Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kitaendelea kupiga vita sera za udini, ukanda na ukabila lakini hakitaacha kutowatambua machifu na watemi hivyo kinawapongeza umoja wa machifu Tanzania kwa kumsimika Rais Samia Suluhu Hassan uchifu mkuu wa machifu wote nchini.
Pia Chama hicho kimesema pamoja na kwamba sera za TANU na baadae CCM kutoruhusu tawala za kichifu na kitemi hiyo haina maana koo za kichifu na mchango wao kwa nchi yetu zisitambuliwe.
Ufafanuzi huo umetolewa jana na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka aliyetakiwa kutoa maelezo iwapo Rais Samia kusimikwa uchifu mkuu ni kushabikia ukabila na kueleza wanaokosoa kitendo hicho wanatakiwa wafanye rejea ya historia kabla ya kusema hayo.
Shaka alisema hata Rais wa kwanza Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere ambaye ndiye aliyekuwa mstari wa mbele kupiga vita himaya za kichifu na kukomesha ukabila ili kujenga misingi imara ya umoja wa kitaifa alikuwa akivikwa mavazi ya kimila na kupewa hadhi za uchifu kwenye makabila yote alipokuwa Rais wa nchi yetu.
Alisema wanaodai kitendo cha Rais Samia kupewa hadhi ya uchifu mkuu wa machifu wote nchini ni kushabikia ukabila waelewe kuwa hiyo ni hadhi inayotolewa kwa watu muhimu na waliotoa mchango mkubwa kwenye jamii zao kama ile itolewayo na vyuo vikuu duniani kote ikiwemo udaktari wa heshima.
"Hatutashabikia ukabila, udini wala ukanda lakini muhimu ikafahamika CCM hakitabeza utamaduni, mila na desturi zetu ambazo ni chanya ikiwemo kuutambua utemi, uchifu na viongozi wa mila kwani kufanya hivyo sio kuendeleza ukabila" Alisema Shaka
Aidha katibu huyo mwenezi alisema hata baada ya mwalimu Nyerere kukomesha ukabila alionekana akivikwa mavazi ya kitamaduni na kiasili katika makabila mbalimbali, mzee Ali Hassan Mwinyi, Hayati mzee Benjamin Mkapa, Dkt Jakaya Kikwete na hayatI Dkt John Magufuli wote walitunukiwa heshima hizo.
"Kwa kuwa wapo washindani wetu wa kisiasa na wamekosa hoja basi watakosoa kila kitu ambacho CCM na viongozi wake itafanya. Hata mwanasiasa Theresa Ntare wa kabila la Waha huko kigoma alitambuliwa kwa heshima yake na akaitwa Mwami Ntare hata baada ya uhuru." Alisema Shaka
Shaka alisisitiza kuwa CCM wakati wote itatambua, itathamini na itaenzi mchango wa machifu na watemi kama vile kina Mangi Meli, Chifu Kimweri wa Usambara, Mtemi Mirambo wa unyanyembe, Makunganya, Kinjikitile Ngwake na kina chifu Songea, Nkossy na Mkwawa ambao walikuwa mstari wa mbele kupigania uhuru na ukombozi wa Mwafrika dhidi ya wakoloni.
Pia katibu huyo alisema machifu na watemi wameshiriki juhudi za mapambano kupinga tawala za kijerumani na kiingereza kwa kuwaeleza kinagaubaga waondoke ili wajitawale wenyewe.
"Hatuwezi kuzungumzia uhuru wa Tanganyika au mapinduzi ya Zanzibar bila kutambua na kuthamini mchango wa machifu, watemi, viongozi wa kijadi na kimila.
Ndiyo maana katika kuenzi mchango wao yapo maeneo mengi ya umma yaliyopewa majina yao kama vile kuna mitaa imeitwa Kimweri, Makunganya; shule zinazoitwa Mkwawa, Mirambo nk" alieleza Shaka
Hata hivyo CCM wamesifu uamuzi wa machifu na watemi kuamua kumsimika uchifu mkuu Rais Samia mkoani mwanza kutokana na umahiri wa uongozi wake katika kutetea maslahi ya Taifa.
Leave a Reply