Mambo ya kufanya unapoombwa rushwa ya ngono chuoni

Mambo ya kufanya unapoombwa rushwa ya ngono chuoni

Haya haya, wale wanaotarajia kuingia chuoni hivi karibuni kuna ujumbe wenu konki hapa niko nao ambao utawasaidia. Kabla sijaenda chuo nilisikia stori za walimu wanaowataka wanafunzi kimapenzi na wakiwakataa wanawafelisha, kwa hiyo kabla sijaenda nilifunga na kuomba Mungu aniepushie kukutana na walimu kama hao, nahisi ni tatizo kubwa sana kuishi kwenye dunia ambayo badala ya kuwa na furaha na kujiandaa kwenda chuo nilikuwa bize kusali ili wahadhiri ambao wanatakiwa kuwa wazazi wangu chuoni wasinitamani kimapenzi. Ila hivyo ndivyo dunia ilivyo. Kutakwa na wahadhiri inaleta mawazo sana na kitu ambacho wadada wengi chuoni wanakiogopa.

Nilipokuwa chuo tulikuwa tunasikia kuhusu watu waliokuwa wanatoka na wahadhiri, wengine kwa ajili ya maksi zao, wengine yalikuwa mahusiano tu ya kimapenzi au pesa, umaarufu na urahisi wa maisha ya chuo unaotokana na kutoka na wahadhiri.

Huwa naamini kwenye kutokumhukumu mtu, kwa vile sijui stori ya mtu na sijatembea kwenye viatu vyake, hivyo sidhani kama kumhukumu bila kumjua ni jambo sahihi mimi kufanya, ila mimi naamini kuwa uko chuo kufaulu kwa akili yako na sio kwa mwili wako, sehemu yoyote ile kwenye maisha yako hauna haja ya kutoa mwili wako.

Hizi hapa ni njia za kujiepusha na rushwa ya ngono/vitu vya kufanya ukijikuta uko kwenye mtego wa mhadhiri;

Rushwa ya ngono ni tatizo ambalo mabinti (kwasababu stori nyingi tunazosikia ni za mabinti) wanalipitia sana kutoka kwa wanaume wenye nguvu (power) kwenye sehemu ambazo wao wapo, kwa hiyo inaweza kuwa sehemu za mazoezi ya vitendo (field), inaweza kuwa ofisini unapoenda kuomba kazi lakini kabla haujafika kote huko ni lazima uwe umevuka chuo na wahadhiri wengi sana huomba rushwa hii kwa wanafunzi wa kike na kwa vile jinsi system ya chuo ilivyo mhadhiri ana nguvu ya kukufaulisha au kukufelisha, basi binti unajikuta uko kwenye mtego mkubwa sana, umkatalie ufeli, au umkubalie, ufaulu.

Kuna wasichana wengi ambao wamerudia miaka chuoni kwa sababu ya kukataa kutoa rushwa ya ngono kwa wahadhiri kwa hiyo hili swala linawaumiza mabinti, kuwapotezea muda na kuwaathiri.

Rushwa ya ngono inaweza kuwa vita ambayo mabinti wanaipigana bila kuwa na vifaa vya kupigania maana hakuna watu wanaoongelea swala hili kwa uwazi na kuwapa ideas za vitu unavyoweza kuvifanya ukijikuta kwenye hali kama hiyo, binti, leo naenda kuwashirikisha namna mbalimbali za kujiepusha na rushwa ya ngono lakini kabla sijakushirikisha ningependa ujue kuwa unaweza kufaulu, unaweza kufanikiwa kwenye maisha bila kutoa rushwa ya ngono.

Na hivyo jambo la kwanza ambalo napenda ulijue ni kuachilia hii mentality ya kuwa inabidi uutoe mwili wako ufanikiwe. Unaweza fanikiwa kwa akili zako, kwa juhudi zako, kwa nguvu zako, uthamini mwili wako sio kila mtu apite. Unaweza kuwaomba wahadhiri msaada, unaweza kuwaomba wakusaidie kukuelimisha bila ngono kuhusika, wahadhiri ni wazazi wako, wachukulie kama hivyo.

Ukikariri huu ujumbe ya kuwa hauwezi kufanikiwa mpaka utoe mwii wako, mtu akitaka rushwa ya ngono utatoa, ila ukiachana na hii mentality, ni rahisi sana ukiwa kwenye hali hiyo kutafuta suluhisho kwa njia nyingine.

