Hatimaye mwanamuziki Zuchu ameachia albamu yake ya kwanza tangu ametoka kimuziki miaka minne iliyopita kufuatia kusainiwa WCB Wasafi, akiwa ni msanii wa saba baada ya Harmonize, Rayvanny, Rich Mavoko, Queen Darleen, Lava Lava na Mbosso.
Hata hivyo, awali Zuchu alishatoa EP, I Am Zuchu (2020) yenye nyimbo saba akiwashirikisha Mbosso na Khadija Kopa, ilifanya vizuri ikikaa tano bora kwenye chati za Boomplay kwa wiki 75, na zile za YouTube Music kwa wiki zaidi ya 100.
Zuchu ameenda kuweka rekodi ya kuwa msanii wa kwanza wa kike wa Bongofleva kutoa albamu mwaka huu, kwa ujumla anaungana na kina Roma (Nipeni Maua Yangu), Jay Melody (Therapy), Young Lunya (Mbuzi), Stamina (Msanii Bora wa Hip Hop), Marioo (The God Son), Rayvanny (The Big One) .
D Voice aliyetoka na kibao chake, Kuachana Singapi (2021), amesikika katika wimbo wa Zuchu ‘Hujanizidi’ ambao ndio wa mwisho katika albamu hiyo ambayo imeshirikisha wasanii watatu tu wa WCB Wasafi, wengine ni Diamond na Lava Lava.
Hivyo ndani ya miaka miwili tu, wawili hao wametoa nyimbo nne pamoja, kwa matokeo hayo D Voice anakuwa msanii wa pili Bongo aliyeshirikiana mara nyingi zaidi na Zuchu baada ya Diamond huku Mbosso na Rayvanny wakifuatia.
Hata hivyo katika albamu hiyo licha ya kusikika wasanii mbalimbali wa nje na ndani ya Tanzania mwimbaji wa Afrobeats kutokea Nigeria, Yemi Alade amesikika katika wimbo ‘Lollipop’ ikiwa ni mara yake ya pili kushirikishwa na msanii wa Tanzania baada ya Harmonize mwenye albamu tano.
Kipindi Harmonize akiwa bado WCB Wasafi alitoa EP, Afro Bongo (2019) yenye nyimbo nne na kuwashirikisha Diamond, Burna Boy, Mr. Eazi na Yemi Alade aliyesikika katika wimbo ‘Show Me What You Got’ uliofanya vizuri.
Utakumbuka Yemi Alade ambaye ni msanii wa kwanza wa kike Afrika kutazamwa (views) zaidi ya mara milioni 100 YouTube, alikuwa miongoni mwa Majaji katika shindano la Tecno Own The Stage 2015 ambalo Zuchu alishiriki pia.
Baada ya D Voice kumshirikisha Zuchu katika nyimbo zake tatu, BamBam (2023), Nimezama (2023) na Nani (2024), awamu hii ikawa ni zamu yake ambapo Zuchu amempa shavu katika albamu hiyo, Peace and Money (2024).
Zuchu msanii wa kwanza wa kike kutoa albamu 2024
Leave a Reply