Msemo wa msanii mkongwe wa Singeli Msaga Sumu, kuwa kila msanii wa nyimbo za aina nyingine ipo siku atakuja kuimba Singeli, umeanza kuonekana.
Baada ya wasanii Zuchu, Jux, Diamond Platnumz, Harmonize, Mbosso, Ali Kiba na wengine kuimba Singeli, Jay Melody ametangaza kuachia wimbo wake mpya wa Singeli hivi karibuni.
Jay Melody baada ya kutangaza kwenye akaunti yake ya Instagram muda wowote ataachia wimbo wenye mahadhi ya Singeli, gazeti hili lilimtafuta kujua kipi kimemsibu kufanya maamuzi hayo na alisema;
"Singeli ni muziki ambao naupenda sana, mi nimehudhuria matamasha na nimeshaenda klabu nyingi yaani ikishafika muda unaona watu wamechoka ila ikipigwa wimbo wa Singeli kila mtu anaamka, kwa hiyo, hiyo ndiyo shauku yangu ilipotokea kutaka kufanya Singeli," alisema Jay Melody.
Aidha Jay Melody aliongeza, "Muziki wa Singeli unapendwa sana Tanzania, hivyo nimeona vyema kuwapa mashabiki wangu ngoma watakayofurahia kwa mda mrefu na kuonyesha hata upande huu nipo vizuri katika uimbaji."

Leave a Reply