Fahamu kuhusu kiharusi

Fahamu kuhusu kiharusi

Kiharusi ni nini?

Kiharusi cha muda mfupi, pia huitwa Transient ischemic attack (TIA), Ni hali ya mfumo wa neva unaotokea ghafla na hudumu kwa muda mfupi. Hii husababishwa na mishipa ya damu kwenye ubongo kuziba kwa muda mfupi.

Matibabu hulenga kuzuia hali hii kujirudia au kupata kiharusi kwa kufanya damu iwe nyembamba na kutibu hali ambazo huongeza uwezekano wa kupata kiharusi. Ingawa hali hii haisababishi madhara ya kudumu kwenye ubongo, ni onyo kuwa kiharusi kinaweza kutokea hivi karibuni. Watu ambao wamepata hali hii wanapaswa kuongea na daktari kuhusu njia za kuzuia kiharusi.

Dalili za kiharusi (Stroke)

Ugonjwa wa stroke humpata mtu ghafla na dalili hutokea kwa muda mfupi sana. Dalili kuu za ugonjwa huu ni:

 • Kuchanganyikiwa

 Mtu akipata shida ya kuongea na kuelewa anachoambiwa.

 • Maumivu ya kichwa

Maumivu haya yanakwenda pamoja na kupoteza fahamu kwa vipindi na kutapika.

 • Ganzi

Katika viungo vya uso, mkono na mguu na hasa vikiwa vya upande mmoja wa mwili.

 • Kupata shida ya kuona kwa jicho moja au yote
 • Kupata shida ya kutembea vikichanganyika na kizunguzungu na kukosa mpangilio wa matendo ya mwili

Athari za kiharusi zinaweza kuwa ni za muda mrefu. Kulingana na muda uliopita kabla ya kuugundua na kuutibu ugonjwa huu, mtu anaweza kupata ulemavu wa muda mfupi au wa kudumu. Pamoja na madhara ya stroke kama yalivyoorodheshwa hapo juu, mgonjwa wa stroke anaweza pia kupata yafuatayo:

 

 • Msongo wa mawazo
 • Maumivu kwenye mikono na miguu yanayoongozeka baada ya viungo hivyo kufanya kazi au kutokea mabadiliko ya hali ya hewa.
 • Kupooza au udhaifu wa upande mmoja wa mwili
 • Kupata shida katika kufanya matendo ya kuonyesha hisia za mwili
 • Kushindwa kumudu matumizi ya kibofu cha mkojo au viungo vya njia ya haja kubwa

Utambuzi wa kiharusi

Daktari wako atakuuliza wewe au mwanafamilia kuhusu dalili zako na ulichokuwa ukifanya zilipotokea. Watachukua historia yako ya matibabu ili kujua sababu za hatari yako ya kiharusi.

Vipimo vya kutambua viharusi

Unaweza kupitia vipimo mbalimbali ili kusaidia zaidi daktari wako kujua kama umepata kiharusi au kuondoa hali nyingine. Mitihani hii ni pamoja na:

 • Vipimo vya damu

Daktari wako anaweza kuchukua damu kwa vipimo kadhaa vya damu. Vipimo vya damu vinaweza kuamua; Viwango vya sukari yako ya damu ikiwa una maambukizi viwango vya platelet yako (jinsi damu yako inavyoganda kwa kasi)

 • MRI na CT scan
 • Electrocardiogram (ECG au EKG)
 • Angiogram ya ubongo
 • Ultra ya carotid
 • Echocardiogram 

Vitu vinavyochangia mtu kupata kiharusi

 1. Ugonjwa wa Shinikizo kubwa la damu (presha)
 2. Uvutaji sigara
 3. Ugonjwa wa kisukari
 4. Magonjwa ya moyo hasa ugonjwa wa mtetemo wa moyo (atrial fibrillation)
 5. Tatizo la mafuta mengi kwenye damu (Lehemu au cholesterol)
 6. Uzito uliopitiliza
 7. Unywaji wa pombe uliokithiri
 8. Kutokufanya mazoezi

Uchaguzi wa matibabu

Matibabu hutegemea ni aina gani ya kiharusi. Kila aina ya kiharusi ina matibabu maalumu na haitakiwi kuyachanganya. Tiba ya aina moja ya kiharusi inaweza kusababisha kifo cha mgonjwa wa aina ya nyingine. Daktari atapaswa kufanya CT scan ili kujua kwa uhakika ni aina gani kabla hajatoa matibabu

 

 • Matibabu ya kiharusi kinachosababishwa na kuziba kwa mishipa ya ubongo. Lengo la matibabu ni kurejesha mtiririko wa damu kwenye ubongo wa mgonjwa haraka iwezekanavyo. Matibabu ya haraka sio tu yanaongeza uwezekano wa kuokoa maisha, lakini pia yanaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa matatizo/athari zitokanazo na kiharusi. 

Madawa: Dawa kama aspirini, warfarin au heparini, zinaweza kutolewa kwa haraka baada ya kiharusi ili kupunguza uwezekano wa kuwa na kiharusi kingine.

Tissue plasminogen activator (TPA) ni dawa yenye nguvu sana inayosaidia kuvunja vunja madonge ya damu yaliyoganda na kuziba mishipa ya damu kwenye ubongo. Dawa hii husaidia watu wengi kupona kabisa na ni marufuku kutumiwa na watu wenye kiharusi kinachosababishwa na kuvuja damu kwenye ubongo.

Upasuaji: Upasuaji unafanyika kufungua ateri zilizoziba.

Carotid endarterectomy: Katika operesheni hii, daktari wa upasuaji hufungua ateri ya karotidi iliyoziba na kuondoa utando ulioiziba. Operesheni hii inaweza kupunguza hatari ya mgonjwa kupata kiharusi.

Angioplasty na stents: Katika operesheni  hii daktari hujaribu kuurekebisha mshipa wa damu ulioharibika pia huweka bomba ndogo kupanua sehemu ya ateri iliyopungua upana ili kuruhusu damu kupita. Stent hubaki ndani ya mwili kuzuia kujirudia kwa tatizo.

 • Matibabu ya kiharusi kinachosababishwa na kuvuja damu kwenye ubongo. Viharusi vingi vinavyosababishwa na kuvuja damu kwenye ubongo huhusishwa na perema (aneurysm) na matatizo ya kimuundo ya mishipa ya damu. Upasuaji hupendekezwa kutibu haya matatizo au kuyazuia. Operesheni ya kawaida hupunguza ukubwa wa perema na kurekebisha matatizo ya kimuundo ya mishipa ya damu. Kurejesha na kukarabati mwili

Daktari atakusaidia kurejesha ujuzi ambao umepotea baada ya shambulio, kama vile kutembea, kuwasiliana au uratibu. Ukarabati ni muhimu sana kwa sababu huamua ubora wa maisha atakayoishi mgonjwa yeye mwenyewe na familia yake baada ya kutoka hospitalini.

Imeandaliwa na Mark Lewis


Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Detricia Pamba

A Digital Journalist, Content Creation Executive at Mwananchi Communications Ltd and Chief Editor of Mwananchi Scoop. I'm also writes stories around Technology, every Wednesday on Mwananchi Scoop. My other famous segments on Mwananchi Scoop include LISTI and WHO’S HOT.


Latest Post