Namna nyingine unazoweza kuzitumia kuepuka rushwa ya ngono ni;

  • Usitumie jinsia yako kutafuta favors zozote zile

Huwa kuna tabia vyuoni unakuta unaambiwa na wanafunzi wa kiume kuwa wewe ndio uende kuongea na mhadhiri kwa vile mwanamke atakuelewa, hapo tayari unatengeneza mazingira ya kutumia jinsia yako kutaka urahisi.

Usitumie jinsia yao kama kishawishi cha kuwatega wahadhiri wa kiume kwa lengo la kupata alama bora.

Ukifanya hivi unakuwa kwenye sehemu nzuri zaidi wa kulaumiwa kwa kukuomba rushwa ya ngono anakuwa mhadhiri pekee, wewe unakuwa haujachangia chochote kupelekea hili.

Naelewa pia muda mwingi mabinti huwa hawana mchango kwenye hili bali wahadhiri wamekuwa wakiwanyanyasa kijinsia wanafunzi wa kike kwa kuwaomba rushwa ya ngono au kuwajengea mazingira ya kuwataka kimapenzi kwa nguvu, lakini ni muhimu kujua hili pia.

  • Jiamini na jiheshimu

Una haki ya kusoma na kumaliza chuo bila kulala na mhadhiri, bila kumpa rushwa ya ngono ili akufaulishe, jiamini na ujiheshimu. Ukiona unaanza kujiuliza ‘nitapoteza nini nikilala na huyu mhadhiri?’ ujue hauoni thamani yako na haujui haki zako.

Usitafute alama za bure, soma vizuri, weka nguvu kama wanafunzi wengine ili usije kujikuta kwenye mtego huu wa wahadhiri. Zingatia maadili na usikubali kurubuniwa na haki yako kupokonywa.

  • Paza sauti ukijikuta kwenye mtego huu

Unaweza kutafuta msaada kutoka kwa dean, washauri wa wanafunzi, mwalimu wa darasa (kama unaona anaaminika), TAKUKURU n.k. Msaada upo na hili ni kosa kisheria kwa hiyo hakikisha hauruhusu utendewe kwa sababu ya woga.

Weka ushahidi, kuna wahadhiri wengi sana tu ambao wamekutana na mkono wa sheria kwa sababu wanafunzi walipaza sauti. Sheria inakulinda, paza sauti, usiumie kimya kimya, jua haki yako. Unaweza kushirikisha pia kitengo cha jinsia cha chuo chako, usijihisi hauna msaada ukiwa chuoni

  • Unganeni, muwe wazi kuzungumzia changamoto mnazopitia

Ukimya ni silaha ya mnyanyasaji, inamfanya awe na nguvu, unganeni kama mabinti vyuoni, muongelee changamoto zenu, mkiongea mtagundua kuwa mnapitia mambo yanayofanana na kwa vile umoja ni nguvu mnaweza kushinda kirahisi changamoto zenu mkiwa pamoja.

  • Mdai kuimarishwa kwa mikakati iliyobainishwa katika miongozo na sheria ndogo ndogo za kuzuia na kudhibiti rushwa ya ngono. Kama zipo tafuta kuzijua.

Kwenye vitengo vya jinsia vilivyopo chuoni, baini sheria ndogo ndogo za kuwalinda, kwa vile hili ni tatizo linalojulikana kuwa lipo, ni vizuri sheria ndogo zikiwepo vyuoni ili kuwalinda dhidi ya unyanyasaji huu wa kijinsia. Au kama sheria hizo zipo, tafuta kuzijua.

Kuna elimu kubwa inayobidi itolewe kuhusu rushwa ya ngono kwa wahadhiri, kuwa wawachukulie kuwa kama watoto wao lakini pia wajue athari za kukamatwa wakiomba rushwa hii kutoka kwa mifano ya wahadhiri waliokamatwa kwa kesi hizi, lakini kwa sasa ni muhimu binti kujiepusha na rushwa ya ngono kwa kujua haya nilioandika hapa.

Epuka rushwa ya ngono, usiharibu elimu yako na usikubali kujishusha thamani yako. Mwalimu anayekuomba wewe rushwa ya ngono anaweza dhani kuwa maisha yako yapo mikononi mwake ila ukweli ni kuwa ikijulikana analolifanya anapoteza hadi kibarua chake hicho. Hivyo usijihisi ni lazima utoe mwili wako kupata haki yako.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags