Mitindo bora kwa mama mjamzito

Mitindo bora kwa mama mjamzito

Baadhi ya wanawake wanapokuwa wajawazito hujiweka kando katika masuala ya mitindo na hata urembo hali inayopelekea kupunguza mionekano yao waliokuwa nayo awali kabla ya kupata ujauzito.

Lakini wataalamu wa masuala ya mitindo na urembo wanaeleza kuwa ujauzito si kigezo cha kuacha kupendeza na kuvutia kama ulivyokuwa awali.

Akizungumza na Mwananchi mshonaji wa nguo za kike na kiume jijini Dar es Salaam, Jackline Maneno anasema kuwa na mimba siyo sababu ya kufanya kuvaa nguo zisizovutia au kuacha kujiweka katika muonekano mzuri.

“Unakuta mtu kabla ya kuwa mjamzito alikuwa akivaa nguo nzuri, anajipenda hivyo anajitahidi kutunza ngozi yake anapopata ujauzito tu anaacha, hii haiko sawa,”alisema.

Alisema ipo mishono na mitindo mbalimbali mingi ipo katika mitandao na tovuti mbalimbali za mitindo, maalum kwa ajili ya wajawazito ambayo anaweza kushona na bado akapendeza na kwenda na ‘fashion’.

Alisema jambo la msingi kwa mjamzito ni kujua na kukubali kuwa mwili wake utapitia mabadiliko mfano katika miezi ya mwanzo ya ujauzito alikuwa na mwili mwembamba anaweza kubadilika na kuongezeka kidogo mwili wake au kinyume cha hapo.

“Lakini pia ni muhimu kadri miezi inavyozidi kuyoyoma ndipo tumbo linavyozidi kuongezeka kutokana na mtoto anavyokuwa na pia anaweza kupitia mabadiliko mbalimbali kama kuvimba miguu,” alisema.

Hivyo ni muhimu katika uvaaji wake kuzingatia size za nguo na viatu anavyovaa ili kumuweka huru kutokana na hali yake.

Lakini pia aligusia wajawazito wanaopendelea kuvaa nguo za kubana na kusema kuwa mavazi hayo si sahihi kwa mama mjamzito kwani anaweza kumfanya asiwe huru na hata kuchoka kwa haraka lakini pia si salama kwa afya yake na mtoto aliyeoko tumboni.

"Mjamzito anatakiwa kuvaa nguo inayomstiri mwili wake vizuri, pamoja na kuwa nguo za kubana sana mwili ni hatari kwake lakini pia haziendani hata na utamaduni wetu wa kiafrika,"alisema.

Kauli hiyo pia imeungwa mkono na daktari wa binaadamu, Rachel Mwinuka ambaye anatueleza kuwa Mama mjamzito anashauriwa kuvaa nguo zisizobana sana ili kuuruhsu kupata mzunguko wa damu na hewa kwa urahsi.

Lakini pia aligusia suala la wajawazito kuvaa viatu virefu kwa muda mrefu na kueleza kuwa uvaaji wa viatu hivyo vinaweza kumsababishia mama maumivu ya miguu na hata kuhatarisha usalama wa mama na mtoto aliyeko tumboni

"Anaweza hata akajikwaa na kudondoka na kuweza kusababisha maumivu ya tumbo na hata kumueka katika hatari mtoto aliyoko tumboni,"alisema

Hivyo alishauri wanawake wajawazito wajitahidi kuepuka uvaaji wa viatu hivyo na wapendelee kuvaa viatu simple au flat shoes.

Nae mtaalamu wa masuala ya urembo , Isha Mtawa anaeleza kuwa katika kipindi cha ujauzito ni vyema mjamzito kuendelea kutunza afya ya nywele zake, ngozi na hata kucha na kuzingatia mavazi yake ili aendelee kuwa na muonekano wa kuvutia.

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Saphinia Suleiman

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, career, skills development and technology.


Latest Post