Jay Melody alivyopenya katika msitu mnene kimuziki!

Jay Melody alivyopenya katika msitu mnene kimuziki!

Staa wa Bongo Fleva, Jay Melody ni miongoni mwa wasanii waliofanya vizuri zaidi katikati kipindi cha miaka miwili iliyopita, hiyo ni baada ya ujio wake mpya wa tangu Januari 2021 ambao umemtakatisha zaidi.

Hata hivyo, Jay Melody aliyetoka rasmi kimuziki na wimbo wake, Goroka (2018) na kisha kupotea, kurejea kwake tena na kuushika mchezo imemlazimu kupinya katika msimu mnene wa kimuziki wenye vizingiti vitatu.

Utakumbuka baada ya kurejea ameweza kuandika rekodi kama msanii wa kwanza nchini Tanzania na Afrika Mashariki kwa nyimbo zake kusikilizwa (streams) mara milioni 200 katika mtandao wa Boomplay bila kutoa albamu wala EP.

Katika mahojiano na Mwananchi Scoop, Jay Melody ambaye ni mshindi wa Wimbo Bora wa Mwaka (Nakupenda), kutoka tuzo za muziki Tanzania (TMA) 2022, ameelezea mtazamo wake kuhusu mafanikio yake baada ya ujio mpya bila ya kuwa na mambo yafuatayo;.

1. Bila Lebo
Asilimia kubwa ya wasanii Bongo wanaofanya vizuri na kupata namba kubwa za mauzo katika majukwaa ya kidigitali ya kusikiliza na kuuza muziki wapo chini ya rekodi lebo za wasanii wenzao au wadau lakini kwa Jay Melody mambo ni tofauti kabisa.

Anafanya vizuri na kupata namba kubwa hata kuwazidi wasanii waliyopo katika lebo kubwa, mathalani wimbo wake, Nakupenda(2022) umefikisha 'streams' milioni 75.8 Boomplay na ndio wimbo pekee wa Bongo Fleva uliosikilizwa zaidi katika jukwaa hilo.

Kuhusu hilo, Jay Melody amesema anaweza kufanya kazi na lebo yoyote pale atakapoona kuna nafasi ya kukua zaidi kimuziki na kibiashara ila sio jambo la kukimbilia kwake kama anavyofanya muziki wake.

"Tamaa yangu ni kufanya kazi na kufanikiwa, mimi ni mfanyabiashara naweza kufanya kazi na msanii yeyote na wa lebo yoyote ambayo itakuwa tayari au itakuwa biashara kwangu na mimi nitaona kitu kwao." amesema.

"Mimi sio msanii wa kusema nianze kuwa na tamaa na lebo, mimi na tamaa na mafanikio, na tamaa ya kufanya kazi iende vizuri, kwa hiyo inapotokea mtu yeyote anataka ushirikiano na mimi kwenye kufanya kazi iendee inawezekana lakini sina tamaa ya kusema niende kwenye lebo yoyote." amesema Jay Melody.

Utakumbuka Jay Melody amekulia kimuziki Tanzania House of Talent (THT) ambapo ndipo alipewa jina hilo na Ruge Mutahaba, anasema THT kwa sasa haihusiki na usimamizi wa muziki wake, walimfundisha muziki na tayari amehitimu kama wenzake.

"Nipo mwenyewe najitegemea, nafanya vitu vyangu, sipo ndani ya THT, pale ni kama Chuo kimenifundisha muziki, ni watu ambao bado tunashirikiana lakini sio kwamba nipo pale kama mwanafunzi." amesema na kuongeza.

"Ukiwa pale bado wewe ni mwanafunzi wa THT, kama Barnaba huwezi kusema yupo THT, alikuwepo THT sasa hivi anafanya mambo yake." amesema Jay Melody.
Ukiachana na Jay Melody, wasanii wengine waliowahi kupita THT ni Mwasiti, Barnaba, Linah, Amini, Ditto, Nandy, Jolie, Maunda Zorro, Benson, Ruby, Marioo, Vumi, Recho, Ibrah Nation, Mataluma, Makomando, Beka Ibrozama, Ally Nipishe n.k.
2. Bila Kiki
Kwa Jay Melody muziki wake ndio unamtambulisha zaidi kuwa yeye ni nani na sio matukio mengine nje ya kazi yake, anatoa nyimbo zake bila kiki na zinafanya vizuri, anasema ndio mtindo aliyoamua kuuza sana yake.

