Mfahamu kocha mwanamke mwenye muonekano tofauti  wa mavazi ya kimichezo

Mfahamu kocha mwanamke mwenye muonekano tofauti wa mavazi ya kimichezo

Imezoeleka makocha wa michezo mbalimbali haswa wanawake wanapokuwa katika masuala ya kimichezo huwa wanavalia nguo za kimichezo kama vile raba, jezi, trucksuit na nyinginezo.

Hata hivyo imekuwa tofauti kwa Sydney Carter ambaye ni kocha msaidizi wa timu ya kikapu ya chuo kikuu cha Texas A&M ambaye anapokuwa akiwanoa wachezaji wake amekuwa akivalia nguo zisizoendana na maudhui ya kimichezo.

Akiwa mkufunzi wa timu, mara nyingi huonekana akiwa amevalia suti, skinjeans, minskirt, gauni fupi au ndefu, jumsuit na kinachowaacha hoi zaidi ni kuvalia nguo hizo kiatu cha mchuchumio jambo ambalo haijazoeleka katika tasnia ya michezo kwa wanawake.

Utofauti wa uvaaji wake umezidi kuwa gumzo na kumpa umaarufu zaidi katika mitandao ya kijamii haswa katika akaunti yake ya Instagramu yenye wafuasi wanaomfatilia 598000.

Baadhi yao wanafurahishwa na uvaaji wake na namna unavyomfanya azidi kuwa mrembo na wengine wakibeza muonekano wake.

Jumapili ya Februari 6 mwaka jana Carter aliweka picha katika mitandao ya kijamii ya twitter na akiwa amevalia suruali yenye rangi ya waridi na turtleneck nyeupe 

Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 31 alipokea 'comment' mbalimbali zikiwemo za kumsifia kuwa amependeza na wengine wakimbeza na kusema amevaa nguo zisizoendana na maadili ya michezo.

"Nadhani tu kwamba baadhi ya  watu hawafurahishwi na mwanamke mweusi kuwa katika nafasi fulani, wanapomuona  mwanamke mweusi ambaye anajiamini na kujikumbatia, nadhani hiyo inawaumiza"

"Wanawake hawawezi kamwe kumridhisha mtu yeyote katika nyanja yoyote ya maisha. Ni vigumu sana kwamba hatulipwi sawasawa au kwamba watu wanafikiri kwamba hatuwezi kufanya baadhi ya mambo sawa au kitu sawa na wanaume katika sekta mbalimbali" Carter alieleza hayo katika mahojiano yake na mtandao wa Yahoo alipoulizwa juu ya comment anazozipata katika mitandao ya kijamii juu ya uvaaji wake.

Malik Hamza mkazi wa Ilala jijini Dar es Salaam anasema haoni tatizo kwa mtu kuamua kujiweka tofauti na anafanya kazi yake kwa ufanisi.

“Sioni hoja ya wanaobeza uvaaji wake ikiwa anafanya kazi zake vizuri tena utofauti wake huo ndio unafanya baadhi ya watu kumjua na kumfuatilia hata mimi binafsi ‘nimemfollow’ katika akaunti yake instagram kutokana na namna alivyojiweka tofauti”

Akizungumza na Jarida hili  Dorice Maliya mwandishi wa habari na kocha wa mpira wa miguu anasema katika mafunzo ya ukocha haswa katika mpira wa miguu katika upande wa mavazi huwa wanasisitizwa kuvaa mavazi ambayo yatakufanya uonekane nadhifu lakini yanayokuweka huru kutembea, kukimbia na kufanya shughuli nyingine unapokuwa unawanoa wachezaji wako.

"Ndio maana baadhi ya makocha huwa wanapendelea kuvaa nguo za kimichezo kama track suit, au suti anapokwenda katika mechi"

Anasema pia inashauriwa kutovaa mavazi ambayo yanaweza kupelekea kuondoa utulivu na umakini kwa wale unaowafundisha katika kile unachokifundisha.

"Si vyema kuvaa nguo ambazo zitawafanya kuondoa umakini kwa kile unachokifundisha na kuanza kuangalia mavazi uliyovaa" anasema.

Anaongeza kuwa inashauriwa kuvaa mavazi ambayo yatakuwa mfano na kiigizo chema kwa wale unaowafundisha.

"Unatakiwa kuwa mfano kwa yule unaemfundisha kwa sababu wewe ni mwalimu hiyo ni pamoja na suala la mavazi"anasema.

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Saphinia Suleiman

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, career, skills development and technology.


Latest Post