Mkongwe wa filamu Marekani, Bokeem Woodbine amedai kuwa marehemu rapa Tupac Shakur '2Pac' alimtongoza Lucy Liu wakati utayarishaji wa filamu yao, Gridlock’d (1997) chini ya Universal Pictures na Gramercy Pictures.
Katika mahojiano ya hivi karibuni na mtandao wa Art of Dialogue, Woodbine, 52, amefichua kumbukumbu hiyo ya kuchekesha na ya kupendeza ya jinsi Tupac alivyowahi kujaribu bahati yake kwa Liu ila hakufanikiwa.
Tupac, mkali wa kibao, All Eyez on Me (1996), ingawa anakumbukwa sana kama moja ya mastaa wakubwa na wenye mvuto katika muziki wa Hip Hop duniani, simulizi hii inathibitisha kuwa hata magwiji nao hukwama sehemu wakati fulani.
"Nakumbuka siku moja kambini, Tupac alikuja kugonga mlango wangu. Akanambia, ‘Aisee, kaka, unaendelea?’. Nikamjibu, ‘Nipo tu, nimepumzika hapa.’ Akasema, ‘Sawa Kaka. Nimetoka tu kwenye chumba cha Liu na nimejaribu kumueleza ni kiasi gani nampenda," ameeleza Woodbine.
Hata hivyo, Liu ambaye inadaiwa alikuwa akifanya sana mazoezi kwa kutumia nyenzo za jadi kutokea Ufilipino, alikuwa makini zaidi kwenye kazi yake ya uigizaji kambini hapo kuliko mvuto wa Tupac.
Woodbine anasema kwa bahati mpango huo haukuenda kama alivyotarajia Tupac, rapa alisainiwa na lebo ya Death Row Records baada ya kutoka jela mwaka 1995 huko New York.
"Nilikua tu nacheka," anasemma Woodbine na kuendelea. "Nikamuuliza, ‘Ilikuwaje? mambo yalienda sawa?’ Akasema, ‘Hapana, mbinu zangu hazijafanikiwa kumshawishi'. Nikamwambia, ‘Usijali, Kaka, huwezi kupata kila kitu,'" alisema Woodbine.
Tupac alimwambia Woodbine kwamba Liu hakuonyesha kuvutiwa naye kimapenzi kivyovyote vile bali alitaka mazungumzo yao yajikite katika kazi na utamaduni wake wa kufanya mazoezi kwa nyenzo za jadi kama kuzungusha fimbo.
"Nilimuuliza Tupac au labda Liu hakuelewa kabisa alichokuwa anamaanisha?. Lakini alinijibu kuwa, 'Ndio, unajua nataka kumfahamu zaidi ila anachotaka tuzungumzie ni kuhusu kuzungusha tu hizi fimbo zake,'" alieleza Woodbine.
Woodbine ambaye pia alionekana katika video ya wimbo wa Tupac, I Ain’t Mad At Cha (1996), anabaki kuwa mmoja wa watu wachache wenye hadithi binafsi na za kuchekesha kutoka kwa rapa huyo ambazo wengi hawakuwahi kuzisikia.
Hata hivyo, pamoja na kuchemka huko, Liu katika mahojiano yake na The Sydney Morning Herald mwaka 2023, alikumbuka mambo mazuri kuhusu Tupac aliyefariki Septemba 13, 1996 kwa kupigwa risasi, wakati huo akiwa na umri wa miaka 25.
"Tupac alikuwa mtu mzuri na tulifurahia muda wetu pamoja. Ni jambo la ajabu kufikiria kwamba sasa hayupo tena nasi," alisema Liu, mwanamke wa pili mwenye asili ya Amerika na Asia kutunukiwa nyota ya heshima ya Hollywood Walk of Fame.
Ikumbukwe filamu ya Gridlock’d, iliyotolewa baada ya kifo cha Tupac mnamo Januari 1997, ilikuwa moja ya kazi zake za mwisho za uigizaji. Ilipata mafanikio kiasi katika mauzo ya sinema na ilipongezwa sana kwa kuonyesha uwezo wa rapa huyo kama mwigizaji.
Filamu hiyo yenye maudhui ya vichekesho na uhalifu, ilisimulia maisha ya vijana wawili waraibu wa dawa za kulevya aina ya heroin waliokuwa wakijaribu kuacha, huku wakipambana na urasimu tata wa mfumo wa maisha mtaani.
Na miezi sita baada ya kifo cha Tupac, hasimu wake kimuziki, The Notorious B.I.G naye aliuawa kwa kupigwa risasi mnamo Machi 9, 1997. Wote walikuwa katika vita vilivyokuwa vinaendelea katika ulimwengu wa Hip Hop kati ya wasanii wa East Coast na West Coast.

Leave a Reply