Ikumbukwe nyimbo alizotoa tangu mwaka 2021 kwa asilimia kubwa zimefanya vizuri huku akishirikishwa zaidi, moja ya nyimbo alizoshirikishwa na kubamba ni 'Puuh' wake Billnass hadi rapa huyo kushinda tuzo ya TMA 2022.

"Unajua kwenye tasnia kila mtu ana jinsi ambavvyo anaifikisha sanaa yake kwenye jamii, inawezekana hizo kiki ni sanaa kwa watu wengine, ila kwa ujumla wake mimi naamini kila mtu ana jinsi anavyouzaa sanaa yake," amesema Jay Melody.

Hata hivyo, Jay anasema tasnia lazima iwe na vitu vyake ili ichangamke lakini pia kuchangamka haimaanishi kuwe na kiki za udhalilishaji, ukiukwaji wa haki za binadamu na sheria za nchi.

"Zinatakiwa kiki ambazo zina mantiki, zinazoeleweka na zinazosaidia kutengeneza, kukuza na kuchangamsha tasnia na kuwafanya watu wawe tayari, yaani wasanii wazungumzeke kwenye mambo mazuri." amesema na kuendelea.

"Siku zote hatuwezi kuimba tu, hiyo haitoshi, tunatakiwa tufanye na vitu vingine ambavyo vyenyewe ni kiki kwa ajili ya lengo la kikazi sio kupata umaarufu na kudhalilishana." amesema.

"Mfano inaonekana wasanii wana bifu halafu wakaja wakafanya kolabo au wakaandaa shoo, hiyo ni stori nzuri kuzungumzika kwa wasanii kwamba jamaa walikuwa wana bifu ila wameenda kubishana kwenye wimbo au kwenye shoo, hiyo italeta maana zaidi na kiki itakuwa sio kitu kibaya." amesema Jay Melody.

Utakumbuka Jay Melody ameandika nyimbo maarufu za wasanii wenzake kama Nandy (Kivuruge, Njiwa, Hallelujah na Do Me) na Benson (Hauzimi) n.k.

3. Bila Amapiano
Jay Melody alirejea wakati muziki wa Amapiano kutokea Afrika Kusini umetawala katika Bongo Fleva ila akawa na ujasiri wa kuachia wimbo wake, 'Huba Hulu' wenye mahadhi ya Pwani, huku ukichukua vionjo vya wimbo, El Habayib wake Amr Diab.

Hadi sasa nyimbo zilizotoka baada ya ujio wake mpya na kufanya vizuri zaidi kimauzo sio za Amapiano, nyimbo hizo ni Huba Hulu (2021), Najiweka (2021), Sugar (2021), Nakupenda (2022), Nitasema (2023), Sawa (2023) na Mbali Nawe (2023).

"Utofauti pia unasababisha watu kupenda kazi, unajua hapa katikati kumeibuka muziki aina ya Amapiano ambao umekuwa gumzo sana, kila mtu aliimba kiasi kwamba wananchi walitaka kusikia vitu tofauti mbali na Amapiano." amesema.

"Labda watu walikuwa wanategemea Jay anaweza kuja na Amapiano na vitu kama hivyo lakini mimi nikaja na aina nyingine ya muziki ndio maana watu ikawa rahisi kukimbilia huko baada ya labda kuchoshwa na Amapiano." amesema Jay Melody.

Wakati wasanii wengine wakifikiria ni jinsi gani watatoka na ngoma kali za Amapiano, Jay Melody anasema wazo la kufanya wimbo, Huba Hulu alilipata akiwa visiwani Zanzibar na kuamua kuweka vitu vya huko vilivyomsaidia kupenya katikati ya Amapiano.

"Hata ukisikiliza huo wimbo una maneno ambayo yana Uzanzibari fulani hivi, kwa mfano biriani ya mama Cholo, kwa hiyo nilikuwa naiweza sana Zanzibar, yale mapenzi ya kule ndio maana ukisikiliza una mahadhi ya huko, kama Uarabu fulani,' anasema Jay Melody.

Ikumbukwe muziki wa Amapiano ulianza mwaka 2012 huko Gauteng, Afrika Kusini ila kumekuwa na mjadala ni wapi hasa asili ya muziki huo nchini humo, wapo wanaodai ulianzia katika vitongoji vya Johannesburg - Soweto na kisha kusambaa Afrika.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post