba radhi kwa nia, na kunyamaza unapoongeleshwa na mwenzio.

 

Kuponda ni nini? Kuponda kunahusu kumshambulia mwenzio bila kujali utu wake, mahali na muda.

Ni vema kila mmoja wenu akatoa dukuduku lake, lakini usimponde na kumshambulia mkeo au mumeo, wakati mwingine mbele ya watu wengine au hata watoto.

Dharau nayo? Dharau ni hatua moja ya kumponda mwenzi wako na inahusisha pia kumuumiza. Dharau ni alama ya wazi ya kutomuheshimu mtu.

Mfano wa dharau ni pamoja na kumshushia hadhi, kukunja uso, au kumchanachana mwenzio kwa vicheko vya kebehi. Tabia hii wanayo zaidi wanawake.

Kujitetea na kutafuta visisngizio je? Kujitetea wakati ugomvi umepamba moto linaonekana ni jambo jema, lakini hakusaidii kuurejesha uhusiano mahali muafaka. Mtu anapojitetea au anapotafuta visingizio, mara nyingi anakuwa kwenye mfadhaiko mkubwa na hivyo kushindwa kusikiliza vema mambo yanayoongelewa. Kukataa kuwajibika kwa makosa yako na kutafuta visingizio ni aina mojawapo ya kujitetea.

Kunyamaza nako? Mtu anakataa kuitikia. Kwa kawaida kunyamaza kunaweza kusiwe kubaya, lakini katika masuala ya uhusiano, kunyamaza wakati wa mtafaruku kunaweza kuhatarisha ndoa yenu. Kama ni mwenye kawaida ya kunyamaza, unajiondoa mwenyewe kwenye ndoa, badala ya kutatua matatizo yenu. Wanaume wana tabia ya kunyamaza zaidi ukilinganisha na wanawake.

Kwa kweli, kwa mujibu wa utafiti wa Gottman wa matatizo manne yaliyotajwa hapo juu ni kwamba, yakibobea katika ndoa yanaweza kutumika kutabiri, kwa usahihi kwa zaidi ya asilimia 80, wanandoa wepi ndoa yao itavunjika.

Majaribio ya kutosha yakifanyika bila mafanikio kujaribu kuokoa ndoa iliyopata dhoruba ya mambo manne yaliyotajwa hapo juu, kuna uwezekano wa zaidi ya asilimia 90 wa ndoa kuvunjika.

Mbinu za kuboresha ndoa na afya yako. Ukizingatia kwamba, kuwa na ndoa imara ni kitu muhimu sana ili kuwa na afya na furaha, italeta mantiki kuelekeza nguvu zenu katika kuifanya ndoa yenu kuwa bora zaidi. Hapa chini kuna vidokezo kwa ajili ya kuifanya ndoa yako kuwa na afya zaidi:

Kwanza lea ndoa yako. Unajua mambo ayapendayo na asiyoyapenda, ndoto, hofu, wasiwasi, na matumaini ya mwenzi wako? Unajua kwa mapana ni nini mwenzi wako alifanya siku nzima ya jana? Unajua aina zipi za shinikizo mwenzi wako anazipata mahali pake pa kazi? Msingi wa ndoa nzuri ni urafiki imara.

Kama ndoa haijajengwa juu ya urafiki imara, itakuwa shida kuishi kwa pamoja kwa muda mrefu. Hakikisha unapata muda kila siku kukaa na mwenzi wako kwa siri ili kumjulia hali na matatizo aliyokabiliana nayo .

Katika vipindi hivi, weka kipaumbele kusikiliza na kujifunza kuhusu fikara, mawazo na hisia za mwenzi wako .

Pili kwa nguvu zote na kwa makusudi, chukua hatua kuboresha mapenzi kwa mwenzi wako. Gottman anasema, hiki ndicho kizuizi kikubwa cha dharau. Kumbuka mambo mazuri ya mpenzi wako.

Ulimpendea nini hadi ukaoana naye? Ni kitu gani kabla hujamuo kilikuvutia kwake kimaumbile? Kwa kurejesha mapenzi kwa mwenzio utakuwa umeboresha mwenendo bora.

Tatu, daima mheshimu mwenzi wako. Katika uhusiano ambao unaporomoka, heshima kamwe haipatikani.

Cha kusikitisha zaidi, wakati mwingine watu wanaishia kuwatendea wenzi wao vibaya zaidi kuliko ambavyo wangewatendea watu wasiowafahamu. Unamgombeza mkeo au mumeo mbele ya rafiki zako au familia?

Nne, mkubali mwenzi wako. Kumbuka kwamba kila mmoja wenu anahitaji kujisikia anakubalika kama binadamu.

Badala ya kumshambulia mkeo au mumeo, jaribu kusikiliza mawazo yake. Ni rahisi kutilia mkazo makosa ya mwenzio na kwa kufanya hivyo tunasahau mema anayofanya.

Tano, sameheaneni, mwenzio anapokuomba msamaha kwa dhati, usimkimbie au usiompe kisogo, wakati mwingine migogoro haikwepeki.

Majaribio ya kurekebisha kasoro zilizojitokeza katika uhusiano yanapopuuzwa, uhusiano unaathirika.

Usifunge milango moja kwa moja kwa mkeo au mumeo anapojaribu kujirekebisha.

Sita, tulia. Unapokuwa umeudhiwa, pumua kwa nguvu. Watu wengi wanahitaji kama dakika 20 kutuliza miili yao baada ya kuudhiwa. Baada ya kutulia chukua nafasi yako, anza upya kulishughulikia tatizo lililo mbele yako, wakati umetulia na utakuwa tayari kumsikiliza mkeo au mumeo vizuri.

Saba, chukulia mambo kirahisi. Ijapokuwa mkeo au mumeo anaweza kufanya mambo ambayo yatakuudhi, kumbuka unaweza kukabiliana nayo.

Si busara kupambana na mkeo au mumeo katika mambo madogomadogo.

Nane, jitazameni upya na kujirekebisha. Uhusiano ni kama dansi. Wewe na mkeo lazima msonge mbele sambamba. Kumbuka kwamba uwe ni mwanamke au mwanaume una udhibiti kwa asilimia 50 wa mambo yote yanayotokea katika uhusiano wenu. Ndio maana wanasema, ndoa ikifa wote mmechangia.

Ni mara chache kupindukia, ambapo mmoja kati ya wanandoa ndiye mwenye mchango.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Shaban Kaluse

A Sales and Marketing in the hospitality Industry and also a freelance journalist, writing about love and relationships and educative articles which aims for youths, every Tuesday on Mwananchi Scoop.


Latest Post

Latest Tags