Pawa ya Mbosso ilivyoanza kuhiti, Baba Levo akachomoka alipokuwa na kusema Diamond alimsaidia Mbosso kuandaa hiyo ngoma. Watu wakabisha wakasema Mbosso tunamjua dogo fundi. Dogo masta. Kusaidiwa kuandaa ngoma sio vitu vyake.
Baba Levo akasimama tena akasema msibishe jamani nina ushahidi nitautoa. Watu tukamdharau. Tukaendelea kuinjoi Pawa na ngoma zingine kwenye EP ya Room Number 3.
Wiki mbili tatu zikakataa mara ghafla Baba Levo akazinduka na kuposti video ikimuonyesha Diamond, Mbosso, produzya S2kizzy na wadau wengine wakiwa studio wakiandaa ngoma ya Pawa. Na kwenye video hiyo Diamond anakwenda kwenye kipaza sauti na kuimba kana kwamba anamuonyesha Mbosso jinsi ya kutambaa na biti.
Baada ya video ile watu wakawaka sana. Wengine wakasema Wasafi wana roho mbaya hawataki kuona wasanii wao wa zamani wakifanikiwa nje ya lebo yao.
Wengine wakasema Diamond muoga sana akiona msanii wake anataka kumvuka anamtengenezea figisu. Kwa kifupi watu walikuwa wanaona mabosi wa zamani wa Mbosso wamezingua.
Baadaye Diamond akaibuka na kuposti kwamba hajamteua mtu yeyote kuwa msemaji wa maisha yake ya kitaaluma wala ya kifamilia kwa hiyo mtu yeyote anayezungumza kuhusu yeye amejisikia tu kuzungumza tusimzingatie na ikitokea umejisikia kumzingatia hilo litakuwa ni tatizo lako.
Binafsi namuamini Diamond anaposema hajamteua mtu, lakini pia naamini ameruhusu watu kama kina Baba Levo kutembea kifua mbele wakijifanya wao ni wasemaji wa maisha yake.
Si mara moja, si mara mbili Baba Levo amewahi kutoa taarifa kuhusu Diamond, watu wanaomzunguka Diamond ikiwemo familia, lebo na kadhalika.
Kwa mfano, hata hiyo Mbosso kutoka WCB alianza kuisema yeye, Lava Lava kutoka kwenye lebo pia tulianza kuisikia kwake Baba Levo.
Hii inamaanisha kwamba Baba Levo ni mtu wa kuaminika. Ni mtu mwenye kutoa taarifa sahihi kuhusu Mondi.
Kina Juma Lokole wameshazungumza sana kuhusu bosi wao huyo hasa kwenye ukurasa wake wa kimapenzi. Walishatuambia sana stori kuhusu Hamisa asivyopendwa na Mama Diamond.
Walimchokonoa sana Zuchu kiasi kwamba kuna wakati walimkwaza mpaka akatishia kujitoa kwenye lebo.

Leave a Reply