Miaka 10 Jela Yanukia Kwa Diddy, Akutwa Na Hatia Mashtaka Mawili

Miaka 10 Jela Yanukia Kwa Diddy, Akutwa Na Hatia Mashtaka Mawili

Baada ya jopo la majaji kutoa uamuzi usiokamilika na kuifanya mahakama kuwarudisha tena kujadili kuhusu kesi ya rapa Sean Diddy Combs, hatimaye uamuzi wa kesi hiyo umekamilika.

Julai 2,2025 jopo la majaji wakiwemo wanaume nane na wanawake wa nne walitoa uamuzi rasmi ukieleza kuwa msanii huyo amekutwa na hatia katika mashtaka mawili kati ya matano yaliyokuwa yakimkabili.

Taarifa kutoka Mahakamani hapo zimeeleza kuwa Diddy amepatikana na hatia katika tuhuma za kufanya usafirishaji unaohusiana na biashara ya ukahaba huku akifutiwa mashtaka mazito zaidi yaliyokuwa yakimkabili katika kesi hiyo ambayo yanahusiana na kuwalazimisha Wanawake kufanya ngono na wanaume wengine ambao walilipwa.

Diddy ambaye ana umri wa miaka 55, alishtakiwa kwa makosa matano shtaka mojawapo ni kula njama na makosa mawili ambayo ni biashara ya ngono na kushiriki katika usafirishaji unaohusiana na biashara ya ukahaba. Hata hivyo hakupatikana na hatia yoyote ya kula jama na kushiriki katika biashara ya ngono.

Jaji amesema Diddy hajapatikana na hatia katika kosa la njama za ulaghai, pia hajapatikana na hatia katika mashtaka ya 'ulanguzi' wa ngono wa mpenzi wake wa zamani aitwae Cassie Ventura pamoja na Jane.

Aidha kwa mujibu wa wataalamu wa kisheria nchini humo wanaeleza kuwa hatua hiyo ni nzuri upande wa Diddy huwenda akakabiliwa na kifungo cha miaka 10 hadi 20 jela kupitia makosa hayo.

Kulingana na kesi hiyo kufikia sehemu mzuri inaelezwa kuwa mawakili wa Sean "Diddy" Combs wamewasilisha ombi rasmi la kuachiliwa kwake kwa dhamana ya dola milioni 1, ambayo imedhaminiwa na mama yake, dada yake, pamoja na binti yake mkubwa.


Mawakili wa rapa huyo kupitia ombi lililowasilishwa mahakamani wametaka nyota huyo kuachiwa mara moja kwani ameonesha kuwa mpole kwenye kesi nzima bila njama za kutoroka hivyo dhamana hiyo itaambatana na kukabidhi hati yake ya kusafiria, kupunguzwa kwa safari zake katika maeneo ya Florida, California, New York, na New Jersey.


Mbali na hilo familia ya msanii huyo ikiwa nje ya mahakama ilionekana kufurahia ushindi wa baba yao huku King Combs akieleza kuwa anafuraha sana na kuwa hivi karibuni baba yao atarudi nyumbani.

Sean "Diddy" Combs alikamatwa Septemba 16, 2024 katika hoteli ya Park Hyatt, Manhattan, New York na kupelekwa moja kwa moja katika gereza la Metropolitan huko Brooklyn. Kesi yake ilianza kusikilizwa Mei 5,2025.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags