Je wewe ni mtu wa kupenda ghafla, yaani mwanaume anapokutamkia kwamba anakupenda huwa unamuamini kwa kiasi gani, unakuwa ni mwepesi wa kumuamini na kujitoa kwa ajili yake au unakuwa na kujivuta vuta ili kujiridhisha kabla ya kuingia katika uhusiano?
Hebu fikiri kabla ya kuamua, jipe muda kwani hakuna jambo lililo jema kama subira linapokuja swala la kupenda.
Subira itakuepusha kupoteza muda wako katika mahusiano ambayo hayana mashiko wakati dhamira yako ilikuwa ni kumpata mwenzi mwenye sifa muafaka, pale utakapoingia mahali ambapo sipo.
Kwa kawaida kutoka katika uhusiano huo kuna gharama kubwa na kunaweza kukusababishia matatizo mengi yakiwemo ya kiafya.
Hapa chini nitajaribu kueleza makosa kadhaa ambayo wanayafanya wanawake linapokuja swal la kupenda:
- Kumbadili mtu awe vile utakavyo:
Usije ukajidanganya kwamba unaweza kumbadilisha mtu mzima na akili zake.
Kama umepata mwanaume ambaye kwa mtazamo wako unamuona ana sifa muafaka lakini anatabia ambazo huzipendi kwa mfano ulevi au kuvuta sigara vitu ambavyo vinakukera sana, usije ukajidanganya kwamba unaweza kumbadilisha na akaacha tabia hizo, anaweza kuacha kwa muda tu ili kukuvuta ukiingia kingi imekula kwako, tabia hiyo inaweza kujirudia.
Ni vyema kama kuna tabia ambazo umezipenda lakini zipo ambazo huzipendi kutoka kwa mwenzi wako, basi weka uzingativu kwenye zile tabia unazozipendfa na zile usizozipenda achana nazo, kama ataamua mwenyewe kuziacha sawa lakini kama akiamua kuendelea nazo, basi zisikuumize kwani unaweza kujikuta ndoa yako inakuwa na migogoro isiyokwisha kwa sababu ya kuonekana una ghubu kwa kujaribu kumbadilisha mwenzi wako na mwisho wake upendo unakuwa haupo na kisirani katika ndoa kinaongezeka.
Kitendo cha kuonekana kuwa na ghubu kinaweza kumuingiza mwanaume katika tabia nyingine mbaya ya kutotumia muda mwingi kukaa nyumbani kwake na kutafuta kampani nyingine, kama akipata kampani ambayo siyo nzuri anaweza kuangikia katika nyumba ndogo ambayo itamkubali bila masharti.
- Njoo tuishi:
Unaweza kukutana na mwanaume ambaye ana nyumba nzuri au amepanga nyumba nzuri na ana kila kitu ndani pamoja na usafiri, anakuwa mwepesi kukupa funguo za nyumba yake ili uhamie muishi pamoja, lakini haweki msimamo wake wazi kwamba ana matarajio gani na wewe.
Kabla ya kukubali kupokea funguo na kuhamia kwake jiulize kama unampenda kwa dhati au umekubali kwa sababu ya nyumba yake nzuri.
Kumbuka nyumba na vitu vingine vinavyotizamika kwa macho (material things) havina mashiko linapokuja swala la kupenda. Kupenda kunahusisha vitu vya ndani kama vile kupenda kwa dhati bila masharti wala kuangalia sifa za nje, kuwa na amani moyoni kila umwonapo mpenzi wako, kuwa na furaha wakati wote mnapokuwa pamoja, kupatwa na msisimko wa mapenzi kila umwonapo au usikiapo sauti yake nk.
Lakini kama utamkubali mwanaume kirahisi kwa sababu tu kakukabidhi funguo za nyumba yake wakati huna mapenzi ya dhati ni janga kubwa kwa sababu hivi vitu vya nje vinaweza kutoweka kirahisi, sasa je ikitokea si mapenzi nayo yatakuwa yamekwisha? Kumbuka kwamba kile kilichokupeleka kwake hakipo.
- Amekuwa ni liwazo kwako
Liwazo linaweza kuwa sehemu ya mapenzi lakini hivi vitu haviendi pamoja.
Unaweza kuwa na mwanaume ambaye mnapendana na mnakamilishana hii ni tofauti na mwanaume unayempenda na ukamgeuza kuwa liwazo pale unapohisi upweke.
Jiulize, je ni kwamba mnapendana na mnafurahi kuwa pamoja au unampenda kiasi kwamba huwezi kuishi bila uwepo wake.
Hapa nazungumzia utegemezi wa kihisia, yaani unakuwa king’ang’anizi mpaka mwanaume anakuona kero, badala ya kufurahia mahusiano yenu mwanaume anakuona kuwa ni kero kutokana na kuwa tegemezi wa kihisia.
Hakuna mwanaume anayependa mahusiano ya aina hii anachoka haraka kihisia na atajitahidi kwa kila namna kukukwepa na ikiwezekana kukutosa na kutafuta ustaarabu mwingine jambo ambalo litakuumiza sana.
- Mwanaume king’ang’anizi:
Mwanaume kutongoza na kukataliwa siyo jambo linalowashughulisha sana kwao kujaribu na kukosa ni sehemu ya maisha, lakini lipo suala la kung’ang’ania, yaani mwanaume kumfuatilia mwanamke kwa hali na mali na kujitoa ili kuhakikisha anampata mwanamke anayemtaka.
Huu ni mtego wa mapenzi, kwani kwa mwanaume kung’ang’ania na kufuatilia mwanamke kwa muda mrefu bila kuchoka hata asumbuliwe kiasi gani haimaanishi kwamba mwanaume huyo amempenda mwanamke huyo.
Wakati mwingine ni matamanio tu ndiyo yamemsukuma kutokana na sifa za nje alizo nazo mwanamke huyo.
Kupenda kwa mwanaume kunahusisha zaidi sifa za nje kuliko za ndani na ndiyo maana mapenzi ya aina hiyo hayadumu yanaanza kama kichaa na kuyeyuka ghafla kama kipande cha barafu juani.
Pale mwanamke anapokutana na mwanaume king’ang’anizi na asiyekubali jibu la hapana, kabla ya kukubali ajiulize kama anakubali kuwa na mahusiano na mwanaume huyo kwa sababu amempenda kwa dhati au kwa sababu ya uking’anga’nizi wake?
Kumbuka kwamba wapo baadhi ya wanawake wanaweza kumkubali mwanaume tu kwa sababu amemfuatilia sana, anajiwa na huruma anakubali kuwa na mausiano naye siyo kwa sababu amempenda bali kwa sababu ya huruma.
Ni vyema ukajiuliza kama na yeye atathamini huruma yako au akishapata alichokitaka atakugeuka na kuwa mwiba mchungu kwako? Tafakari na chukua hatua.
Leave a Reply