Dr. Almasi alivyoukataa uzee, ajifananisha  na Diddy, Snoop Dogg

Dr. Almasi alivyoukataa uzee, ajifananisha na Diddy, Snoop Dogg

Kuzeeka ni mpango wa Mungu ila kuchoka ni kujitakia kauli hii ameitoa Mwigizaji Steven Charles Almasi maarufu kama Dr. Alsmasi baada kuzungumza na Mwananchi Scoop na kufunguka mengi kumuhusu yeye na kazi yake.

Dr. Almasi aliyetambulika kwa kuvaa uhusika katika filamu na Tamthilia mbalimbali ameeleza kuwa licha ya kuwa na familia yenye watoto watatu na wajukuu lakini bado ameendelea kujikubali na kuishi katika mtindo wake mwenyewe.

“Mimi nina watoto na wajukuu lakini sijaruhusu kuchoka bado najikubali kutokana na mtindo wangu wa maisha kwa sababu ukiangalia katika jamii yetu wazee wengi wamejichagulia kuchoka na kuchakaa sasa mimi kwangu ni tofauti sijachagua kuchakaa.

“Walio wengi wanaamini ukiwa mzee au umri umeenda basi hutakiwi kuvaa vizuri, kujipulizia pafyume na kwenda na dunia inavyoenda hususani kwa zama za sasa” Amesema.

Kutokana na mwonekano wake amesema unampatia deal nyingi za mambo ya fashion huku akidai kuwa anawatazama zaidi Snoop Dogg, P Diddy, R Kelly
“Watu wanatakiwa wajue mimi siishi katika mipaka ya Tanzania au life style ya hapa kwa sababu mimi ni fashionist ambaye naangalia mitindo na mionekano kutoka njee hususa kwa wasanii wenye umri kama wa kwangu ambao tumeachana miaka miwili au mitatu kama akina Snoop Dogg, P Diddy, R Kelly” Anasema Dr. Alimasi

Licha ya kuzungumzia mwonekano wake hakuacha kuelezea namna soko la uigizaji Tanzania linavyoenda kwa kasi kutokana na wakati.
“Sasa hivi soko la ugizaji kwa hapa Tanzania linaenda kwa kasi sana kutokana na utandawazi wa mitandao na ndiyo maana unaona kuna thamthilia nyingi tofauti na zamani ambapo kazi zilikuwa zinawekwa kwenye DVD au mikanda.” Anasema.

Kipi kinamfanya kuwa bora katika ugizaji?
Ubora au pekee wa mwigizaji unatokana na kitu binafsi alichonacho msanii anapowasilisha kazi yake ya sanaa kwa upande wa Almasi amedai kuwa hajawahi kusemwa vibaya katika kazi yake zaidi ya watu kupenda swaga zake na mtindo wa pekeyake katika sanaa.

“Namshukuru Mungu tokea nilipoanza sanaa sijawahi kuzungumziwa vibaya katika kazi zangu zaidi ya kupewa maua yangu siku hadi siku kwa sababu ya watu wanapenda ‘swaga’ zangu namna ninavyocheza katika filamu kama uhalisia wa kweli.

“Wakati nilipokuwa mtoto hii sanaa ninayofanya sasa hivi ilionekana mapema sana sema wazazi wangu walikuwa wananiona kama mtukutu nisiyesikia kumbe mimi ni staa wa baadaye na hatimaye sasa hivi napata kongole nyingi kutoka kwa mashabiki zangu” Anasema.


Afunguka hakutamani kuwa msanii

Dr. Almasi anaturudisha nyuma kuwa hakutamani kuwa msanii hapo awali japo alikuwa anaishi maisha ya kisanii ambapo mwaka 2017 aliomba kuwa kwenye filamu ya ‘A lot of money’ wakati huo alikuwa najishughulisha na masuala ya hoteli tu

“Ni Mungu tu amebariki mpaka nimefikia hapa kwa sababu ingawa nilikuwa naishi maisha ya usanii ila mwanzoni sikutamani kuwa msanii ilipofika mwaka 2017 nikaomba nionekane katika filamu hapo ndiyo safari yangu ya ugizaji ilipoanzia kabla ya hapo nilikuwa najishughulisha na masuala ya hoteli” Anasema mwigizaji huyo.


Mambo gani anazingatia kabla ya kufanya kazi ya mtu?
Ni kawaida kabla ya mtu kufanya kazi fulani kuangalia maslahi anayoweza kuyapata kutokana na kazi anayofanya, kwa upande wake Dr. Almasi ameeleza kuwa anapotaka kufanya kazi ya sanaa na mtu huwa anaangalia kama stori itambeba ama itamuua ubora wake.

“ Unajua watu wanapenda kufanya sanaa ilimradi tu ameitwa kwenye kazi na director fulani basi anafanya lakini mimi ninapoenda kufanya kazi ya mtu kwanza huwa naangalia vitu mbalimbali kama stori ya hiyo filamu itanibeba ama itaniangusha? pia Quality ya vifaa kwa sababu mimi kamera za harusi siwezi ku-shoot, na kiwango cha pesa ninachokitaka mimi mwigizaji kulingana na hadhi yangu”. Anasema

Dr. Almasi ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 60 amewahi kushiriki katika filamu na tamthilia mbalimbali zikiwemo Dosari, Olema, Toboa Tobo, Nia, Uhuru Una Gharama Zake, Salamu, Chausiku, Sarafu, Bongo Dar es Salaam na nyingine nyingi.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Asha Charles


Latest Post

Latest Tags